Wednesday, December 24, 2008

Mkapa hachunguzwi

 TAKUKURU yasema


Rais mstahafu, Benjamin William Mkapa


Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, hachunguzwi kwa kosa au tuhuma yoyote ya jinai, imeelezwa. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Dar es Salaam jana, ilisema uvumi kuwa Rais huyo mstaafu anachunguzwa na vyombo vya dola ikiwamo taasisi hiyo, hauna ukweli wowote. 

Tamko la taasisi hiyo limekuja huku kukiwa na uvumi katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa kiongozi huyo anachunguzwa na Takukuru, kutokana na vitendo vingi vya ufisadi vinavyodaiwa kufanywa wakati wa uongozi wake. 

Tayari mawaziri wawili Basil Mramba na Daniel Yona waliowahi kushika nyadhifa nyeti katika Serikali ya Awamu ya Tatu ukiwamo uwaziri wa Fedha, wameshafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7. 

Lakini pia baadhi ya watuhumiwa katika kesi za kuchota mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT), ambao wamefikishwa mahakamani, wanadaiwa kufanya wizi huo kati ya mwaka 2004 na 2005 kipindi ambacho Rais Mkapa alikuwa madarakani. 

Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kipwani alisema jana kuwa, taasisi yake haina uwezo wa kumchunguza kiongozi huyo kutokana na Katiba ya nchi kutotoa nafasi hiyo katika Ibara ya 46 (3) ya Katiba ya Tanzania. Kapwani alieleza kuwa taasisi yake inaheshimu Katiba na ina wajibu wa kuilinda na kuheshimu matakwa hayo ya Katiba. 

“Takukuru inawafahamisha wananchi kwamba uvumi huu hauna ukweli wowote, hatumchunguzi kiongozi huyu kwa kosa au tuhuma yoyote ya kijinai,” alisema. “Ni kwa msingi huu, Takukuru imeona ni vyema kuwafahamisha wananchi ukweli dhidi ya uvumi huu. 

Tukumbuke wakati wote kwamba taifa letu lina Katiba ya Nchi ambayo imeweka misingi mikuu ya kuendesha nchi yetu, haki na wajibu wa kila Mtanzania. Katiba kama sheria mama imeweka pia mipaka katika kushughulikia mambo mbalimbali ya nchi na kwa mantiki hii, haina budi kuheshimiwa wakati wote.” 

Kifungu hicho cha Katiba kinaeleza kuwa “Ni marufuku kumshitaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la kumdai mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo lolote alilofanya yeye kama Rais wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais kwa mujibu wa Katiba hii.” 

Kapwani alisisitiza kuwa Takukuru itaendelea kufanya kazi zake kwa mujibu wa Katiba na sheria ya nchi na sio vinginevyo. Katika siku za karibuni, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vinaripoti kuwa Mkapa anachunguzwa na Takukuru licha ya kuwa ana kinga ya kutoshitakiwa. 

Vyombo hivyo vimekuwa vikimwandama kwa madai kuwa ufisadi mkubwa umefanyika katika kipindi ambacho alikuwa madarakani. Watu wenye mtazamo huo wamekuwa wanataka kiongozi huyo aondolewe kinga na afikishwe mahakamani kujibu tuhuma mbalimbali za ufisadi. 

Wiki hii, Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo alieleza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi katika kikao kijacho cha Bunge kuomba kifungu kinacholinda marais wastaafu kutoshitakiwa kirekebishwe. Mkapa anatajwa katika tuhuma kuhusu ununuzi wa ndege ya Rais, ununuzi wa rada, wizi wa mabilioni ya EPA, uuzaji wa nyumba za serikali, mikataba yenye utata kama ya NetGroup, Alex Stewart na ubinafsishaji wa mgodi wa Kiwira.


Kutoka gazeti la HabariLEO

No comments: