Bosi wa Richmond
aburuzwa kortini
MKURUGENZI wa Kampuni ya Richmond Development ya Tanzania, iliyowahi kupewa zabuni ya kuagiza mitambo ya kufua umeme wa dharura nchini, Naeem Adam Gire, juzi alifikishwa mahakamani akikabiliwa na mashitaka matano, likiwamo la kughushi nyaraka.
Naeem Gire alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kusomewa mashitaka hayo, baada ya kufunguliwa kesi namba 15 ya mwaka 2009.
Naeem anashitakiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa mujibu wa hati ya mashitaka, shitaka la kwanza linalomkabili ni kughushi, kinyume cha sheria.
Hati hiyo ya mashitaka inaeleza kuwa Machi 13, mwaka 2006, akiwa katika Jiji la Dar es Salaam, alighushi akiwa na lengo la kuhadaa mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuifanya iamini kuwa Mohamed Gire ambaye ni mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond Development LLC ya Texas Marekani, alisaini kuridhia aendeshe (Naeem) biashara na kampuni ya Richmond Development LLC ya Tanzania.
Katika shitaka la pili, anatuhumiwa kuwasilisha nyaraka zisizo sahihi kinyume cha sheria za nchi.
Inadaiwa kuwa Machi 20, mwaka 2006, katika kituo cha umeme eneo la Ubungo, kandokando ya Barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam, akijua kuwa ni makosa aliwasilisha nyaraka zisizo sahihi za Machi 13, 2006 zikionyesha kuwa Mohamed Adam Gire, Mwenyekiti wa Richmond Development LLC ya Texas, Marekani amesaini nyaraka kuridhia afanye biashara na kampuni ya Richmond Development LLC nchini Tanzania.
Waendesha mashitaka wa Serikali Leonard Manyanda na Boniface Stanslaus walidai kuwa katika shitaka la tatu Naeem aliwasilisha taarifa za uongo kwa serikalini kinyume cha sheria.
Walidai kuwa Machi 20, mwaka 2006, katika ofisi za TANESCO Ubungo jijini Dar es Salaam, mtuhumiwa aliwasilisha katika bodi ya zabuni ya TANESCO taarifa ambazo anafahamu kuwa ni za uongo.
Na katika taarifa hizo alidai kuwa Richmond Development LLC ya Texas, Marekani ilikuwa na uwezo wa kuzalisha megewati 100 za umeme ili kuishawishi bodi hiyo iiteue kampuni hiyo na kuipatia zabuni.
Katika kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na Hakimu Wariawande Lema huku upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Kato Zake, ilidaiwa kuwa Naeem kama ilivyo kwa shitaka la tatu, aliwasilisha taarifa za uongo kwa watendaji wa Serikali, lakini katika shitaka la nne taarifa hizo aliziwasilisha kwa wajumbe wa Timu ya Serikali (GNT).
Ilidaiwa kuwa aliwasilisha taarifa hizo katika GNT huku akitambua kuwa taarifa hizo ya kwamba kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha megawati 100 za umeme si za kweli.
Katika shitaka la tano ilidaiwa na upande wa waendesha mashitaka mahakamani hapo kuwa Juni 2006, akiwa jijini Dar es Salaam huku akitambua kuwa si sahihi, alighushi nyaraka ili kuthibitisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa ameridhiwa kuendesha shughuli za kibiashara za kampuni ya Richmond Development LLC nchini Tanzania.
Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa
Gire alipelekwa rumande Keko, jijini Dar es Salaam na anatarajiwa kurejeshwa mahakamani Kisutu leo.
Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond ndiyo chanzo cha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, pamoja na mawaziri Dk. Ibrahim Msabaha na mwenzake, Nazir Karamagi.
Walilazimika kujiuzulu mara baada ya Kamati Teule ya Bunge kuwasilisha taarifa yake ya uchunguzi kuhusu mradi huo wa umeme wa dharura. Kamati hiyo iliongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harisson Mwakyembe na kusomwa bungeni Februari, mwaka jana.
Kutoka Raia Mwema
No comments:
Post a Comment