Friday, January 23, 2009


Henry Joseph

asajiliwa na timu ya

Tromsø ya Norway




Sosthenes Nyoni, Mwananchi

NAHODHA wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars na klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Henry Joseph Shindika anarajia kuondoka nchini Jumatatu kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM) kwenda Norway kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Tromso.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Frederick Mwakalebela alisema kuwa tayari mchezaji huyo amekutana na Kocha Mkuu wa Taifa Stars , Marcio Maximo na kupata baraka zote.

Alisema kuwa TFF iliridhia na kutoa baraka kwa mchezaji huyo kwenda kufanya majaribio nchini humo baada ya kuwa amekubaliana na uongozi wa klabu yake.

"Alipokuja hapa tulimwambia kwanza akamalizane na uongozi wa klabu yake, akafanya hivyo na sasa leo 'jana' ameongea na mwalimu wake Maximo na kupata baraka zote,"

Mwakalebela alisema kuwa mpaka wakati huo, TFF ilikuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha visa ya kusafiria ya kiungo huyo kutokana kutambua umuhimu wa wachezaji kucheza ligi za kulipwa.

"Mpaka wakati huu tupo katika harakati za kumpatia visa ya kusafiria kwani tunatambua umuhimu wa nchi kuwa na wachezaji wa kulipwa ndiyo maana hata Maximo huwa nasisitiza hili"alisema Mwakalebela.

Mwakalebela alisema kuwa mchezaji huyo ambaye amefanyiwa mpango wa kwenda nchini humo na mmoja wa mawakala wanaotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ataongozana pia na mchezaji mwenzake kutoka klabu ya Simba, Emeh Izuchukwu.

Kutokana na kuondoka kwake, endapo atafuzu, atafanyiwa taratibu za kuondoka nchini kwenda kucheza soka ya kulipwa ikiwa ni pamoja na kutumiwa hati za uhamisho wa kimataifa.

Henry amekuwa kiungo muhimu kwa klabu yake ya Simba na Taifa Stars, na kuna wasiwasi wa kuikosa michuano ya Afrika kwa wachezaji wa Ndani, CHAN, inayotarajia kufanyika nchini Ivory Coast kuanzia Februari 22 hadi Machi 8.

Stars ni kati ya mataifa yatakayotia timu ikiwa Kundi A pamoja na Zambia, Senegal na wenyeji Ivory Coast. Kundi B lina timu za Zimbabwe, Libya, Congo DR na Ghana.


Kwa wapenzi wa soka, soma zaidi kuhusu timu ya Tromsø:

http://www.til.no/

http://en.wikipedia.org/wiki/Tromsø_IL


No comments: