Mwenyekiti wa AU
Kanali Muammar al-Ghaddafi,
Rais anayelindwa na
wanawake bikira
* Ni nadra kupanda ndege
* Anguko la Saddam lilibadili ukali wake
Hilo linatokana na ukweli kwamba kiongozi huyo aliyekalia madaraka tangu Septemba 8, mwaka 1969 amekuwa mwenye ubavu wa kuweka sera ambazo wananchi wake wanazifuata hata kama haziwafurahishi.
Mtawala huyo alizaliwa Juni 19, mwaka 1942 katika eneo la Surt, Tripolitania na aliingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi. Mapinduzi hayo yamemfanya kiongozi huyo kupewa heshima kubwa nchini mwake na washirika wake nje ya taifa hilo.
Gaddafi mtoto wa wakulima masikini nchini humo alianza kuonyesha makucha yake tangu akiwa na umri mdogo. Alikulia katika eneo la jangwa la Sirte. Alipata elimu ya jadi na ya kidini katika shule ya dini ya Sebha huko Fezzan kati ya mwaka 1956 na 1961.
Kiongozi huyo alijiunga na marafiki zake wachache na kuunda kikundi cha kijeshi ambacho kama masihara kikaja kupindua Libya.
Alivutwa sana na utawala wa rais wa zamani wa Misri, Gamal Abdel Nasser. Alichompendea Nasser ni msimamo wake katika kuunda umoja wa Waarabu.
Kutokana na kupenda kwake siasa, Gaddafi alitimuliwa shuleni mwaka 1961. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Libya kusoma sheria na inaelezwa kuwa alifanya vizuri darasani. Mwaka 1963 alijiunga na chuo cha jeshi cha Benghazi.
Akiwa huko, aliunda kikundi cha siri kwa ajili ya kuangusha utawala wa kifalme wa Libya uliokuwa unaungwa mkono na nchi za Magharibi. Miaka miwili baadaye akaenda Uingereza kwa mafunzo zaidi ya kijeshi na kuhitimu mwaka 1966.
Kiongozi huyo wa Libya kwa miaka mingi amekuwa msiri wa mambo mengi lakini kubwa ni msimamo wake katika ulinzi binafsi.
Gaddafi amekuwa kiongozi wa kipekee anayelindwa na wanajeshi wa kike. Kikundi chake hicho cha walinzi wake binafsi kinajulikana kama Amazon kinachoundwa na wanawake 200.
Inasemekana pia kuwa sifa kuu ya kuingia katika kikundi hicho ni mwanamke kuwa bikira. Swali linakuja ni nani anahusika na usaili huo?
Swali hilo limekuwa gumu kupata jibu lakini ukweli wa mambo ni kwamba wanawake hao ni wakakamavu kwani hupitia mafunzo ya hali ya juu katika medani za kivita pia.
Ni mahiri wa karate na aina nyingi za mapigano ya kujilinda na wengi wao hawajaolewa jambo linalowafanya watumie muda wao mwingi kuwa karibu na Gaddafi.
Mara nyingi Gaddafi hupenda kutumia gari kusafiri masafa marefu. Si mwepesi wa kupanda ndege au usafiri mwingine. Huenda hiyo ni staili yake nyingine aliyoamua kujiwekea maishani.
Lakini pamoja na kuonekana kuwa mtawala asiyetetereka? Gaddafi ni kama kunguru mwoga. Hili lilijihidhirisha Machi mwaka 2003 baada ya Saddam Hussein kuondoshwa madarakani nchini Irak na majeshi ya Marekani na washirika wake.
Baada ya Saddam kuangushwa, Gaddafi akaitangazia dunia kuwa nchi yake haikuwa na silaha za maangamizi na hivyo kuruhusu waangalizi kuingia Libya kufanya ukaguzi.
Kutokana na tangazo lake hilo, jumuiya ya kimataifa ikamwona kuwa Gaddafi alikuwa mwoga kwani aliamini kuwa kilichompata Saddam kingeweza kumpata yeye pia.
Bila shaka msimamo wake huo ulimweka katika sura mpya katika ulimwengu wa siasa. Alipunguza maadui wakubwa waliokuwa wamemwandama. Marekani na Uingereza zikamwona kuwa aliyezaliwa upya.
Gaddafi ana watoto wanane, saba kati ya hao ni wa kiume. Mtoto wake mkubwa ni Muhammad Gaddafi, ambaye sasa ni kiongozi wa Kamati ya Olimpiki ya Libya na anamiliki kampuni nyingi za mawasiliano nchini humo.
Anayemfuata Saif al-Islam Gaddafi, ni fundi mwashi ambaye pia anaendesha taasisi ya kuwatetea wapiganaji wa Kiislamu waliotekwa hasa katika maeneo ya Ufilipino.
Tofauti na watoto wengine, Saif Al Islam amekuwa akipinga utawala wa baba yake na mwaka 2006 alilazimika kuondoka Libya lakini alirejea baada ya miezi kadhaa. Anatajwa kuwa mmoja wa waliokuwa mstari wa mbele kumtetea daktari wa Kipalestina na wauguzi wa Kibulgaria waliokumbwa na kesi ya kuwachoma watoto sindano yenye virusi vya Ukimwi.
Mtoto wake mwingine Al-Saadi Gaddafi ni Rais wa Shirikisho la Soka la Libya na ni mchezaji pia wa timu ya soka ya U.C. Sampdoria ya Italia. Utajiri wake mkubwa umetokana na kuuza petroli na utengenezaji wa filamu.
Binti pekee wa Gaddafi anakwenda kwa jina la Ayesha. Huyu ni mwanasheria maarufu na alikuwa mmoja wa mawakili wa utetezi wa Saddam Hussein.
Makala haya yametayarishwa na Mwandishi INNOCENT MUNYUKU kwa msaada wa intaneti na majarida.'
Kutoka gazeti la Rai
No comments:
Post a Comment