Sunday, February 22, 2009



Siri ya vitambulisho

vya taifa yafichuka



Shadrack Sagati


Kampuni mwelekezi wa mradi wa vitambulisho vya taifa Gotham Internation Ltd imesema kiasi cha Sh bilioni 200 ambazo zimepangwa kutumika katika mradi huo haziendi zote kwa mkandarasi atakayeshinda zabuni ya kutengeneza vitambulisho hivyo. 

Badala yake, kampuni hiyo ya kitaalamu imesema kuna maeneo 14 ambayo fedha hizo zitatumika huku kampuni mkandarasi atakayepewa jukumu la kutengeneza vitambulisho hivyo atalipwa sio zaidi ya Sh bilioni 35. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Gotham International Dk. John Kyaruzi alitaja maeneo mengine ambayo alisema yatagharimu fedha nyingi kuwa ni majengo na wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho hivyo (NIDA), utambuzi wa Mtanzania, uboreshaji wa sheria pamoja na uelimishaji wananchi. 

"Gharama kubwa iko kwenye kumtambua Mtanzania pamoja na kugharamia uhamasishaji kupitia vyombo vya habari na sio manunuzi," alisema Dk. Kyaruzi ambaye kampuni yake imeingia mkataba na serikali kutoa ushauri juu ya mradi huo. 

Kampuni sita za kigeni tayari zimepita katika hatua ya awali ya kuwania utengenezaji wa vitambulisho hivyo. Kampuni hizo ni Unisys ya Afrika Kusini, Giesecke & Devrient Fze ya Dubai, Iris Corpotaration Berhad ya Malaysia, Madras Security Printers ya India, Maruben Corporation ikishirikiana na Zetes na Nec ya Japan, Tata Consultancy Services ikishirikana na Ontrack Innovations Ltd ya India. 

Mtaalamu huyo pia alitaja gharama nyingine kuwa ni baadhi ya kazi zilizotajwa katika mradi huo zitapata bajeti ya wizara nyingine husika na sio kweli kuwa zote ni za mradi huo. Alitoa mfano wa bajeti ya kuboresha mitandao iko katika Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia huku bajeti ya kuandikisha inaweza kuwa katika Serikali za Mitaa. 

Kampuni hiyo imelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuwapo malalamiko kuwa fedha nyingi zimetengwa katika mradi huo ambao unaonekana kuanza kuzua mtafaruku miongoni mwa wanasiasa. 

Lakini alifafanua kuwa vitambulisho hivyo wao kama wataalamu wamependekeza kuwa vitolewe bure kwa Watanzania huku wageni wakiwamo wanadiplomasia na wakimbizi watalazimika kuchangia kidogo. 

Dk. Kyaruzi alisema mradi huo ni wa muungano na ndiyo maana hakukabidhiwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali au Wakala wa Vifo na Vizazi (Rita) kwa vile vyombo hivyo sio vya muungano. 

"Ndiyo maana mradi huo uko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ni ya muungano, ndiyo maana imeundwa mamlaka na sio wakala," alisema Dk. Kyaruzi. 

Alisema katika bajeti hiyo ya vitambulisho kuna fedha zitapitia kwenye wizara nyingine kama Uhamiaji, Rita na taasisi nyingine visiwani Zanzibar ambazo zinajishughulisha na usajili wa vizazi na vifo. "Hivyo sio kweli kwamba fedha zote ni za NIDA." 

Mtaalamu huyo alitetea bajeti hiyo kwa kueleza kuwa mradi huo sio aghali kama nchini nyingine kwa sababu hakuna kitu kilichokwishafanyika bali taifa linaanza upya kwa kila eneo. 

Naye Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Jack Gotham alisema kampuni yake imeajiriwa na serikali kufanya kazi hiyo chini ya sheria namba tatu ya mwaka 2001 na wanajitahidi kutoa ushauri kuhakikisha mradi huo unapata mafaniko makubwa. 

Kuhusu teknolojia ya Smart Card, Gotham alisema walipendekeza hiyo kwa vile kitambulisho hicho kitakuwa na maelezo mengi hivyo kuwa faida kubwa kwa taifa katika masuala ya usalama na uhalifu. 

Kuhusu habari ambazo zimekuwa zinaandikwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa kampuni hiyo haina mkataba na serikali, Gotham alionyesha mkataba walioingia na serikali Novemba 10, 2004. 

Alisema kampuni yake imekuwa inafanya kazi vizuri na taasisi zote za serikali ambazo zinajihusisha na vitambulisho hivyo akasisitiza kuwa ushauri ambao wameutoa kwa serikali wanaamini kuwa una lengo zuri la kuwafanya Watanzania waweze kutambuana. 

Mradi wa vitambulisho vya taifa ulipitishwa na kikao cha Bazara la Mawaziri kilichoketi Februari 2, 2007 na kutangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo Joseph Mungai. Mchakato wa maandalizi yake ulianza mwaka 1995 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2009. 

Mradi huo wa vitambulisho hivi karibuni umekuwa unaandikwa zaidi kwenye vyombo vya habari hasa ikiwamo kuachwa kwa Kampuni ya Sagem ya Uswisi katika hatua ya pili ya kuwachuja wazabuni hao. 

Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa Waziri Masha amelalamika kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda juu ya kuachwa kwa kampuni hiyo hadi akashauri Bodi ya Zabuni ipate ushauri PPRA kitendo kilichotafsiriwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa anataka kuibeba kampuni hiyo. 

Lakini pia baadhi ya vyombo vya habari vimeibuka hivi karibuni vikiishambulia Kampuni ya Gotham kuajiriwa na serikali bila kuingia mkataba wowote. Hata hivyo kampuni hiyo jana iliwaonyesha wanahabari mkataba huo.


No comments: