Taifa Stars yaifunga
Pichani wachezaji wa Stars wakishangilia kwa namna yake.
BAO pekee lililofungwa dakika ya 37 kwa kichwa na Mrisho Ngassa katika mchezo dhidi ya Ivory Coast jana, ilifufua matumaini ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kufuzu nusu fainali ya michuano ya Afrika kwa wachezaji wa Ndani (CHAN). Ngassa alifunga bao hilo kutokana na mpira wa krosi uliopigwa na Henry Joseph na kutua kichwani mwa Ngassa aliyeukwamisha wavuni.
Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny umeifanya Stars kufikisha pointi tatu, ikiwa na mchezo mmoja mkononi, lakini matokeo hayo yameifanya Ivory Coast iage mashindano hayo, ambapo mchezo wake wa mwisho Jumamosi dhidi ya Senegal utakuwa wa kukamilisha ratiba.
Hadi sasa Zambia inaongoza kundi hilo la A ikiwa na pointi nne na mabao matatu, huku Senegal ikishika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi nne na bao moja la kufunga na Stars inashika nafasi ya tatu, huku Ivory Coast ikiwa ya mwisho haina pointi.
Mwandishi ni Anastazia Anyimike wa HabariLeo.
No comments:
Post a Comment