Ban Ki-Moon ziarani
Tanzania

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-Moon, amewasili nchini na kupata mapokezi makubwa kwenye uwanja wa ndege wa zamani, jijini Dar es Salaam.
Ndege ya Umoja huo yenye namba EC-JJS iliyomchukua Ki-Moon na wajumbe kadhaa waliopo katika msafara wake, ilitua kwenye uwanja huo saa 8:53 mchana.
Umati wa wakazi wa jijini Dar es Salaam, wakiwemo viongozi kadhaa wa serikali, walifika uwanjani hapo kumlaki Ki-Moon, aliyeteremka kutoka ndani ya ndege hiyo saa 9:06.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliwaongoza watu waliofika uwanjani hapo kumlaki Ki-Moon.
Waziri mwingine aliyekuwepo uwanjani hapo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Batilda Burian.
Pia, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, Oscar Fernandez-Taranco, alikuwa miongoni mwa watu waliofika kumpokea Ki-Moon.
Baada ya kuwasili, Ki-Moon aliyeongozana na Waziri Membe, alipigiwa wimbo wa Umoja wa Mataifa na ule wa Taifa, kisha akakagua gwaride lililoandaliwa na askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Pia Ki-Moon, alitembelea na kushuhudia vikundi mbalimbali vya ngoma za asili, vilivyokuwa uwanjani hapo kwa ajili ya kusherehesha mapokezi hayo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa kuhusu ujio huo, Ki-Moon alitarajiwa kuonana na kufanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete jana na kutoa mada katika mhadhara uliofanyika jijini hapa.
Leo Ki-Moon atatembelea Zanzibar na Arusha, kisha kurejea jijini Dar es Salaam, ambapo atazungumza na waandishi wa habari.
Ki-Moon, yupo katika ziara ya siku mbili ambapo kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa juzi na Fernandez-Taranco, kiongozi huyo wa UN atagusia masuala ya uhalifu wa kivita, mabadiliko ya hali ya hewa na mageuzi katika mfumo wa Umoja huo.
Hii ni ziara ya kwanza ya kikazi ya Ki-Moon hapa nchini tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo.
- SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment