Friday, February 06, 2009

Waziri Masha asafishwa


Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Raia, Lawrence Masha


* Wajumbe wa Kamati ya Bunge wakataa kuzungumza kilichojiri 
* Ripoti yake ya maamuzi yasuburiwa kwa hamu na wananchi 

Na Waandishi Wetu 

WAKATI Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, akishambuliwa kwa madai ya kuingilia kati mchakato wa utoaji wa zabuni za vitambulisho vya taifa, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (Public Procurement Regulatory Authority – PPRA), imemsafisha ikisema iwapo asingechukua hatua hiyo, Serikali ingejikuta ikiingia mtegoni. 

Vyanzo vya habari vimedokeza jijini Dar es Salaam kwamba PPRA katika maoni yake, imesema kuwa endapo Waziri Masha asingechukua hatua hiyo, kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa kampuni zilizoenguliwa katika zabuni hiyo, kuishitaki Serikali, na pengine kuidai mamilioni ya shilingi, kutokana na kuenguliwa kinyemela. Habari za kusafishwa kwa Masha zinakuja wakati Kamati ya Bunge Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, ikiwa imekutana kwa siku mbili mjini Dodoma, kujadili tuhuma zilizotolewa na Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa, kwamba Masha amekuwa akiingilia uteuzi wa mzabuni wa kutengeneza vitambulisho vya taifa, kwa kuipigia kifua moja ya kampuni zilizoenguliwa. 

Kilichopo katikati ya sakata hili ni barua ambayo Masha anadaiwa kumwandikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akilalamikia utaratibu uliotumika katika kutathmini makampuni yaliyoomba zabuni hiyo ambayo itaigharimu Serikali mabilioni ya shilingi. 

Lakini tofauti na Dk. Slaa, ambaye anaiona barua hiyo kama ni hatua ya kuingilia uteuzi wa mzabuni wa radi huo mkubwa, PPRA wanasema kwa hatua yake hiyo, Masha ameliokoa taifa kutokana na ukweli kwamba utaratibu uliotumika kuziteua kampuni tisa kati ya 21 zilizokuwapo, ulikuwa na walakini na ambao kisheria, ungeweza kuigharimu nchi. 

Hadi jana jioni, hakukuwa na taarifa za nini kilichojadiliwa katika kikao cha siku mbili cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, huku Mwenyekiti wa kamati hiyo, Wilson Masilingi, akiwakwepa waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia suala hilo kwa kila hali. 

Ingawa bado hakuna taarifa rasmi kuhusiana na nini kilichojadiliwa katika Kamati ya Masilingi, ukweli kwamba uamuzi huo umebarikiwa na PPRA, chombo kinachosimamia taratibu za ununuzi wa Serikali, uwezekano wa Masha kutundikwa msalabani kupitia maamuzi ya kamati, unakuwa mdogo. 

Inaelezwa kuwa pamoja na mambo mengine, baada ya kuona suala hilo likiwa gumu kwake, hasa kutokana na kuingiliwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, aliyetaka mchakato wa kumpata mzabuni uharakishwe, Masha alipendekeza kwa Bodi ya Zabuni, kuomba ushauri wa kitalaamu kutoka PPRA, ili kuepusha manung’uniko kutoka katika kampuni zilizoenguliwa kwenye zabuni hiyo. Wakati sakata la Masha na kuingilia kwake uteuzi wa mzabuni wa kutengeneza vitambulisho vya taifa lilipokuwa imepamba moto, gazeti hili liliwahi kuandika habari kuwa mtu anayedaiwa kuchomoa waraka wa Serikali kutoka katika mafaili ya Wizara ya Mambo ya Ndani, alikuwa akisakwa kwa udi na uvumba na makachero. 

Ilitarajiwa kuwa mtu huyo ambaye habari zinasema ni mmoja wa vigogo wizarani hapo, angejadiliwa katika kikao cha Kamati ya Bunge na hatua dhidi yake zingeamuliwa kutokana na kutoa nje siri za Serikali. Hata hivyo, uzito wa hatua dhidi yake, unategemea na maamuzi ambayo kamati hiyo itayatoa dhidi ya Masha. 

Jitihada za kuzungumza na Masha mwenyewe pamoja na Dk. Slaa kuhusiana na nini kilichojiri katika kikao hicho zilishindikana jana baada ya wote wawili kukataa katakata kuzungumzia, wote wakisema wanatii agizo la Spika wa Bunge, Samuel Sitta, aliyewaonya wenyeviti wa kamati kuzungumzia mambo wanayoyajadili kabla hayajawasilishwa bungeni.


Kutoka Mtanzania

No comments: