Eti mke kwenda masomoni
na mume kubaki analea
watoto, ni hujuma au!
Mpenzi msomaji, lipo jambo moja ambalo nimelinasa likilalamikiwa na baadhi ya kinababa. Linahusu wimbi la kinamama kuanzisha mchakato wa kujiendeleza kielimu katika vyuo mbalimbali vya hapa nchini na hata ng`ambo.
Juhudi hizo kwa upande mmoja zinaonekana ni njema, lakini kwa upande mwingine ni aina fulani ya hujuma. Kwanini muonekano huo ulete utatanishi? Vuta subira msomaji wangu nikumegee vionjo.
Ni kawaida katika baadhi ya familia zetu, baba kwenda masomoni na kumuacha mkewe na watoto nyumbani.
Kadhalika hali iko hivyo kwa kinamama wanaopenda kujiendeleza kutafuta vyuo viwe vya ndani ya nchi au hata nje kujiweka katika ufahamu wa juu zaidi kitaaluma.
Wapo wanaolazimika kujiendeleza chini ya taratibu za kule wanakofanyia kazi au wengine hujitegemea katika kujigharimia kimasomo.
Swali ni je, pamoja na nia hiyo nzuri, ipo harufu yoyote ya hujuma kwa maana ya uvunjifu wa uaminifu watu hawa wawapo masomoni?
Hivi majuzi nilikutana na kinababa fulani wakawa wanaelezea wasiwasi kuhusu wimbi la kinamama walioolewa kuonekana wakijizatiti kwenda kusoma na kuwaachia waume zao jukumu la malezi ya watoto.
Nilipotaka kujua kwanini kinababa hawa wanahofia mkakati huo wa kinamama walioolewa kung`ang`ania kujiendeleza kielimu, wakawa na haya ya kusema;
``Wengine ni janja yao tu, kwanini mama anayeishi Dar es Salaam, aende chuo cha hapa hapa halafu asirudi nyumbani akalale huko huko?
Ukiuliza anadai eti huwa wana group discussions...kwani lazima majadiliano yafanyike usiku? Kwanini yasifanyike mchana, halafu akarudi nyumbani kwa mumewe? Mmoja aliuliza maswali yote hayo.
Mwingine akadakiza, ``ufisadi mtupu, mama wa Dar es Salaam kulala chuoni na mume na wanawe wako hapa ujue ana lake jambo…lazima ana bwana wa pembeni huyu…``
Mwingine akakoleza kwa kutoa mfano, ``Yuko mke wa rafiki yangu alipata mwanya wa kwenda kusoma ng'ambo.
Alipomaliza masomo ya miaka miwili akatarajiwa angerudi nyumbani, lakini akazamia huko huko.
``Mume kudadisi akadokezwa kuwa mkewe alishaolewa na mzungu siku nyingi na wala hana mpango wa kurudi nyumbani.
Kwa hiyo, mkakati wa kujiendeleza kimasomo kwa baadhi ya wanawake walioolewa, kwa kiasi fulani umelenga hujuma na usaliti kwani wengine wanatafutia njia ya kuondokea kama wakikuchoka``, anamalizia kusema baba huyu.
Baba huyu wa mwisho alinikumbusha kisa kimoja ambapo ndoa fulani ilidumu kwa miaka kadhaa bila kujibu(kupata mtoto). Wakati fulani baba huyu akapata ajali moja mbaya ya gari.
Chanzo cha ajali ile inasemekana alikuwa akiendesha gari huku akiwa anapapaswa na kidosho. Hamadi akajikuta anagonga kwa nyuma gari lililokuwa mbele yake na kujiingiza mvunguni.
Baadaye akalazwa hospitalini taaban huku akiwa amevunjika sehemu mbalimbali za mwili. Mama akachunguza chanzo cha ajali na kupata data zote.
Alichofanya ni kumuuguza mumewe hadi akapata nafuu, kisha akatafuta kozi yake ya nje ya nchi ambayo aliipata. Akamuacha mume huyu kwenye wheel-chair akihudumiwa na ndugu zake, kisha yeye huyoooo akaishia zake ulaya.
Hadi leo hii inasemekana hajarejea na huko ng`ambo tayari amempata mzee wa kizungu ambaye anaishi naye kinyumba na wala hana mpango wa kurudi tena huku kwani hakuacha hata mtoto. Ama kwa hakika, Maisha Ndivyo Yalivyo. Au siyo msomaji wangu?
Kwa hili unasemaje msomaji wangu? Hebu nikupe fursa nawe uchangie maoni tuelimishane. Hili ni tatizo linalohitaji ufumbuzi wa pamoja. Ukiwa tayari nikandamizie kupitia;
Anti Flora Wingia
Nipashe
1 comment:
Hapa Norway tunao kina dada wengi wameacha waume na watoto zao Bongo na kuja kusoma. Kwa sababu za kutafuta makaratasi ya kuishi, wameolewa huku na kuwatekeleza waliowacha nyumbani...
Post a Comment