|
Mwanamke wa shoka bibi ni yule anayejua nini aseme na wakati gani aseme, huo ndio ukweli. Na si kila mwanamke analijua hili la kupima cha kusema kabla hakijatoka mdomoni mwake, shoga upo hapo…. Kwanza ya yote naomba nikusabahi, kisha nikukaribishe kwa moyo mkunjufu, katika kona hii nikiwa na imani kubwa utafaidika na utakachokisoma hapa leo… Wakati wanawake wengi wakiwa hawayafahamu haya naomba nakukaribisha katika ulimwengu wa wanaume usikie mwenyewe, kile ambacho kinawatia udhia wanaume kusikia wake zao wakikiongelea. Ukweli ni kwamba vipo vitu ambavyo mara nyingi huzungumzwa kwa nia njema kabisa lakini vikaleta udhia mkubwa kwa upande wapili, na hii wengi hufanya kwa kujua na wakati mwingine kutokujua. Aidha si kila mtu anajua kuchagua cha kuongea linapokuja suala zima la kuwasilisha mambo. Na hii ndiyo sababu nikawaweka chini wanaumme saba wa rika tofauti kuzungumza nao machache; yale yanayowakera kusikia kutoka kwa wake zao kwa faida ya wanawake wenzangu hapa leo. Utafiti huu mdogo umekuja na haya mambo 15 ambayo wanaume wamesema yanawakera kuyasikia kutoka kwa wanawake zao wakiyaongelea. 1. Stori za wanaume zako waliopita… Stori zozote zile za aliyekuwa mwanaume wako wa zamani huleta udhia kwa mumeo, hata zikiwa ni zile za kumkashifu mwanamme huyo bado zinaweza kujenga maswali kwa mumeo. Si vizuri kumuongelea mara kwa mara kuhusu mwanamme wako wa zamani mbele ya mumeo wa sasa kwa kuwa humfanya mumeo ajisikie dhaifu na huenda akadhani bado moyoni mwako uko kule. Ingawa si vibaya kuzungumza juu ya mahusiano yenu yaliyopita kipindi cha mwanzaoni mwa uhusiano mpya lakini si vizuri kurudia kuongea habari za mabwana zako waliopita kwa huyu bwana mpya. Ingawa wanaume wengine wangependa kuzungumzia kuhusu bibi zao wa zamani, wewe jifunze kufunga mdomo wako. Na akidai umweleze mpotezee. 2. Kukusikia ukimsifia mwanamme mwengine... Kama mumeo ni mfupi akisika unasifu urefu wa mwanamme fulani bila kuuliza utaona tu katika sura yake. Wakati mwingine unaweza usifie kwa nia nzuri tu, lakini kwa mwanamme hisia ni kwamba unamlinganisha na wanaume hawapendi kulinganishwa na majibu ni kwamba umemdharau. 3. Kusikia unausema udhaifu wake… Nani anayependa udhaifu wake uanikwe, bila shaka kila mtu hapendi udhaifu wake uanikwe. Ni hakika kuwa hakuna binaadamu aliyetimia. Basi umeujua udhaufu wake ulipo, uweke kifuani, usimweleze mbele ya macho yake kwa kumbeza na usiutumie kama mzaha, kwa kuugeuza kuwa utani. Ukifanya hivyo bila kujua unamchukiza na kumfanya ajisike bwege, na sidhani kama kuna mwanamme anayeipenda hii feeling. 4. Umetongozwa, komesha... keep it to your self! Wengine hudhani kumwambia mwanamme fulani kanitongoza kunazidisha mapenzi, na wengine hutumia njia hiyo kuwatia wivu waume zao, wakati mwingine huleta maana nyingine. Umetongozwa mkomeshe aliyekutongoza, haelewi unaweza ukatafuta msaada kwa mumeo. Wenaume wengine shosti huigeuza upande wako, wanadai mpaka mwanamke aseme katongozwa jua kuna kitu, si wote wanaokutongoza ukawakubali utamwambia. 5. Stori mbaya za marafiki zako... Ingawa atakusikiliza, na utahisi anafurahi kuzisikia stori hizo kwa picha ya nje, picha ya ndani bibi jua anakuhesabu katika mabaya hayo kwakua unayesimulia stori yake ni rafikiyo. Bila kukwepa unahusika kwa namna fulani. Kunasiku utashangaa atakuja kukulaumu nazo kuwa umeharibiwa na marafiki zako. Kama vipi zitupe kapuni na muepuke rafiki huyo. 6.Wanaume wengine hawapendi ukweli... Ukweli wanasema lazima usemwe, lakini wakati mwingine ukweli inabidi uachwe, na ikibidi upindishwe kwa nia njema kabisa, na si semi udanganye. Mfano "Nimechoka," wanawake wengi huisema hii. unaweza kuwa unamwambia kwa nia njema kabisa na kweli umechoka, ila akaichukulia vibaya. Umechoka ulikuwa wapi? unafanya nini...? Na mara zingine ukisema umechoka basi mwenzako ataanza kufikiri hakuridhishi ndo maana unamkwepa. huo ni mfano mmoja wa ukweli... Naishia hapa kwa leo usikose kumalizia muendelezo wa makala haya wiki ijayo. Mpaka hapa, nasubiri maoni yenu: asmahmakau@mwananchi.co.tz |
No comments:
Post a Comment