Thursday, March 26, 2009


Wabongo Masalia!




Imeandikwa na Joseph Kulangwa;

Tarehe: 24th March 2009

Habari Leo


Wabongo kweli ngozi ya goti. Utawaona tu wako mitaani, wanacheka, wanataniana, wanakula miwa na kutupa maganda barabarani. Wengine wanabwia na kuvuta na wapo hawa washikaji maarufu tu mijini ambao huvizia mkono wako udondoke, wanywe. 

Nawasema hawa ambao utawakuta mitaani wanaangalia mfuko wako umetuna vipi au simu yako umewawekea kihasarahasara vipi wakusaidie kuitunza! Wapo na hawa ambao kila kukicha asubuhi, wako vituo vya mabasi wakihanikiza Temeke, Temeke, Temeke, Ubungo, Ubungo, Ubungo! nk.
 

Hawa ni wale muda wote kwao ni usingizi, muda wote kwao ni vichanga, kwani ni udenda kwa kwenda mbele. Wanawaita mateja hawa. Hawajui limekucha au limekuchwa, ili mradi waone daladala kituoni baaasi ndio mateja hawa a.k.a wapiga debe.
 

Bila kutafuna maneno hawa wamewashinda jamaa zetu wavaa krauni hawa, wamewashinda hata hawa wateule wa JK, wanaoteuliwa kutusimamia sisi katika mikoa yake hii. Mnakumbuka alivyongia Abbas sijui akitoka zake Arusha huko, akaanza nao, lazima waondoke, akahanikiza weeee! Wapiii! Mara akaingia na huyu mvaa krauni Suleiman, akitokea zake huko Mbeya, na moto wake, wataondoka tu hawa wanasumbua abiria vituoni kwa kuwaibia na kupiga kelele. Sura hizi zilizosheni makovu kila sehemu ya mwili kutokana na kuchomana bisibisi, wakamwangalia wakamwacha kama alivyo.
 

Kama alivyoingia Abbas mpaka pale Uwanja wa Fisi, ndivyo Suleiman naye alivyokuja akisema ataanza na Kinondoni na Ohio pale, kwa dada poa wetu pale. Nadhani huko walikokuwa hawakuwapo akina dada wa aina hii. Bila kuzingatia falsafa ya Mao Dze Dung wa Uchina, wakaingia kichwakichwa.
 

Mao alikuwa anasemaaaa, usifunue domo bila kufanya utafiti. Jamaa zetu hawa wakaingia
 
wakidhani Sardalamu ni mahali unaingia tu na kupanda juu ya miti na kuanza kutangaza sera zako, hawakujua kuwa kuna wenyeji, bila kuwaona kwanza utaangamiza sera zako na utoke
 mikono mitupu. Masikini hawa hawakujua kuwa kumbe akina dada poa na washikaji mateja na wapiga debe wana magodifaza wao ambao ndio wanawaweka mujini ili kuwasaidia kwa mambo fulanifulani ya kujipoza kiakili na kimwili. 

Sasa unapovunja kambi za Uwanja wa Fisi madingi waponee wapi! Unapozuia Kinondoni na
 Ohio, vigogo wetu wakasalimikie wapi wakati nyumbani hapakaliki, akina mama ni shubiri kwa kwenda mbele. Wee unadhani Mizengo alichokifanya pale Feri cha kutaka waondoke mateja ni kipya? Thubutu! Walipita akina Edo wakahanikiza waondoke watu pale, walipita akina Fred wakapaza sauti mateja waondoke karibu na Jengo Jeupe, kwa sababu moshi wa ganja umefukuza tausi na swala waliokuwa katika jengo hilo, lakini wapi, vijana wakawa wanapanda kwenye miboti chakavu pale na kuwambia: "mnacheza nyie"! 

Haya kaibuka Suleiman wa Mashimo ya Sentro, kasema atawamaliza pale Feri, sisi tunamwangalia tu tuone, kwa sababu tumeshatumiwa ujumbe wa maneno mafupi katika SMS
 
zetu, vijana wanasema "mnachezaaa". Wanauliza muwafukuze Feri wakale wapi? Wakiwapigeni loba za misumari mnakuja juu.
 

Wanajivutia vibange vyao na kujibwilia vijiunga vyao mnawafuata. Basi nao wanataka watengewe maeneo maalumu ya kubwilia vijiunga vyao na kujivutia vibange vyao na kulala wala msiwabughudhi! Wawekeeni maghorofa kama ya Karume pale basi. Wana tofauti gani na hawa jamaa zangu Wasabato Masalia?
 

Ambao wanaamini nyoka hana sumu huku anawaua! Nasema Wabongo ngozi ya goti, kwa sababu wanashindwa kuona nini kinaendelea duniani hivi sasa! Uchumi umeharibika kabisa, na sasa viinchi vyetu hivi ambavyo vinakwenda kimatonyamatonya, haijulikani vitakuwa wapi baada ya miaka hii kadhaa ijayo?
 

Wabongo wanaonyesha kutotikisika kabisa, wanadhani maisha yataendelea hivi hivi? Hawaoni wenzao huko Ughaibuni wanavyohaha. Matajiri wanahaha, je masikini, fukara hohehahe kama sisi ndo tunafanya nini kujinusuru? Tumekalia ubishi, malumbano na kutukanana tu.
 

Kila kukicha unasikia nanihii kaoa, ukigeuka huku tunaulizana Kagoda ni nani? Ukichungulia huku unamkuta mwanasiasa anasema namfahamu Kagoda, mwambie mtaje, anarudi nyuma! Ukimuuliza hali ya uchumi ikoje anakwambia tunamwachia Mungu! Huu si usabato masalia kweli huu!
 

Wabongo sisi yetu ni majungu hatuoni mbele, hatutafuti suluhisho la matatizo, kunakucha, kunapambazuka, linakuchwa, tunajadili Richmondi, Dowanz na Pawa Pulu tupu, hakuna kingine kweli? Hivi matatizo yetu yamekwisha?

 

Hivi tukisema fulani kaoa dogodogo ndiyo matatizo yetu yatamalizika? Tukilipia kumbi na kuhanikiza kuwa Kagoda ni mwizi au fulani ni fisadi kuanzia nywele hadi kucha ndipo tutaweza kula milo minne kwa siku? Bahati mbaya hata sisi vimasikini kunuka, tunashabikia, tunatumiwa bila kujua na umasikini unabaki pale pale. 

Haya angalieni jinsi vitegemezi vyetu vinavyohangaika kufika shuleni, kisa eti wenye vipanya nao wana kijiserikali chao, wamejifanya ni akina Rajoelina, Dijei aliyeingia Ikulu hivi hivi tu, kumbe udijei unasaidiasaidia mtu kuingia Jumba Jeupe? Freeman upo? (Natania tu mshikaji).
 

Angalia akina mama zetu bado hawalali ili kuwania maji alfajiri, tena kwa kupanga mawe kwenye mabomba kama si visima vya maji chumvi, kama enzi zetu zilee za mgao wa nunua kilo ya sukari upate sabuni. Akina mama zetu wanavyohangaika kujifungulia chini na kuua vichanga.
 

Hivi sasa kukicha asubuhi ni sawa kabisa na kichanga kuzaliwa, yaani lazima ulie tu, kwa sababu hujui kama litakuchwa salama na una kitu cha kula na kulisha vitegemezi! Wabongo bado tu wapofu hili hatulioni, tunayaacha yaende hivyo hivyo, kwa sababu tunamwachia Mungu.
 

Ninyi ni Wasabato Masalia wahedi. Maovu mengi yamejifutika huko tunakoishi na huko tunakokwenda kila asubuhi kuganga njaa. Tunayaona na kuyafumbia macho eti mpaka Mrisho aje au Mizengo aje. Wasipong'aa sehemu hiyo au Mrisho asipokuiteni pale Jumba Jeupe hakuna kitu kinafanyika.
 

Hivi ni kweli haya? Kwa huu mdororo, mtikisiko, mvurugano na mkanganyiko wa uchumi duniani humu, kuna haja ya kuendelea kuwa na vigogo wooote hawa ndani ya Sirikali au 'tupigane panga' ili kila mtu ajiju? Eeh sasa mnawasaidiaje ndugu zetu hawa ambao wanalivalia njuga hili huku sisi tunalitafunia njugu! Nakuoneni tu sasa mmeanza kutoana macho, mwaka huo unaokuja patachimbika tu.
 

Mmewakwepa walalahoi hawa muda wote huu, na sasa mnajongea mkijipitishapitisha na kujifanya wakarimu kutoka Mbinguni, huku wengine mkidhani mmechanjiwa majimboni hamtaki vimbwenelehi vikaingia humo. Mmeanza kuwauliza mlikwina nasi tutakuulizeni mlikwina. Vichwa vyenu. Msitubabaishe, tatueni matatizo yetu kwanza. Ala!
 

No comments: