WAFANYAKAZI wenzake na marehemu katika Hoteli ya Mwanza, ambao hawakupenda majina yao yatajwe gazetini, wameibua mambo mapya kwa kutoboa siri za Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi na Mwanasheria Mkuu wa zamani wa serikali, kwa kueleza uhusiano wake na mmoja wa Marehemu Vicky ulivyokuwa kabla ya ajali...Taarifa hizo zimepatikana kufuatia utata uliojitokeza juu ya kuwepo kwa mahusiano ya karibu kati ya Mh. Chenge na marehemu kabla ya ajali hiyo ya Machi 27, mwaka huu iliyotakana na gari la mheshimiwa huyo aina ya Hilux Pickup kugonga Bajaji yenye namba za usajili T 736 AXE na kuua watu wawili, ambapo walidai kuwa kila alipokuwa Mwanza alikuwa akipumzika Kings Casino mahali ambapo Vicky alikuwa akifanya kazi ya uhudumu.
Wafanyakazi hao waliendelea kusema kwamba Chenge alikuwa akipendelea kuhudumiwa na wahudumu watatu tu ambao ni mmoja wa Marehemu Vicky, Asha na Salome waliokuwa karibu naye sana na walipokosekana basi alikuwa akiwaulizia na hakutaka ahudumiwe na mwingine yeyote zaidi ya hao.
Katika kuunga mkono hilo Mama wa Marehemu Vicky aitwaye Nadhifa Kambi akiongea na moja ya Gazeti la kila siku alinukuliwa akisema kuwa binti yake huyo amekuwa akiwasiliana na Mbunge huyo mara kwa mara anapokuja Mwanza na mara nyingine hata akiwa mapumzikoni amekuwa akimwita amuhudumie katika Casino hiyo iliyoko jijini Mwanza.
Duru zaidi za habari kutoka kwa wafanyakazi hao, zilikanusha kuwepo kwa mahuhusiano ya kimapenzi baina ya Mh. Chenge na wasichana tajwa, na kusisitiza kuwa uhusiano wao ulijikita kwenye huduma pekee.
“Ni kweli kuwa kila wakati mheshimiwa (Chenge) anapokuwa Mwanza hufikia Hotel ya Mwanza ambapo ndani yake kuna Kings Casino, lakini uhusiano wake na marehemu Vicky na wasichana tunaowataja hapa, huwa ni wa kikazi tu na si vinginevyo,” alisema mmoja wa wafanyakazi wenzake marehemu kwa njia ya simu.
Aidha, wakati hayo ya ukaribu yakifafanuliwa, suala la mwanamke aliyekuwepo naye kwenye gari lake siku ya ajali ambalo nalo lilizua utata, sasa limewekwa wazi na baadhi ya mashuhuda waliokwenda eneo la tukio kwa mara ya kwanza, kutoa msaada.
Mashuhuda hao walisema kwamba mara walipofika kwenye eneo hilo walimkuta dereva wa Bajaji iliyogongwa akiwa na miili ya Marehemu Vicky na Beatrice Constantine na msichana mmoja kwenye gari la Chenge ambaye walimtambua kama mtoto wake ingawa haijulikani mara moja walikokuwa wakitoka usiku huo.
Uwazi lilipowauliza walivyothibitisha kama yule alikuwa ni mtoto wa Chenge na si mwanamke wa kawaida, walisema kwamba waliyasikia mazungumzo yao ambapo msichana alimuita mheshimiwa kwa kiingereza dadi.
“Tulisikia yule msichana akisema, ‘Daddy are you okay?’ naye akajibu ‘I’m okay’ na msichana huyo ambaye kwa sura anafanana na Mh. Chenge tulimuona Kituo cha Polisi Osterbay wakati mbunge huyo alipokuwa akishikiliwa,” alisema shuhuda mmojawapo.
Akielezea kuhusu tukio hilo, Dada wa marehemu aitwaye Rena Ndosi alisema kuwa, marehemu Vicky alifika Dar es Salaam akitokea Mwanza Jumatatu ya wiki iliyopita akija kuagana na rafiki yake wa kiume (jina kapuni) ambaye alikuwa akielekea Australia.
Rena anazidi kusimulia kuwa, Marehemu ilipaswa asafiri kuelekea Mwanza siku iliyofuata ingawa kwa siri alielekea Klabu ya Usiku ya Maisha akiwa na rafiki yake Beatrice kwa lengo la kutoka hapo na kuelekea Stendi ya Mabasi Ubungo ili kuanza safari.
Hata hivyo wakati wakitoka katika klabu hiyo ya Usiku kwa lengo la kwenda Ubungo walikutwa na ajali hiyo mbaya na hatimaye mauti.
Kuhusiana na taarifa zilizokuwa zimezagaa kwamba, marehemu Beatrice alikuwa akimpeleka Vicky kuolewa Zanzibar, Rena alikanusha kwa kusema kuwa hiyo ilikuwa ni ‘gea’ ambayo rafiki huyo wa mdogo wake aliitumia kupata ruhusa kwa ndugu zake ili waende Klabu.
Kulikuwepo na utata uliojitokeza juu ya namna ambavyo miili ya marehemu ingesafirishwa kwenda Mwanza hali iliyopelekea ndugu wa Vicky na wasamaria wema kutoa fedha zao kuifanya kazi hiyo kufuatia kutoelewana na Mh. Chenge ambaye hapo awali alitakiwa awasafirishe.
Hata hivyo siku iliyofuata (Jumapili), kwa mujibu wa Ndugu mmoja wa Marehemu. Mh.Chenge aliahidi kutoa laki saba ‘vijisenti’ kwa kila familia iliyokutwa na msiba husika ili kusaidia shughuli za mazishi ikiwemo na usafirishaji wa miili yao kwenda Mwanza kuzikwa.
Wakati huohuo Christopher Lissa anaripoti kuwa, Mhe.Chenge jana amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka matatu, ambapo mawili ni kusababisha vifo vya watu wawili na kosa la tatu ni uzembe barabarani.
Mwendesha mashtaka wa Polisi David Mwafimbo alidai mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo Emerius Mchauru kuwa mnamo Machi 27 majira ya Saa 9 Usiku katika makutano ya Barabara za Karume na Haileselassie Oysterbay Jijini Dar es Salaam Chenge akiendesha gari yenye namba za usajili T512 ACE aina ya Toyota Hilux Pick up alisababisha ajali kwa kuigonga Pikipiki aina ya Bajaji yenye namba za usajili T736 AHE na kusababisha vifo vya watu wawili.
Hata hivyo Chenge alikana makosa yote na aliachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambapo alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja na Shilingi Milioni moja.Kesi imeahirishwa hadi April 30 mwaka huu itakapotajwa tena.
Katika hali ya kushangaza mara baada ya kigogo huyo kusomewa mashitaka alitolewa kwa siri mlango wa nyuma na kuwahishwa kwenye gari kisha gari hiyo kuondolewa kwa kasi mahakamani hapo.
Tuesday, March 31, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment