Waziri Mkuu Mstaafu
ahofia mgawanyiko
| ||||
| Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba, ametoa tahadhari kuhusu Dowans kuligawanya Bunge Tanzania | ||||
![]() |
SUALA la ununuzi wa mitambo ya umeme ya Dowans, linazidi kuchukua sura mpya baada ya Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba kusema malumbano yanayoendelea kati ya Kamati za bunge na wabunge yanaonyesha kuna mgawanyiko ndani ya bunge.
Katika majibu yake kwa Mwananchi Jumapili, Warioba alisema malumbanano kuhusu suala la mtambo wa umeme ni jambo la kushangaza kwani ununuzi wa bidhaa na huduma ni kazi ya serikali.
Alisema sheria, kanuni na taratibu zipo, hivyo serikali inaweza kuzitumia bila ya kutaka maoni ya bunge na kwamba hata kama ni dharura pia kuna kanuni na taratibu zake.
" Inakuwa vingumu kuelewa kwa nini Serikali ilipeleke suala la ununuzi wa mtambo wa umeme kwenye kamati ya Bunge. Inaonekana kama ni njia ya kukwepa lawama za kisiasa au kukwepa wajibu," alisema.
Maoni hayo ya Warioba yamekuja wakati kamati mbili za bunge tayari zikiwa katika mvutano mzito, moja ikitaka inunuliwe na nyingine ikipinga.
Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, chini ya Mwenyekiti wake, William Shelukindo imeshakataa kulipa baraka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco ) kununua mitambo hiyo kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria ya manunuzi, huku kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe imeamua inunuliwe ili kunusuru taifa na giza.
Warioba alisema cha kushangaza zaidi kuhusu jambo hili ni jinsi wabunge walivyochangamkia suala hili huku wanajua kwamba siyo kazi ya Bunge kujihusisha na maamuzi ya utekelezaji.
Warioba alihoji " Kwa nini Kamati za Bunge zimekubali kupokea na kuzungumzia suala ambalo haliwahusu?
Hata hivyo, alisema tatizo kubwa la nchi ni kupata umeme wa kutosha hivyo, tuzungumzie hilo badala ya malumbano ambayo hayatuongezei umeme.
Alishauri bunge na wabunge wafanye kazi ya kusimamia, siyo kutenda na kwamba wasihangaike kusaka nyaraka za serikali ili wapeleke hoja bungeni kwa mambo ambayo ni ya utendaji.
Warioba alisema hoja binafsi ni kitu kizuri, lakini bunge ni lazima liwe makini kuangalia ni hoja gani zinaambatana na kusimamia utendaji na ni hoja zipi zinaliingiza bunge jikoni.
Alionya kwamba bunge limeanza kuingilia madaraka ya serikali na mahakama ingawa limekuwa likijitetea ukweli ni kwamba Bunge limekwenda nje ya madaraka yake limejichukulia hata madaraka ya kutafasiri sheria ili kuhalalisha maamuzi yake.
Hata hivyo, jana Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Idrisa Rashid juzi alitangaza rasmi kujitoa katika ununuzi wa mitambo yenye utata wa kufua umeme ya dharura Dowans Tanzania na kueleza kuwa hospitali zitakaposhindwa kutoa huduma asilaumiwe.
Alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona mwelekeo wa suala hilo linatupeleka kwenye ugonvi wa wanasiasa, jukwaa ambalo sisi hatuna mamlaka nalo.
Warioba pia alivionya vyombo vya habari kuwa navyo hivi sasa vimekumbatia suala moja tu la ufisadi kwa kiwango cha ajabu.
Alisema mahakama zinazosikiliza kesi za ufisadi zimegeuka kuwa ni kumbi za kupatia habari habari kwa waandishi na kwamba taarifa kutoka mahakamani zinapewa kipaumbele katika vyombo vyote na zinaandikwa kwa kirefu.
Alisema upungufu wa chakula, kushindwa kuuza marobota ya pamba, Kampuni ya Barrick kujitoa kwenye mradi wa umeme wa kusini ni habari za kupita ambazo hazipatiwi umuhimu unaostahili.
Warioba alisema uchumi wa dunia utakuwa katika matatizo kwa kipindi cha miaka miwili mitatu au zaidi, kasi ya kukua kwa uchumi wa Tanzania utapungua na mfumko wa bei utapanda.
"Watu watapoteza kazi na wahitimu wa elimu watakosa kazi. Wateja wa wafanya biashara watapungua kwa sababu ya kupanda bei. Bei ya mafuta imepungua lakini uchumi wa nchi kubwa ukitulia mafuta yatapanda bei na nchi ndogo zitapata matatizo zaidi,"alisema .
Alisema katika hali hii tuweke pembeni tofauti zetu za itikadi, makundi na mitandao kila taasisi ielekeze nguvu kwenye matatizo ya uchumi ili watu wengi wakatumia matatizo ya njaa katika uchaguzi mkuu kununua wananchi.
" Mwaka kesho ni mwaka wa uchaguzi. Katika mwaka wa uchaguzi maamuzi magumu hukwepwa. Lakini tusipolivalia njuga suala la uchumi tunaweza kuingia kwenye kipindi cha uchaguzi wakati watu wana njaa, wengine watakuwa wamepoteza kazi na wengine wanashindwa kupata kazi.
" Tunaweza kuwa na uchaguzi wenye uchafu kuliko ilivyotokea huko nyuma. Wenye fedha watatawala na kununua uchaguzi kwa takrima," alisema.


No comments:
Post a Comment