
Chokochoko za
Na Salim Said
SIKU chache baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutamka kuwa suala la gesi asilia na mafuta visiwani humo si la muungano, wabunge wawili wameitaka serikali kuchukua hatua za haraka ili kuinusuru nchi.
Wamesema migogoro ya muungano inasababishwa na katiba ya Jamhuri na kwamba iwapo serikali itaendelea kukwepa mambo hayo, yatakuja kulipuka na kuingiza nchi katika matatizo makubwa.
Mbunge wa Karatu Dk Wilibrod Slaa alisema jijini Dar es Salaam jana, matatizo ya muungano yanasababishwa na katiba na kwamba yanafukuta chini kwa chini huku akionya kuwa iko siku yatalipuka na nchi kusababisha mpasuko katika nchi.
“Ndivyo katiba inavyosema” alijibu Dk Slaa alipoulizwa kuhusu tamko la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na kuongeza:
“Matatizo ya muungano ni ya kwetu, kwa nini tuyakatae? Tutapata matatizo makubwa nchini ikiwa tutaendelea kujifanya wajanja. Nchi itapasuka kwa sababu mambo haya yanafukuta chini kwa chini na kwa muda mrefu”.
Alisema, iwapo serikali haitakubali kutambua kasoro za muungano na kuzirekebisha kikatiba, nchi itaingia katika matatizo makubwa.
“Mambo ya msingi katika muungano yalikuwa 11 tu, lakini yameongezwa bila ya kufuata utaratibu na sasa ndio yanaleta mgogoro huu,” alisema Dk Slaa.
Alisema, chanzo cha matatizo yote hayo, ni katiba na kwamba dawa yake ni kuitisha mjadala wa wazi wa kitaifa kwa ajili kujadili matatizo ya kikatiba na muungano.
“Miaka 48 ni mingi sana kuwa na katiba isiyopitiwa na kurekebishwa, hata ndoa watu husherehekea kufikia miaka 25 au 50, wenyewe hukaa na kuangalia wamekosea wapi na kipi cha kurekebisha,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Kwa nini isiwe katiba au makubaliano ya muungano. Haya ni ya kwetu tu, tunayo tu tunaogopa nini? Yatatuletea matatizo baadae."
Dk Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alihoji kuwa kama mafuta ni suala la muungano kwa nini yamewekewa wizara yake Zanzibar.
Alihiji pia ni vipi wazanzibari wanafaidika na gesi asilia ya Songas kwa kuwa nayo ni mfano wa madini yaliyopo Zanzibar.
Kwa upande wake Mbunge wa Micheweni kisiwani Pemba, Shoka Khamis Juma alisema, mkataba wa muungano umepotoshwa na kwamba kuna mambo mengi yaliyoongezwa kinyemela.
Alisema, asili ya mambo ya muungano ni 11, lakini kuna wajanja waliyaongeza kinyemela hadi kufikia 24 hivi sasa, jambo ambalo ni kinyume cha makubaliano ya Rais Abeid Karume na mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
”Sisi Zanzibar hatuna vitegauchumi vingi vya kutuendeleza ukilinganisha na wenzetu bara, wao wana viwanda, madini, gesi na hata ardhi kubwa lakini, je sisi tunafaidika vipi na mambo hayo,” alisema na kuongeza:
“Hawajatosheka tu mambo yote hayo, na hii tembe ya mafuta ambayo hata hayajathibitisha kuepo kwake hawataki kutuachia”.
Shoka alipendekeza kuwa, kufanyike mazungumzo ya kitaifa kuhusu masuala ya muungano au kutangazwe mgogoro wa kikatiba, ili ipitiwe na kurekebishwa kwa kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa matatizo haya.
Masuala ya muungano yamekuwa yakisumbua serikali kwa muda mrefu, ambapo rais Jakaya Kikwete aliunda kamati maalumu ya kushughulikia kero za muungano.
Hivi karibuni SMZ iliwasilisha tamko lake katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na kukataa kabisa kulihusisha suala la mafuta yaliyomo visiwani humo kuwa la muungano huku ikitaka uchimbwaji wa mafuta hayo usimamiwe na SMZ kwa maslahi ya watu wake.
Kutoka gazeti la Mwananchi

No comments:
Post a Comment