
hakuna kugawana
mapato ya mafuta!
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetupilia mbali taarifa ya mshauri mwelekezi kuhusu mgawanyo wa mafuta na gesi asilia na kutaka suala hilo sasa kuondolewa katika mambo ya Muungano. Inataka masuala ya mafuta na gesi asilia kuondolewa katika Muungano, kwa madai yaliingizwa kinyemela huku Zanzibar ikidai haifaidiki na mgawanyo wa rasilimali za gesi za Tanzania Bara.
Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansoor Yussuf Himid aliyasema hayo jana katika Baraza la Wawakilishi alipowasilisha ripoti ya mshauri mwelekezi kuhusu mgawanyo wa mafuta na gesi asilia. Himid alisema ripoti ya Mshauri Mwelekezi imetaka suala la mafuta na gesi asilia kubaki katika mambo ya muungano, lakini imeshauri kuwapo kwa wizara ambayo itaratibu masuala hayo katika Muungano.
Aidha, katika ripoti hiyo imetaka kuundwa kwa chombo kipya kitakachoshughulikia na kusimamia pamoja na uchimbaji na utafutaji na utoaji wa leseni ya mambo ya mafuta.
Himid alisema katika ripoti ya mshauri mwelekezi, imegundua kwamba Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), halina sura ya Muungano. Kwa sasa shirika hilo yupo Mjumbe mmoja wa Bodi kutoka Zanzibar, hali inayodaiwa inaonyesha halipo kwa ajili ya maslahi ya Wazanzibari kwa ujumla.
Aidha, alisema shirika hilo limeundwa kwa mujibu wa amri ya rais mwaka 1969 na kuundwa tena kwa mujibu wa sheria ya mashirika ya umma, lakini hata hivyo halijapata baraka na kupitishwa na chombo kinachotunga sheria cha Baraza la Wawakilishi, hivyo ni batili na haliwezi kufanya kazi zake Zanzibar.
Huku akishangiliwa kwa makofi na wajumbe wa pande mbili kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wapinzani CUF, Himid alisema kitakuwapo chombo chenye mamlaka ya kutoa leseni ya uchimbaji wa mafuta kwa kampuni mbalimbali za nje kitakachofanya kazi Bara na hivyo Zanzibar kukosa mapato. “Katika hili, tumegundua Zanzibar itakosa mapato yake makubwa kwa makampuni ya kuchimba mafuta ambayo yatasajiliwa Tanzania Bara...hili litainyima mapato mengi Zanzibar,” alisema.
Alisema Zanzibar haikubaliani na baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na mshauri mwelekezi kutokana na kuwapo kwa upungufu mwingi huku Zanzibar na Tanzania Bara ikiwa na sheria zinazotofautiana, ikiwamo ya mambo ya umilikaji wa ardhi. Alisema mapendekezo ya SMZ kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, suala la mafuta kuondolewa katika mambo ya muungano kwani hapo awali halikuwa katika orodha hiyo kwa mujibu wa sheria.
Alisema hadi sasa Zanzibar haijafaidika na mapato yanayotokana na mauzo ya gesi asilia ambayo tayari inazalishwa Tanzania Bara, ikiwamo katika maeneo ya Songosongo na Mnazi Bay. “Suala la mafuta na gesi ni mambo ya muungano, lakini hadi sasa Zanzibar haijafaidika na mapato yanayotokana na uzalishaji wa gesi na mafuta,” alidai Himid ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Alisema Tanzania Bara zipo maliasili nyingi ambazo hazijaorodheshwa katika mambo ya muungano na Zanzibar haifaidiki nayo ikiwamo almasi, tanzanite, mafuta na gesi. Alisema ushauri wa mtaalamu aliyeletwa kwa ajili ya kufanya mgawanyo wa mafuta na gesi ambaye anataka suala hilo kuwa la muungano, lakini linaweza kusababisha matatizo makubwa na linaweza kuleta mvutano wa hali ya juu.
“Kama itakuwa suala la mafuta ni bora kubakia katika mambo ya muungano basi suala la marekebisho ya Katiba linahitajika kwa sababu Zanzibar haifaidiki na mafuta na gesi iliyopo Bara,” alisema. Alitahadharisha na kusema suala la mafuta katika nchi zenye muundo wa muungano au shirikisho limeleta matatizo makubwa na ugomvi wa watu kuuana, ikiwamo Nigeria na India.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na SMZ ilitafuta mshauri mwelekezi kwa ajili ya kupata mgawanyo mzuri wa rasilimali za mafuta na gesi itakayozalishwa nchini. Mshauri huyo kutoka Uingereza, Aupec Limited alimaliza kazi yake na ripoti hiyo kuiwasilisha kwa serikali zote mbili.
Miongoni mwa mambo yaliyomo katika orodha ya muungano wa nishati na mafuta ya gesi inayopatikana katika sehemu yoyote ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini Zanzibar inadai mambo ya mafuta na gesi yaliingizwa kinyemela bila ya kupata ridhaa kwa upande wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment