Hivi Taifa letu lipo
salama kweli?
WATANZANIA huwa hatukosi mijadala. Kuthibitisha hilo, hebu angalia. Wiki moja tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kuuzima mjadala wa Dowans, umeibuka mjadala mwingine wa DECI.
Mjadala wa DECI umeibuliwa na viongozi wa Benki Kuu (BoT) na Mamlaka ya Masoko ya Dhamana na Mitaji (CMSA). Vyombo hivyo vimetoa hadhari kwa wananchi kujiepusha kuwekeza fedha katika DECI, wakisema hawana leseni wala uhalali wa kuendesha shughuli za upatu.
Kwenye tangazo lao kwenye magazeti, wanasema hivi: “Mamlaka zinazohusika zimekwishaanza upelelezi wa kina kuhusu shughuli za DECI (T) Limited ili kujiridhisha juu ya upeo wa mtandao wake na misingi ya shughuli hizo. Kwa sasa umma unatahadharishwa kutoshiriki kwenye biashara ya ‘Vuna Kutokana na Mbegu Uliyopanda’.”
Nimetumia mfano huu hali wa BoT na CMSA kujaribu kueleza udhaifu mkubwa walio nao viongozi katika kukabiliana na mambo yanayotuzunguka.
DECI ilianzishwa mwaka 2002 kama taasisi ya kidini, ikilenga zaidi kuwashirikisha waumini wake katika kujipatia fedha ili kuondokana na ukata wa kupindukia.
Lakini ni miaka mitatu sasa tangu ianze utaratibu huo wa “Vuna Kutokana na Mbegu Uliyopanda” Fikiria. Ni miaka mitatu sasa tangu watu waanze “kupanda na kuvuna”.
Miaka mitatu baada ya shughuli kushamiri, ndipo viongozi wetu wa BoT na CMSA wameamua kuzomoka na kuihadharisha jamii!
Kwanza, nisema wazi kwamba sitetei wala sipindi uwapo wa DECI au shughuli inazoendesha. Wataalamu wa fedha pamoja na wanachama wa upatu huo, ndiyo wenye haki ya kuamua.
Hofu yangu ni kwa vyombo vya ulinzi na usalama katika nchi yetu. Tunapoambiwa na Gavana miaka mitatu baada ya shughuli hizo, ya kwamba upelelezi wa kina umeanza, maana yake nini?
Miaka mitatu yote walikuwa wapi? Inakuwaje chombo kisajiliwe, kipate wanachama na viongozi, kifungue ofisi, kivute maelfu kwa maelfu ya wananchi kwa miaka mitatu bila mamlaka husika kuwa na taarifa?
DECI hao hao wamekuwa wakilipa kodi kubwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Hawa wanafurahi kuwa na chanzo hicho. TRA ni serikali. Je, sheria za ukusanyaji mapato zinawaruhusu kukusanya fedha kutoka popote bila kuhoji uhalali wa chanzo cha mapato husika? Kama DECI hawa si halali, kwa nini fedha za kodi ziwe halali? Au ndio msemo wa baniani mbaya kiatu chake dawa?
Ninachojaribu kudadisi hapa ni uwezo wa utendaji kazi wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hapa nchini. Hili la DECI ni moja tu kati ya mifano halisi mingi.
Tuna viongozi wengi ambao wapo kwa sababu wapo. Tuna viongozi waliobweteka na kujisahau kabisa, wakijiona kama wao ni wa mpito! Ukiwatazama viongozi wetu, utadhani wameshika madaraka kwa muda wakisubiri viongozi ‘halali’ waje.
Mawaziri wanajiona kama mawaziri wa mpito. Badala ya kushughulikia mambo na kuyamaliza, hawafanyi hivyo. Akili zao zinawatuma kuwa wao ni mawaziri wa mpito tu. Kama akili zao haziwatumi hivyo, bila shaka tungeona mambo ya maana kutoka kwao.
Nchi hii ina Idara ya Usalama wa Taifa. Sijui, lakini ni vigumu sana kuwaaminisha wananchi kwamba Usalama wa Taifa wa Tanzania, ni usalama wa Taifa kweli. Wameajiriwa vijana wengi wenye mbwembwe, hasa wanapokuwa na viongozi wa kitaifa.
Zamani, usalama wa taifa walikuwa waibuaji wa mambo makubwa katika nchi. Tuliishi na usalama wa taifa, lakini hatukuwajua. Walipiga kambi vijijini. Wakalima vibarua katika mashamba, wakaajiriwa kupeleka mifugo machungaji.
Wengine tuliowaona vichaa, kumbe walikuwa kazini. Kwa mwonekana walikuwa wachafu, wengine walevi, mara kadhaa walithibitisha hilo hata kwa kutoa matusi, lakini mwisho wa siku, walichokwenda kukifanya kilionekana.
Leo tuna usalama wa taifa ambao wanashinda baa. Hawashindi kwa sababu wanavizia jambo, wanashinda kwa sababu wana fedha za kulewa.
Wanakunywa na kucheza dansi, huku wengine wakipoteza fahamu. Kama ofisa wa aina hiyo anaweza kulewa, akabebwa au akapoteza simu, kweli kuna usalama wa taifa hapo?
Haishangazi siku hizi usalama wa taifa kujitambulisha kwenye hadhara. Hukosi kusikia, “jamaa anafanya kazi Ikulu!” Hakuna mahali ambako utambulisho wa namna hiyo unaweza kumsaidia mtu kufanya kazi nyeti aliyotumwa na taifa lake.
Nahoji haya kwa sababu haiwezekani chombo kama DECI kianzishwe, miaka mitatu baadaye wajitokeze viongozi wakubwa waseme wanafanya uchunguzi.
Ilipaswa suala kama hilo , usalama wa taifa, makachero wa polisi na wengine, wawe wameshafanya utafiti ili kubaini kama kweli chombo hicho kina manufaa. Maana kama wananchi kweli watakuwa wamewekeza, ikatokea fedha zao zikapotelea huko, wa kulaumiwa ni vyombo vya dola.
Vyombo vya dola ndivyo vinavyopaswa kuwa na “akili” zaidi ya wananchi. Hapa namaanisha kwamba vyombo hivyo vina watalaamu wenye uwezo wa kujua lipi baya, au lipi jema. Inapobainika kuwa kuna jambo baya, vyombo hivyo vinatakiwa vilizime mara moja bila kusubiri.
Umakini wa vyombo vya usalama hasa kwa wakati huu ambao wananchi wanakabiliwa na msongo wa maisha, ni muhimu mno. Vyombo vya utambuzi sasa vinatakiwa vifanye kazi zake kwa umakini na kwa kasi ili kuwaepusha wananchi na mambo ya hatari.
Hizi ndizo zama tulizoona wanaibuka watu kama kina Kibwetere ambao waliweza kuwarubuni watu kwa imani za kijinga na kusababisha maafa makubwa. Sasa tunao wengine wanajiita Sabato Masalia.
Hawa wanaota kwenda Ulaya bila kuwa na hati za kusafiria wala viza. Wamepiga kambi. Kuna mauaji ya albino. Kisa cha mauaji hayo ni imani kwamba ukiwa na mfupa au ngozi ya binadamu wa aina hiyo, basi wewe ni tajiri!
Mambo haya ni mengi mno. Hatuwezi kukataa kwamba yanachochewa na ugumu wa maisha. Inapotokea kasi ya kuwapo kwake ikawa haiendi sambamba na kasi ya kuyachunguza na kuyazuia, matokeo yake ni kuwaingiza wananchi kwenye matatizo makubwa. Vyombo vya usalama vina wasomi.
Moja ya kazi kubwa ya wasomi ni kuwalinda wananchi dhidi ya mambo yasiyo na manufaa kwao.
Lakini hatuoni kama kweli wasomi, viongozi na watu waliopewa dhamana ya kuwalinda wananchi, wanawajibika ipasavyo.
Ukiacha suala la DECI, kuna mambo mengine mengi mno ambayo viongozi wetu wa usalama wamelala na kusababisha adha kubwa.
Kwa mfano, sasa nchi yetu inakabiliwa na wimbi la watu wengi wasio raia. Hao ndiyo wenye pasi za kusafiria za Tanzania na haki nyingine nyingi kuliko Watanzania wenyewe.
Eneo kama Sinza kuwa wageni wengi mno kutoka mataifa jirani na ya mbali. Wageni hawa wanaendesha shughuli ambazo zingeweza kufanywa na Watanzania. Nimeshuhudia katika duka moja Sinza kuna wahudumu wanaotoka nchi jirani. Fikiria. Watu kama hawa wanaingia na kuajiriwa, huku watu wetu wa usalama, tena wakiwa wateja wa sehemu hizo, wakiwaangalia tu.
Tumekuwa na wageni waliojipenyeza na kushika nyadhifa kubwa kwenye chama tawala, serikali na katika vyombo nyeti vya usalama. Watu hawa wameachwa hivi hivi kwa miaka yote. Wameshitukiwa wakiwa wameshajua kila kitu chetu. Alijitokeza bwana mmoja, Peter Kinyanjui, aliongoza Chama cha Soka Tanzania (FAT) hadi alipoumbuliwa. Akakimbilia kwao Kenya . Tumekuwa na viongozi wakubwa tu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao si raia, huku wakiwa wamezungukwa na maofisa usalama wetu.
Kama mtu anaweza kujipenyeza hadi akashika wadhifa wa juu kabisa katika nchi, hali ikoje mitaani? Bila shaka hali ni mbaya zaidi. Huko kuna wageni waliohodhi ardhi. Wananchi wanawajua kuwa ni wageni, lakini watu wa ulinzi na usalama hawataki kuwasumbua!
Tumefikia hatua hii mbaya kutokana na udhaifu wetu. Hatuna makachero. Kama tunao, basi wengi wao ni wala rushwa.
Uzalendo kwa nchi yao hawana. Makachero wa leo, kuwapa habari ya kuwapo kwa watu hatari mahali fulani, maana yake ni kuwapa mtaji wa kununua magari au kujengea nyumba.
Kutoka gazeti la Rai
No comments:
Post a Comment