Kandoro aondolewa
Dar es Salaam
Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa kwa kuwahamisha 11 kutoka vituo vyao vya sasa vya kazi, huku Waziri wa zamani, William Lukuvi akiwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa imesainiwa na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri, lengo la mabadiliko hayo ni kutoa msukumo zaidi wa shughuli za serikali. Katika mabadiliko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro aliyeteuliwa kushika wadhifa huo takribani miaka mitatu iliyopita akitokea Arusha, sasa anahamia Mwanza, akimpisha Lukuvi anayehamia kutoka Dodoma.
Katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Lukuvi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. James Msekela anahamia Dodoma. Wakuu wa mikoa wengine waliobadilishwa ni Enos Mfuru kutoka Kagera kwenda Mara, Issa Machibya kutoka Mara kwenda Morogoro, Said Kalembo kutoka Morogoro kwenda Tanga, Mohamed Abdulaziz kutoka Tanga kwenda Iringa na Amina Mrisho kutoka Iringa kwenda Pwani.
Wengine ni Dk. Christine Ishengoma kutoka Pwani kwenda Ruvuma, Monica Mbega kutoka Ruvuma kwenda Kilimanjaro na Mohamed Babu kutoka Kilimanjaro kwenda Kagera. Mbali ya kuwa wakuu wa mikoa, Lukuvi, Mbega, Ishengoma, Abdulaziz na Msekela pia ni wabunge. Mabadiliko hayo ya wakuu wa mikoa yamefanyika wiki tatu tangu Rais Kikwete afanye uteuzi wa wakuu wa wilaya kwa kuteua wapya 15, kustaafisha saba na kuwabadilisha vituo vya kazi 54.
1 comment:
Rais Kikwete ameanzia na wakuu wa wilaya, halafu wakuu wa mikoa. Je, ni mawaziri wanaofuatia? Yetu masikio na macho!
Post a Comment