Thursday, April 16, 2009



Rais Kikwete

ziarani Saudi Arabia


Mfalme wa Saudi Arabia, Abdullah bin Abdulaziz al Saud, amemtunukia Rais Jakaya Kikwete, Medali ya Watu Maalumu iitwayo Abdulaziz, akiwa ni Rais wa kwanza kutoka Afrika kupewa medali hiyo. Mbali na medali hiyo, Rais Kikwete amekuwa Rais wa kwanza pia kufanyiwa dhifa ya kitaifa nyumbani kwa mfalme. Kwa kawaida hapa, mawaziri ndio hupokea wakuu wa nchi na kuwafanyia dhifa. 

Akizungumza jana na waandishi wa habari juu ya mapokezi ya Rais Kikwete, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Idd, alisema ziara hiyo imepewa heshima kubwa ambayo hajawahi kupewa kiongozi yeyote wa Afrika. “Kabla Rais Kikwete kuja hapa, walikuja marais wa Uturuki na Senegal na wote walipokewa na mawaziri, bila mapokezi makubwa ya aina hii. Pia kuna orodha ya marais wengi wanataka kuja, lakini Rais Kikwete amepewa kipaumbele,” alisema Balozi Idd. 

Rais Kikwete anakuwa Rais wa kwanza kutoka Tanzania kufanya ziara nchini hapa tangu kufunguliwa kwa Ubalozi wa Tanzania hapa mwaka 1986. Kikwete aliwasili hapa juzi kwa ziara ya kiserikali ya siku nne kwa mwaliko wa Mfalme Abdullah. Katika hatua nyingine, Mfalme Abdullah aliahidi kuisaidia Tanzania katika ujenzi wa barabara ili kusaidia kuboresha usafirishaji wa mazao ya kilimo. Ahadi hiyo aliitoa wakati wa mazungumzo maalumu na Rais Kikwete katika siku ya pili ya ziara yake.


No comments: