Nchi tajiri chanzo na
mwisho wa matatizo
na D. Haji Semboja,
Raia Mwema
MGOGORO au mtikisiko wa sasa wa kiuchumi uliotokea katika soko la fedha ya Marekani, tangu katikati ya mwaka 2007 mpaka mwishoni mwa 2008, umeanza kuleta athari za muda mfupi, wa kati na muda mrefu, katika nchi nyingi zilizoendelea, nchi zinazoendelea na nchi changa masikini zinazoendelea katika Bara la Afrika.
Athari mojawapo za muda wa kati na awali kiuchumi, ni pamoja na kudhoofika kwa mfumo wa kifedha na mabenki, kupungua uwekezaji, kuzorota kwa uzalishaji mali, kupunguka kwa ajira katika sekta rasmi na binafsi, upungufu wa mapato ya serikali, na kuongezeka kwa umasikini katika nchi zinazoendelea.
Mgogoro au mtikikisiko wa kiuchumi dunia wa sasa 2007 - 2009 ulianza kwa kusambaratika kwa soko la fedha na mitaji nchini Marekani, baada ya kusambaratika kwa soko la ujenzi wa majengo na nyumba katika sekta binafsi, mwaka 2007; ambalo lilikuwa linakuwa kwa kasi kubwa.
Athari za awali za kusambaratika kwa soko la fedha na mtaji katika sekta ya majengo na nyumba ndio chanzo kikuu na kiini cha mtikisiko mkubwa wa soko la fedha na mtaji hatimaye kuletea msambaratiko wa kiuchumi katika ulimwengu mzima.
Athari kuu zilizojitokeza katika uchumi wa dunia unaonyesha ishara kuwa sera, sheria, taratibu na taasisi za uchumi wa utandawazi wa sekta binafsi na biashara huria wa kipebari unaweza kuleta athari kubwa kwa jamii, taasisi na sekta zote duniani.
Ni vema kuungalia mkitisiko au mgogoro huu katika mtazamo wa kihistoria ya maendeleo ya uchumi wa kibepari duniani, uchumi huria ambao hauna mipaka wala heshima kwa mila na mataifa mengineyo.
Imetokea migogoro na mitikisiko ya aina nyingi, sababu na athari tofauti katika historia ya dunia. Jambo likitokea kwa mapebari wakubwa, linawakumba waliomo na wasiomo katika mfumo wa maendeleo tegemezi.
Sababu za migororo zimekuwa za kisiasa na usalama. Matokeo ya awali ya athari za mtikisiko ya kisiasa, kijamii na usalama yameibua migogoro ya kiuchumi duniani.
Hatimaye, migogoro hii imeathiri masoko yote ya bidhaa na huduma. Bahati ni kuwa katika kila mgogoro na mtikisiko, jamii ya kimataifa imeweza kushirikiana na kutafuta suluhisho (mfano Marshall Plan, World Bank / IMF), na baadaye zipo jamii na mataifa yalioneemeka.
Hii ndiyo imekuwa desturi ya mitikisiko na migogoro, yaani, baada dhiki na faraja.
Tanzania kama nchi nyingine masikini katika Bara la Afrika imepitia katika mitikisiko au migogoro ya uchumi aina mbalimbali, na kila mara imekuwa inaathirika vibaya.
Hapa tunakumbuka mtikisiko wa uchumi uliotokea baada ya kupanda kwa bei za mafuta ya petroli miaka ya kabla na baada ya vita kuu za dunia, kupanda kwa bei za mafuta mwaka 1973 na 1978 na kuathirika kwa nchi zote zilizoendelea ambazo ni wananunuzi (importers) wa mafuta ya nishati katika miaka ya 1980.
Hivi karibuni, miaka ya 1997- 1998 na 2003-2004 kulitokea mtikikisiko mdogo wa soko la fedha katika Bara la Asia.
Jambo la kushangaza ni kuwa, pamoja na mitikisiko ya uchumi katika vita kuu za dunia, mtikisiko wa sasa umekuwa kabambe na umetishia uchumi wa nchi zilizoendelea zaidi.
Uzuri wa nchi hizi ni kuwa wao wana uwezo wa kutengeneza matatizo na pia wana uwezo wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao.
Tatizo ni nchi masikini na tegemezi kama Tanzania. Tanzania ina uwezo wa kuambukizwa matatizo na sasa ni dhahiri kuwa tutajenga uwezo wa kuomba kuokolewa katika athari za mtikisiko wa uchumi wa dunia.
Mtikisiko au mgogoro huu wa uchumi, mwaka 2007 hadi 2009 ni lazima utambulike kama ni aina mojawapo ya migogoro ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ya muda mrefu ulimwenguni ambayo itaathiri jamii zote duniani kutokana na uhusiano wa utandawazi, teknohama, biashara na mifumo ya sekta binafsi zilizo huru kuvuka mipaka ya nchi zao.
Maendeleo haya ya utandawazi yamefanya benki za biashara kuwa ni taasisi zinazounganisha na kuhusisha mwenendo, tabia, mahitaji na vitendo vya jamii, familia na sekta binafsi na mahitaji yao ya fedha, mitaji na mikopo kwa ajili ya maendeleo yao.
Utandawazi umefanya huduma za benki za biashara kupanuka na kuboreka zaidi, kiasi kuwa wao si tu ni benki za kuweka na kuhifadhi fedha za wateja wao, bali wanashiriki kutoa huduma za ushauri, udalali, kutafuta na kutoa mitaji na mikopo inayohitajika kwa maendeleo ya sekta binafsi.
Huduma hizi zimepanuka katika sekta zote za maendeleo na zinavuka mipaka ya nchi na mabara kutokana na ukuaji wa mashirika na taasisi za kifedha nje ya mipaka ya nchi zao.
Utandawazi umefuatana na kupanuka kwa biashara huria katika soko la fedha, na maendeleo haya yanatokana na maboresho ya mifumo ya sera, sheria na taratibu za nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
Dunia imekuwa kitu kimoja, na huduma za kifedha zinazofanana zipo katika nchi zote kwa faida ya mapebari wawekezaji katika mataifa yao.
Hii inasababisha kuwa sera za kifedha na mabenki ya zamani kushindwa kuzuia maendeleo haya ya utandawazi kutoka nchi zilizoendelea kwenda nchi zinazoendelea, (Dirk Willem, 2008).
Hii ina maana kuwa ipo haja ya kuwa na aina mpya ya maboresho katika soko la fedha na uchumi katika nchi changa.
Katika kipindi cha 1985/1986 mpaka 2007/2008, Tanzania, na Afrika kwa ujumla imekuwa inatekeleza sera na mikakati mbalimbali ya maboresho ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, kwa lengo la kuleta mabadiliko na maendeleo endelevu katika sekta binafsi, soko huria kwa kuboresha sera, sheria, taratibu na taasisi zake.
Mafanikio ya maboresho haya yameonekana kuwa mazuri, walakini sasa upo katika tishio la kukwama kutokana na mtikisiko wa sasa wa uchumi duniani.
Msambaratiko na mikasa ya awali
Inatambulika kuwa, mtikisiko wa soko la fedha duniani umeanza kwa kusambaratika kwa shughuli za mikopo na rehani za mitaji msingi (subprime mortage crisis) Marekani na kuleta mfululizo wa misambaratiko katika hatua au ngazi mbalimbali za aina ya masoko ya mitaji, mikopo na fedha.
Kusambaratika na mtikisiko wa rehani za mitaji msingi ndiyo kiini na chanzo cha mtikisiko wa kiuchumi katika kipindi cha kati ya mwaka 2007 na 2008, ambako baadaye pakatokea uhaba wa mitaji ya fedha katika soko la mikopo, na taasisi za kifedha Marekani, Ulaya na Asia, na sasa kuingia rasmi Afrika.
Chanzo kabisa cha mikasa cha msambaratiko na tatizo la kwanza (ngazi au hatua ya mwanzo), lilitokea katika soko la mikopo ya kujenga, kujengea, kuuza, kununua na kupangisha majumba au nyumba kwa ajili ya makazi, shughuli za maendeleo ya kiuchumi na biashara mbalimbali.
Ni vema kutambua kuwa nchi zilizoendelea wana sera, sheria, taratibu na taasisi ambazo nia yake ni kutoa fursa kwa wananchi wao kupata uwezo wa kifedha kutoka katika taasisi za fedha na benki, kupata mikopo na kuitumia kujenga, kupanga, kutumia na kuendeleza ujenzi wa nyumba na majengo kwa ajili ya matumizi ya malazi au maendeleo ya kibiashara.
Wananchi wengi, bila ya kuchunguzwa kuhusu nia, njia, uwezo na utekelezaji wa sera za ujenzi wa nyumba, walipata fursa hiyo na kuitumia ipasavyo.
Hii ilitoa mwanya kwa watu na sekta binasfi kuwa na uwezo wa kujenga nyumba hizo kwa wingi.
Nyumba za sekta binafsi na nyumba za familia nyingi zilijengwa kwa wingi hivyo kulifanya soko la nyumba kufurika wajenzi na wenye nyumba wengi.
Tatizo na hatua ya pili ilikuwa watu wengi na sekta binafsi walishiriki kujenga nyumba nyingi nzuri na kubwa bila kutambua hali halisi ya mahitaji yao na mahitaji ya soko la nyumba katika sehemu nyingi ndani na nje ya Marekani.
Tatizo la tatu lililojitokeza katika kipindi hicho hakuna aliye na shida au mahitaji ya kupanga au kukodisha nyumba ya mtu mwingine.
Kwa kuwa ujengaji wa nyumba ulikuwa mkubwa kuliko mahitaji ya upangaji, basi bei za ukodishaji au pango la nyumba zilianza kushuka na kufanya thamani ya nyumba hizo kushuka siku hadi siku.
Tatizo la nne na kubwa lilikuwa gharama za mikopo kuongezeka na kusababisha waliokopa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, kuanza kushindwa kulipa riba za benki na kutoweza kurudisha mikopo.
Walioshindwa kulipa riba za benki iliwabidi wakabidhi mali zao, waweke rehani katika benki au taasisi za kati zenye utaalamu wa rehani za mitaji.
Tatizo la tano na kubwa zaidi kuliko la awali ni kuwa nyumba na mali nyingi za thamani kubwa zilizokuwa katika rehani na kuwekwa kwa madalali na kushikwa na mabenki zilikuwa za gharama kubwa kuliko thamani katika soko hivyo benki na madalali wao walishindwa kuzinadi na kuziuza kwa watu na sekta binafsi.
Ilikuwa kazi kubwa kwa benki za mikopo kuanza shughuli za kuweka rehani mali na dhamana na ilikuwa vigumu kwa wao kwa sababu hii ilikuwa ni shughuli kubwa na pevu kwa sekta ya benki za mikopo.
Tatizo la sita ambalo ndio kabambe zaidi likajitokeza kuwa benki za biashara nazo zikawa haziwezi kurudisha riba na mikopo yao.
Kwa sababu za ukata wa kifedha, wakashindwa kulipa riba na mikopo yao kutokana na fedha walizokopa kutoka benki nyingine kuu na taasisi zake za fedha, na hatimaye kutoweza kutimiza masharti ya mikopo na uendeshaji shughuli za benki kibiashara na kushindwa kwa benki kuu kufuatilia, kutathmini na kusimamia soko la fedha na shughuli za mabenki ya nchi hizo.
Kutoka Raia Mwema....Itaendelea.
Dk. Haji Semboja ni mhadhiri kutoka Kitengo cha Utafiti wa Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment