Wednesday, April 08, 2009

Suala la mafuta na gesi





Muhammed Seif Khatib: 

Wanaonichokonoa wana chuki, malengo binafsi

* Asema Urais si hoja kwa sasa

Na Khatib Suleiman, Zanzibar

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatib, amesema baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wanamchokonoa kutokana na chuki na malengo binafsi. Kutokana na hilo, alisema kamwe hataomba radhi kwa wajumbe hao, kwani suala la mafuta na gesi limeingizwa katika mambo ya Muungano kwa kufuata taratibu na kwa ridhaa ya wabunge kutoka Zanzibar. Khatib alisema kama Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wanataka suala hilo liondolewe katika mambo ya Muungano, wanapaswa kufuata taratibu kwa hoja hiyo kupelekwa Baraza la Mawaziri kujadiliwa, kabla ya kufikishwa Bungeni na kuamuliwa kwa kupiga kura.

Aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya CCM, Kisiwandui mjini hapa, kufafanua shutuma dhidi yake zilizotolewa na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

“Niombe radhi kwa lipi? suala la mafuta sikuliingiza mimi... limepata ridhaa ya wabunge kutoka Zanzibar walikuwepo katika kikao...kama Wazanzibari hawalitaki basi wafuate utaratibu kwa mujibu wa Katiba,” alisema Khatib.

Waziri huyo, alisema anashangazwa wajumbe kuacha kuchambua hoja ya mafuta na kuamua kumshambulia yeye binafsi bila ya sababu za msingi. Alipoulizwa kama Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekuwa na wasiwasi na yeye kuhusu mbio za kuwania urais wa Zanzibar kwa kuwa yeye amekuwa akitajwa, alijibu kwa kusema kwamba urais si hoja. Khatib alisema urais una wakati wake na si hoja ya msingi kwa sasa, na kufafanua kwamba hana ugomvi na mtu yeyote.

“Nadhani wanaona mimi ni tishio...labda,” alisema Khatib na kuongeza, kwamba huu si wakati wa kuchafuliana majina.

Alisema yeye ni waziri mwenye dhamana ya mambo ya Muungano, hawezi kukwepa wajibu wake wa kuelezea ukweli wa mambo ulivyo katika masuala ya Muungano.

“Mimi nimeapa kwa ajili ya kulinda na kutetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano...siwezi kukwepa wajibu na ukweli wa mambo ulivyo...suala la mafuta na gesi lipo wazi...kama watu hawalitaki basi wafuate utaratibu...upo unajulikana na ni bunge ndilo lenye uamuzi wa mwisho,” alisema Khatib.

Juzi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walimjia juu Waziri Khatib, wakimshutumu kwamba haweki mbele maslahi ya Wazanzibar. Walitoa shutuma hizo wakati wakijadili hoja ya mafuta na gesi, na kumtaka Waziri Khatib, kuwaomba radhi kwa kile walichodai kuwapotosha wananchi katika suala zima la mafuta ya Zanzibar. Hoja hiyo, iliwasilishwa na Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansoor Yussuf Himid, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi. Mapema akichangia hoja hiyo, Mwakilishi wa jimbo la Chake Chake kwa tiketi ya CUF, Omar Ali Shehe, alimtaka Waziri Khatib kuwaomba radhi Wazanzibari kutokana na kauli zake za dharau kwa wananchi wa visiwa hivyo. Mwakilishi Ali Mohamed Bakari (Tumbe-CUF), alidai kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa ikibanwa katika mambo ya Muungano.

“Tunataka sasa kusimamia mambo yetu kikamilifu ikiwemo nishati na gesi…suala hili liondoshwe mara moja katika mambo ya Muungano,” alisema.

Naye Mwakilishi Said Ali Mbarouk (Gando-CUF), alimlaumu Waziri Khatib kwa kudai kwamba ni yeye aliyeondoa hati za kusafiria kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

“Huyu mtu anautaka urais wa Zanzibar kwa nguvu…lakini hana maslahi kwa wananchi wa Unguja na Pemba,”alidai.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi, alidai matamshi ya Waziri Khatib ni kejeli kwa wananchi wa visiwa vya Pemba na Unguja. Naye Mwakilishi Ali Suleiman Ali (Kwahani-CCM), alidai kwamba nia ya Waziri Khatib ni kuchukua fomu za kuwania urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani. Jumla ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi 20 hadi sasa wamechangia ripoti ya mafuta na gesi, huku wajumbe wengine zaidi 15 wakisubiri kuchangia.

Chanzo: Gazeti la Uhuru

 

2 comments:

Anonymous said...

Hili nalo la mafuta na gesi ya Zanzibar linaonyesha wazi nyufa za Muungano. Nyufa zinaongezeka na sasa zinaonekana wasiwasi na tukifanya mchezo nyumba itaanguka!!!!

Jamani Watanzania tufanye hima na tuzibe hizi nyufa ama sivyo tutajuta huko tunakoenda.

Anonymous said...

Ilikuwa isomeke "wazi wazi"