Sunday, June 14, 2009

Maandamano na ghasia

baada ya uchaguzi nchini Iran



Rais wa Iran, Mahmoud Ahmedinejad  


Rais Mahmoud Ahmedinejad ametetea matokeo ya uchaguzi yaliyomrudisha tena madarakani katika hotuba yake aliyoitoa kwa taifa kupitia televisheni. Amesema uchaguzi ulikuwa huru na uliofanyika kwa njia nzuri. Hata hivyo matokeo hayo ya uchaguzi yamezusha maandamano ya ghasia katika mji mkuu Tehran.Maelfu ya wafuasi wa mpinzani wake mkuu, waziri mkuu wa zamani Mir Hossein Mousavi wamepambana na polisi wa kukabiliana na fujo katika mji huo. Mousavi ameyapinga matokeo ya uchaguzi akisema kumefanyika wizi wa kura.Wizara ya mambo ya ndani imefahamisha kwamba rais Ahmedinejad alishinda asilimia 62 ya kura wakati Mousavi akiwa na asilimia kiasi 33. Inakadiriwa kwamba asilimia 85 ya wapiga kura walijitokeza kushiriki katika uchaguzi. Hapo jana waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton akizungumzia kuhusu Iran amesema ikulu ya Marekani inafuatilia kwa karibu matokeo ya uchaguzi huo.

Umoja wa Ulaya kwa upande wake umesema unawasiwasi kuhusu mvutano katika uchaguzi huo wa rais pamoja na ghasia zilizozuka.Katika taarifa ya Umoja huo kupitia mwenyekiti wake umesema unatarajia serikali mpya itachukua jukumu lake kuelekea jumuiya ya kimataifa na kuheshimu sheria za kimataifa.

No comments: