Friday, July 10, 2009

Mjini Urumqi:

Misikiti mikubwa yafungwa



Msikiti mmoja mjini Urumqi.


Ürümqi (inataamkwa Urumchi), Xinjiang, China


CHINA imeagiza kwamba misikiti yote iliyoko katika mji wa Urumqi isifunguliwe leo kwa ajili ya sala ya Ijumaa.

Agizo hilo limekuja baada ya siku kadhaa za ghasia kati ya kundi la kiislamu la Uighur na watu wa kabila la Han waishio nchini humu ambazo zilisababisha vifo vya watu wapatao 156.

Hadi sasa maelfu ya wanajeshi wameendelea kujizatiti katika mji wa Urumqi ambao ndio mji mkuu wa Jimbo la Xinjiang ili kujaribu kutekeleza agizo hilo.

Serikali ya hapa imekwishatoa agizo la kuwaadhibu wote waliohusika katika ghasia hizo na misikiti mingi ilifungwa tangu yalipolipuka mapigano hayo Jumapili iliyopita.

Ofisa mmoja ambaye hakutaja jina lake ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP, kwamba agizo hilo la kuzuia kufunguliwa misikiti siku ya Ijumaa ambayo ni siku ya kuabudu Waislamu imetolewa kwa sababu za kiusalama.

"Kutokana na kutokuwepo kwa hali ya usalama ya kutosha misikiti yote imewaambia waumini kwamba hakutakuwepo na sala ya Ijumaa na badala yake wakae nyumbani na kusali huku huko," alisema ofisa huyo.

"Serikali inahofia kwamba watu wanaweza kutumia udini kuunga mkono makundi yote matatu," aliongeza.

Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) aliyeko Urumqi amesema kwamba Serikali imeamua kuwa ni bora kuwadhibiti Waislamu katika Jimbo la Xinjiang kwa kupiga marufuku sala ya Ijumaa kuliko kuwaruhusu maelfu ya watu kukusanyika misikitini.

Ghasia hizo ziliibuka Jumapili iliyopita baada ya kundi la watu kabila la Uighurs kuandamana kupinga mauaji ya wenzao waliouawa wiki kadhaa zilizopita katika mapambano kati ya kundi la Uighurs na Han yalitokea kwenye kiwanda kimoja kilichoko katika Jimbo la Guangdog lililoko Kusini mwa nchi.

No comments: