Mokiwa:
Kesi za ufisadi ni usanii
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Mhashamu Dk. Valentino Mokiwa, ameitaka serikali kuziendesha kesi za ufisadi kwa kasi, vinginevyo zitaonekana kama ni usanii kwa wananchi.
Pia ameitaka serikali kuifanyia maboresho ama marekebisho sheria ya makosa ya jinai inayotumika hivi sasa katika kukabiliana na matukio ya ufisadi ili iweze kufanya kazi zake kwa haraka katika kipindi hiki ambapo taifa linakabiliana na vita dhidi ya ufisadi.
Akizungumza hivi karibuni mjini Tabora wakati akitoa mahubiri katika ibada maalumu ya kuweka wakfu Kanisa jipya la Mtakatifu Stephano, Askofu Mokia alisema wananchi wameanza kupoteza imani na serikali juu ya kesi hizo, kwani hatua ya kuwafungulia mashitaka baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi haitoshi bila kuwapo kwa kasi ya uendeshaji wake na hatima yake kujulikana mapema.
Huku akishangiliwa na umati wa waumini wa kanisa hilo mkoani Tabora, akiwamo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, Askofu Mokiwa alisisitiza kuwa ugoigoi katika kuharakisha kesi za watuhumiwa wa makosa ya ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma, unakwaza wananchi japo kuwa serikali inajitetea kwa kusema sheria ni msumeno.
“Ingekuwa vyema kwa serikali kuwa na utaratibu kama unaotumika katika hospitali za umma kama Muhimbili na zile za binafsi wa huduma za haraka, yaani (first track) katika kushughulikia kesi za mafisadi, kwa vile wameangamiza nchi na kusababisha madhara makubwa kwa jamii,” alisema Askofu Mokiwa.
“Kufikishana tu mahakamani si njia ya kuwafanya wananchi kujenga imani na serikali, lakini hatima ya kesi na uchunguzi wake unaweza kurudisha imani za wananchi hao kwa serikali yao na hili tunataka kuiuliza serikali, kulikoni na ufisadi? Mnataka kila Mtanzania ajiuliuze swali hili?” alisema Askofu Mokiwa.
Kuhusu kufutwa kwa misahama ya kodi kwa taasisi za kidini na baadaye kurejeshwa upya, Askofu Mokiwa alisema anasikitishwa na baadhi ya viongozi wa serikali kushangilia hatua ya serikali ya kufuta misamaha ya kodi kwa asasi za kidini kwa vile kuna baadhi ya viongozi wa makundi hayo wamekuwa wakiitumia vibaya misamaha hiyo.
“Ni kweli inawezekana kuwa wapo baadhi yetu na hili nalisema ili kila kiongozi wa kidini, kwa vile sisi si malaika, kujichunguza na kubaini kama anafanya hivyo atubu, kwani hiyo ni dhambi mbele ya Mungu wetu, lakini pia mbona kesi za ufisadi zinaonekana kama ni usanii kwa wananchi?” alihoji Askofu Mokiwa.
“Ninawaomba mtoe kwanza boriti katika macho yenu ndipo mpate vibali vya kuona boriti katika macho ya wenzenu, viongozi wa umma na dini ni kitu kimoja na inawezekana askofu kama mimi na wengine wakaingia katika mkumbo wa ufisadi, ninadhani jinsi ya kushughulikia kesi zao itofautiane na ile ya watu wa chini, kwa nia ya kuonyesha msimamo wa dola,” alisema Askofu Mokiwa kwa kujiamini na kuongeza kuwa ni vyema kesi hizo zikamalizika kabla ya mwaka 2010.
Huku akimkazia macho Spika wa Bunge, Sitta, Askofu Mokiwa alisema wananchi wana imani kubwa na Bunge, lakini pia kuna dalili kwamba chombo hicho cha maamuzi, kinazidiwa nguvu na mamlaka nyingine zilizopo nchini na kuhoji, suala la kashfa ya Richmond linawezaje kumalizwa kwa baadhi ya viongozi kujiuzulu tu.
Waliojiuzulu kutokana na kuguswa kwa kashfa hiyo ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa (Monduli).
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi; na aliyekuwa akishikilia wadhifa huo kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha.
“Ina maana kujiuzulu tu kwa nafasi za viongozi wetu katika sakata zito la Richmond inatosha? Na hii ina maana gani? Je, ni kwa ajili ya kuhakikisha watu wa aina hiyo wanaendelea kupewa heshima ama ndiyo sifa ya kuwapo kwa utawala bora?” alihoji Askofu Mokiwa huku mamia ya waumini na viongozi wa kanisa hilo wakimshangilia.
Ingawa Askofu Mokiwa hakutaja majina ya watu waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ni aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gray Mgonja.
Mwingine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona. Yumo pia Amatus Liyumba, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wafanyabiashara maarufu, ambao wanakabiliwa na kesi hizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Pia askofu huyo alielezea umuhimu wa kulinda amani na utulivu wakati wa uchaguzi mkuu mwakani, kwa kuwataka wananchi kutowachagua viongozi wanaotaka kuingia madarakani hata kama damu itamwagika.
Aliposimama kutoa salamu zake kutokana na mwaliko aliopewa na kanisa hilo, Spika Sitta hakusita kuonyesha jinsi anavyokerwa na suala la ufisadi na kwamba, ndiyo maana yuko mstari wa mbele kukabiliana nalo.
“Ndugu zangu, kwanza nawashukuru kwa kunipa heshima hii kubwa, najisikia mwenye raha ninapokuwa miongoni mwenu, lakini nawaomba niungane na Baba Askofu, kukemea tabia ya ufisadi katika jamii, kwani si nzuri,” alisema Spika Sitta.
Spika aliongeza kwamba ufisadi umechangia kuharibu miundombinu katika jamii, ambapo hali hiyo imesababisha kukosekana kwa maji salama ya kunywa na kuwafanya wananchi wengi kunywa maji machafu, hali inayochangia vifo vya kina mama na watoto wadogo.
“Kwa uhakika ninachukia ufisadi, na hata nikiwa bungeni ninalalamikia suala hili kwa nguvu zangu zote, lakini nimekuwa nikishikilia msimamo wa Kibiblia, ambapo kuna mahala kitabu hiki kitakatifu kinasema kwamba, “Mtetezi wangu yu hai na ananipigania katika mazito yote ninayoyapitia,” alisema.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mama Margaret Sitta, aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alisema serikali iko tayari kushirikiana na taasisi za dini katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Kutoka Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment