Wednesday, July 15, 2009

Ni vigumu kukubaliana

na Rais Kikwete




BAADA ya Rais Jakaya Kikwete kukabidhiwa majina ya watu wanaijihusisha na biashara ya dawa za kulevya mwaka 2006, niliamini kwamba sasa watu hawa wataanza kushughulikiwa vilivyo kutokana na falsafa yake ya Ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya ambayo aliingia nayo madarakani.

Niliami hivyo kwa sababu nilijua kwamba, kwa sababu Rais wetu kapewa majina, hatakuwa na shida tena ya kuwatafuta nani wanaofanya biashara hii haramu bali atakachofanya ni kuyachambua kujua wahusika halisi na kuwachukulia hatua.

Hilo sikuliona linafanyiwa kazi, kama aliifanyia kazi majina hayo ambayo yalikuwa pia ya watu maarufu wakiwamo wanasiasa mashuhuri hapa nchini; basi watu hao hawakuchukuliwa hatua yoyote. Nasema hivyo kwa sababu, watu hao tunawafahamu, lakini mpaka leo hakuna mtu aliyechukuliwa hatua.

Kama hitoshi baadaye Rais Kikwete akabidhiwa orodha ya majina ya vigogo wala rushwa na majambazi sugu yaliyokuwa yakisumbua nchi kwa muda mrefu. Hapa kuna nafuu kidogo kwani tuliona ikifanyika operesheni ya kuwadhibiti majambazi hao; lakini nayo ilikuwa ya nguvu za soda baadaye wakachoka na majambazi yakaanza tena kutikisa nchi na yanaendelea mpaka sasa.

Hatukuona wala rushwa vigogo wakishughulikiwa kama alivyoahidi, tukakata tamaa kwamba serikali hii haiana uwezo wa kupambana na vigogo wa wala rushwa kwa sababu ni sehemu ya serikali na chama tawala chenyewe.

Kilichonisikitisha wiki hii ni kumsikia Rais Kikwete akilalamikia na kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuhakikisha inadhibiti rushwa kuanzia ndani ya vyama mpaka kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Acha ninukuu maneno ya Rais Kikwete:

"Kama mjuavyo, hivi karibuni tutaingia katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kwa kutambua tatizo la rushwa katika siasa, ningependa mjizatiti na kuona kuwa ni kwa namna gani mtasaidia kudhibiti rushwa kuanzia ndani ya vyama mpaka kwenye uchaguzi wenyewe. "Natarajia kuwa mtajipanga vizuri wakati wa mchakato huo na kuidhibiti rushwa vilivyo katika siasa. Tumeona wazi kwamba, tukiiacha rushwa hii iendelee bila kudhibitiwa, tutaruhusu mwanya wa kuwa na viongozi wapenda rushwa na watakaohatarisha maendeleo ya taifa letu".

Akaongeza kuwa watumishi wa Takukuru ambao ni waoga wa kupambana na wala rushwa ni bora wakatafute kazi nyingine kwa sababu serikali hawatawavumilia.

Aliwahakikishia watumishi wa taasisi hiyo kuwa serikali haitawaingilia katika kazi zao na kwamba watakuwa huru kufanya kazi yao kama majukumu yao yanavyowaongoza na kwamba, serikali inatarajia Oktoba kuwasilisha bungeni muswada miwili ya kudhibiti fedha haramu katika uchaguzi na sheria iatakayowaba wafanbiashara kujihusisha na uongozi wa kisiasa.

Kwa hakika, maneno ya Rais Kikwete ni matamu mno kuyasikia, lakini sio rahisi pia kuaamini anachokisema kama kinaweza kutendeka.

Kwa bahati mbaya sana rais wetu amekuwa bingwa wa kutoa ahadi ambazo kwa hakika nyingi hazijatekelezwa mpaka sasa tangu aingie madarakani, ndio maana nachelea kuamini hata kwa hili analoliahidi la kuifanya Takukuru sasa kufanya kazi zake barabara.

Najua Takukuru ingawa wanaweza kuwa hawana uwezo mkubwa wa kupambana rushwa kubwa, lakini kwa kiasi kikubwa wameshindwa kutumia uwezo wao waliona nao kuwadhibiti mafisadi anaotaka Kikwete wachukuliwe hatua kwa sababu ni marafiki wakubwa wa mawaziri ni viongozi wa juu wa CCM.

Kikwete asijaribu kutuhadaa Watanzania kwamba, Takukuru iachiwe ifanye kazi zake kwa uhuru wakati ni yeye huyo huyo ambaye amekwamisha kuifnya ifanye kazi zake sawasawa kwa mfano kitendo chake cha kuwapa nafasi watuhumiwa wa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya nje katika Benki Kuu ya Tanzania (EPA) kurejesha fedha hizo kimya kimya bila ya kuchukuliwa hatua kama vile walikuwa wakitoa mahari kwa mwali ambaye wametuolea, ni sawa na kuzuia jitihada za kupambana na ufisadi.

Je, ina maana mkono wa sheria kwa watuhumiwa hao waliorejesha fedha ambazo waliiba benki kuu tena kwa kughushi nyaraka haufiki kwa sababu walifanya jambo jema hilo?

Leo hii asimilia kubwa ya watuhumiwa wa ufisadi nchini ni wanachama wa CCM tena wengi wakiwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati kuu, vikao ambavyo ndivyo vikubwa kabisa vinavyotoa maamuzi mazito ya nchi.

Katika hali hiyo ni afisa gani wa Takukuru anaweza kuwakamata watu hawa? Kwani hajipendi, awakamate aone cha moto kitakachomtokea. Ni mara ngani tumeshuhudia baadhi ya viongozi wa CCM au wajumbe wa NEC wanakamatwa makosa mbalimbali zikiwemo nyara za taifa lakini kesi zao zinayeyuka kama barafu.

Hilo ni kwa sababu CCM haiwezi kuwatosa viongozi wake waandamizi waingie katika kashfa za rushwa kwa vile kufanya hivyo kutakifanya chama kionekane hakifai na kinazungukwa na mafisadi.

Kama nilivyosema awali kwamba, kama Kikwete kweli anataka kumaliza ufisadi nchini, lazima aanze kuisafisha CCM, vinginevyo anachokifanya ni sawa na baba katika familia kuamua kuanzisha vita vya kuchoma moto vibaka mtaani wakati hata yeye mwenyewe nyumbani ana vibaka wengi zaidi kuliko walioko mitaaani.

Hatari nyingine ambayo ninaiona hapa ni kwamba, kwa vile Takukuru haiwezi kuwa na ubavu wa kuwadhibiti vigogo waliopo ndani ya CCM; kuna hatari taasisi hiyo ikatumika kisiasa.

Kauli ya rais kuhusu Takukuru ni amri, na amri ya Rais lazima itekelezwe na kwa sababu maafisa wa taasisi hiyo wanataka kulinda vibarua vyao kwa kufanya kazi kwa bidii, basi ipo hatari taasisi hiyo katumiwa na baadhi ya wanasiasa hao mafisadi kama silaha ya kuwapigia maadui zao kisiasa.

Ni wazi kwamba, kwa sababu Takukuru hataweza kumtia mbaroni fisadi ambaye ni mjumbe wa kamati kuu au mjumbe wa NEC atakachokifanya fisadi huyo ni sasa kuwatumia wao kama silaha yake ya kuwaagamiza maadui zake kisiasa.

Mpaka sasa tunashuhudia baadhi ya viongozi wa CCM wakiwamo baadhi ya wabunge wanaopambana na ufisadi bungeni wakilia kwamba, mafisadi wana mpango wa kutaka kuwang'oa majimboni kwao kwa kupandikiza watu wengine ambao watatumia fedha nyingi mno.

Mwandishi wa safu hii anapatikana kupitia baruapepe:

juliusmagodi@yahoo.com
Simu +255 754 304336

Gazeti la Mwananchi.



No comments: