Saturday, July 11, 2009

Norway:

tutahamisha na kupeleka

wakimbizi wote Tanzania.

Nembo ya Fremskrittspartiet (FrP)


Chama cha wahafidhina wenye siasa kali nchini Norway, Fremskrittspartiet (The Progress Party) kimepanga mikakati ya kuwaondoa waomba hifadhi za kisiasa na wakimbizi toka Norway na kuwahamishia nchini moja ya Afrika, kusini ya jangwa la Sahara, Tanzania au Uganda. Tanzania panafaa kwa sababu inapokea hela nyingi za misaada kila mwaka toka Norway. Hayo yamesemwa na msemaji wa Fremskrittspartieiet, wa masuala ya wakimbizi/wageni Bw. Per-Willy Amundsen.

Msemaji huyo amenukuliwa na gazeti la kila siku la hapa Norway, VG (Verdens Gang). Fremskrittspartiet wanasema kuwa Norway ijenge kambi za wanaotaka kuomba hifadhi za ukimbizi na kisiasa Tanzania. Kwa kufanya hivyo watu wengi wakisikia kuwa kwanza utakaa kwenye kambi za wakimbizi nchini Tanzania kusubiri ukubaliwe kuingia Norway, watafadhaika na kuogopa, na itapunguza wanaokuja Norway kwa sababu za kudanganya danganya.

Fremskrittspartiet wanaamini kuwa wengi wa wanokuja Norway kuomba ukimbizi, si wa kweli. Wengi wao wanakuja kuomba ukimbizi kwa sababu za ukali wa maisha wanakotoka. Pia wanadai kuwa kuna wageni wapatao kati ya 20 000 na 30 000 wanaishi bila ya makaratasi hapa Norway.

Mwaka jana Norway ilipokea watu 14 000 waliokuja na kudai hifadhi za kikimbizi, na kwa mahesabu ya Fremskrittspartiet, hadi mwaka huu kwisha kutakuja watu zaidi ya 18 000 watakaoomba hifadhi za ukimbizi.

Fremskrittspartiet wanataka watakaokubaliwa kuingia Norway wawe ni wakimbizi wa kweli na si wa kujipa.

Jumatatu Septemba 14 ni uchaguzi mkuu hapa Norway. Kutokana na kura za maoni za hivi karibuni, Fremskrittspartiet (FrP) wanaweza kupata wingi wa kura na kwa kushirikiana na chama kingine kikongwe cha wahafidhina wenye siasa zisizo kali, Høyre (The Conservative Party of Norway), wanaweza kuunda serikali ya mseto na kuangusha serikali iliyopo sasa madarakani ya mseto wa Labour Party (Arbeiderpartiet), Socialist Left (SV) na Aggrarian Party (Senterpartiet) inayoogozwa na Jens Stoltenberg wa Labour Party.

Kama FrP watafanikiwa kuunda serikali, uwezekano mkubwa kuwa kiongozi wao, Bi. Siv Jensen ataibuka na kuwa waziri mkuu. Na kama Frp wakichukua usukani wa kuongoza Norway, basi kuna wasiwasi kuwa watatekeleza ilani zao zote za uchaguzi, ikiwemo hii ya kuwahamisha waomba ukimbizi kuwapeleka nchi itakayokubali matakwa yao ya kujenda kambi ya wakimbizi wa kutaka kuingia Norway.


1 comment:

Anonymous said...

Haya jamaa wakati mwingine wanasema vitu bila kufikiria. Wanasema kwanza na halafu wanafikiria baadaye!

WAnasema hivi kwa vile kampeni za uchaguzi zimeanza na wanajua masuala ya kuingia kwa wageni hapa Norway kiholela ni neyti na yanawagusa Wanorweji wengi.

Wanategemea kuwa wakianza na masuala ya wageni, basi watazinyakua kura za wapiga kura wengi.

Yetu macho.