Monday, July 06, 2009

Watanzania na aibu

ya kukibeza






Imeandikwa na Olga Ivanovna Givishivili,

Moscow.


WAVULANA wa Tanzania, aibu aibu! Mbona aibu? Ninaeleza. Siku chache zilizopita, nilisikia katika metro (treni ipitayo chini ya ardhi) mazungumzo ya Waafrika wawili na raia mmoja wa Amerika. Ninafikiri kwamba Waafrika walikuwa Watanzania kwa sababu walisema “in our Tanzania” (walikuwa wakisema kwa Kiingereza).

Walionekana kutofurahia Kiswahili, walisema kwamba Kiingereza ni lugha ya maana kubwa, na inabidi kufukuza Kiswahili kutoka katika idara, ofisi na vyuo vikuu na kuingiza Kiingereza. Mimi sikuweza kujiingiza katika mazungumzo yao kwa sababu nilikuwa ninafuata Wataliano wawili kama mfadhili wao ili kwenda katika hospitali moja ili kuzungumza ugonjwa wa kansa.

Lakini ningezungumza na wale Watanzania ningesema yafuatayo; Mimi ni mfasiri, ninazungumza bila taabu Kifaransa, Kihispania na Kiitaliano. Ninafasiri mazungumzo juu ya mambo ya biashara, uchumi, utabibu, ufundi. Kwa mfano, viwandani ambapo vyombo vipya vinapandwa, nina elimu mbili za juu ya fizikia na linguistiki.

Ninafasiri lugha na vyeti vya Kiingereza, Kireno, Kirumeno, Kipolako, Kicheko, Kbugalo na Kiserobobroato. (Kwa ufupi ni daktari kwenye general and historic, and, comparative linguistic). Nilijifunza Kiswahili mwaka 2006. Niliipenda lugha hiyo mara moja wakati nikiwa nasafiri katika metro Novokuznetskaya, niliona watoto wachache Waafrika wazuri sana ambao walikuwa wanazungumza lugha yao.

Walikuwa wanazungumza na mke muuzaji katika kiduka cha ice cream ambaye baadaye nilipokwenda kumuulizia, alisema walikuwa Watanzania. Nilipendezwa na watoto wale, haiwezekani zaidi ya kukimbia katika maktaba ya vitabu vya kigeni ili kuchukua kitabu cha masomo ya Kiswahili. Ndipo nilianza kujifunza lugha hiyo nzuri na hadi sasa naweza kuandika hivi nilivyoandika barua hii.

Mimi ninashughulika sana na kazi yangu ya kufasiri, lakini ikiwa ninapata muda kwa mfano, dakika 10 ninazidi kusoma kitabu cha masomo ya Kiswahili kiandikwacho na Profesa Bibi Siodorowa wa hapa Moscow. Na nina hakika ya kusema yafuatayo: Katika Urusi, Kiingereza kinatumiwa mara kwa mara, lakini hapana Mrusi ambaye anasema kwamba inabidi kuifukuza lugha ya Kirusi katika idara, ofisi na vyuo vikuu na kuingiza Kiingereza.

Lakini nasikitika kwamba vijana wa Tanzania sasa wanaonekana kuichukia lugha yao, wanatamani ifukuzwe iondolewe kama lugha rasmi ofisini. Kwa kweli hii ni aibu kubwa. Katika Tanzania, pia Kiswahili inabidi kushinda lugha ya Kiingereza, Kiswahili kinakwenda kuitwa lugha mojawapo muhimu katika lugha saba au tisa za dunia.

Ni Watanzania wenyewe ndio wenye jukumu la kukuza lugha yao na sio mtu mwingine. Kama watu wa nje tunatamani kujifunza Kiswahili, iweje Watanzania wakibeze?

* Mwandishi ni raia wa Urusi na anaishi mjini Moscow. Ameandika waraka huu kwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Jaka Mwambi.

Anapatikana kwa baruapepe: givishivili@mtu-net.ru

No comments: