Salma Rashid Kikwete
MKE wa Rais Jakaya Kikwete, Salma, ana majukumu mengi ya kijamii, kitaifa na kimataifa hivyo si rahisi kupata wasaa wa kuzungumza naye lakini pamoja na ratiba finyu ya mama huyo, Mwandishi Wetu TUMA ABDALLAH alipata nafasi ya kumhoji hivi karibuni na kuzungumzia changamoto zinazomkabili akiwa mke wa rais, mama na mwanamke kama ifuatavyo:
Swali: Ni ipi historia fupi ya maisha yako?
Jibu: Mimi naitwa Salma Rashid. Nilizaliwa katika wilaya ya Lindi Mjini, Novemba 30, 1963. Baba yangu anaitwa Rashid Yussuf Mkwachu na mama yangu ni Mwanapaza binti Shariff. Kwa asili, baba yangu anatoka Sarai, Rufiji mkoani Pwani na mama yangu anatoka Ng’apa, Lindi. Katika familia yetu, upande wa mama, tulizaliwa watoto saba, wasichana watatu na wavulana wanne. Mimi ni wa sita, ila kwa baba ni wa pili, nina kaka yangu na mdogo wangu. Nina wadogo zangu wengine watatu ambao tunachangia baba, kati yao wavulana ni wawili na msichana mmoja.
Baba yangu alikuwa mfanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977 na kituo chake cha kazi kilikuwa Mtwara, wakati baba anafanya kazi, mama alibaki Lindi, hali ambayo ilinifanya nipate elimu yangu ya msingi kuanzia mwaka 1973 katika shule nne tofauti; Nnaida ya Mikindani, Mtwara, Rahaleo ya Lindi, Ligula (Mtwara) na Stadium, Lindi ambapo nilimalizia elimu yangu ya msingi.
Ingawa wakati ule nafasi za kujiunga na sekondari zilikuwa chache, namshukuru Mwenyezi Mungu nilikuwa miongoni mwa waliochaguliwa. Nilichaguliwa kujiunga na sekondari ya Lindi ambako nilisoma hadi kidato cha nne na kumaliza mwaka 1984. Baada ya hapo, nilichaguliwa kusomea ualimu katika Chuo cha Ualimu Nachingwea kwa miaka miwili, kuanzia mwaka 1985 hadi 1986.
Nilipomaliza nilijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria kwa mafunzo ya kijeshi ya mwaka mmoja na baadaye nikapangiwa kazi Lindi na kufundisha katika shule ya msingi ya Chikonji mwaka 1988.
Swali: Katika nafasi yako hii ya mke wa Rais, nini majukumu yako ya kila siku?
Jibu: Majukumu yangu ya kila siku kama mama, mwanamke na mke wa Rais yapo mengi. Kama mke nina majukumu ya kifamilia yakiwamo yale ya kumsaidia mume wangu ili aweze kutekeleza vyema majukumu mazito aliyonayo ya kuliongoza Taifa letu na watu wake. Jukumu mojawapo ni kuhakikisha namsaidia katika hali zote.
Ingawa tunazungumzia masuala ya haki sawa, lakini kuna mambo ambayo mwanamke lazima umsaidie mumeo, na ili shughuli zake ziende vizuri ni lazima apate mapokezi mazuri nyumbani. Ingawa nyumbani tuna watu ambao wakati wote wanatusaidia, lakini mimi kama mke au mama, lazima nisijisahau jukumu langu la kumhudumia mume wangu kupata kile ambacho kitamridhisha.
Kwa upande wa chakula kwa mfano, mimi mkewe najua nini mume wangu anapenda zaidi au hapendi, ni wakati gani yuko kwenye hali nzuri na wakati gani hapana. Kwa hiyo kila siku najitahidi kwa kadri ninavyoweza, kuhakikisha kwamba mazingira ya nyumbani yanakuwa mazuri ili aweze pia kufanya kazi zake vizuri. Katika hili wala sioni tabu, baadhi ya wakati naingia jikoni kupika.
Yeye akiwa Rais, ana watu wa kumsaidia, lakini hilo halimpotezei haki ya kupata huduma yangu kama mkewe. Hata hivyo, wakati mwingine hii inakuwa ngumu kwa sababu wasaidizi wetu hawapendi, kutokana na maadili ya kazi zao.
Kuwa mke wa Rais kuna majukumu makubwa na mazito sana, kwa sababu kuna kazi nyingi ambazo inabidi uzifanye au uzishughulikie ambazo zimegawanyika katika maeneo mbalimbali. Kuna kazi ambazo nafanya kama mke wa Rais lakini pia kuna zile ambazo napaswa kuzifanya kama Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA).
Swali: Eleza kwa ufupi shughuli za taasisi ya WAMA.
Jibu: Hapa WAMA tuna mipango mikakati ambayo tumejipangia. Tuna mambo makubwa manne, tunashughulikia elimu, lakini hasa elimu ya mtoto wa kike na pia masuala ya afya na tumejikita katika masuala ya Ukimwi na afya ya uzazi, hasa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto na magonjwa mengine. Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni eneo jingine tunalolishughulikia na eneo la mwisho ni watoto yatima.
Shughuli hizi zinafanyika kwa kufuata mfumo maalumu ambao tumeutengeneza unaowezesha shughuli kuendelea hata kama mimi sipo. Kuna watendaji kadhaa, ambao kwa pamoja tumegawana majukumu. Nashukuru kazi zinakwenda vizuri kwa mujibu wa malengo tuliyojiwekea.
Swali: Wakati unaanzisha taasisi ya WAMA ulikuwa na malengo gani na mpaka sasa umefikia wapi katika kuyatekeleza?
Jibu: Lengo langu lilikuwa ni kujaribu kuondoa kero katika maeneo hayo manne niliyoyataja hivi punde. Ingawa WAMA bado ni changa, ilizinduliwa mwishoni mwa mwaka 2006 kwa hiyo haina hata miaka mitatu, tayari tumepata mafanikio ya kuridhisha katika maeneo yote hayo kutokana na mambo ambayo tumeyafanya.
Na hii yote ni kutokana na mikakati tuliyoipanga ambayo imetuwezesha kufanya mambo mbalimbali. Kwenye eneo la elimu, tumepeleka watoto sekondari kwa sababu lengo letu kubwa lilikuwa ni elimu ya mtoto wa kike… kuwasaidia watoto hawa hasa wale waliotoka katika mazingira magumu na hatarishi, kupata elimu ya sekondari na hapa si kwamba tunapeleka kila mtoto, ila tunaangalia wale waliofanya vizuri mtihani wa Taifa wa darasa la saba na wakachaguliwa ila wakashindwa kupata hizo fursa kutokana na mazingira wanamotoka.
Tunashirikiana na Wizara ya Elimu ambao wanatusaidia kuwatambua wanafunzi wanaostahili kusaidiwa. Mpaka sasa tumesaidia watoto zaidi ya 400 ambao ni pamoja na wanafunzi watano kutoka kila mkoa Bara na Visiwani.
Ila kuna wengine ambao wanaletwa hapa hapa kwenye ofisi zetu na tukiona kwamba malengo yao ni ya msingi tunawachukua, wengine tunawapata kutoka kwa wadau wa maendeleo.
Vile vile kuna maeneo mengine ambayo tumeweza kuwaingiza wengi zaidi kwa sababu kuna msaada wa pekee unaohitajika hata USAID (Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani) kwa mfano wakaona wasaidie. Lindi, kwa mfano, wamewajengea bweni ambalo linachukua wanafunzi karibu 200 ambao zamani walikuwa wanakaa nyumbani.
Baada ya kuona watoto ni wengi na wako katika maeneo tofauti, tuliamua kujenga shule ambayo ujenzi wake uko katika hatua nzuri. Kwa upande wa afya, tupo katika hatua nzuri pia. Tunajenga kituo cha afya Mkuranga, ujenzi upo katika hatua nzuri.
Hata hivyo kitu kikubwa tunachokishughulikia katika eneo hili, ni kupunguza vifo vya uzazi. Tumetoa elimu kwa njia ya semina na pia tunaboresha mazingira ya kujifungulia kwa kutoa vifaa mbalimbali vikiwamo vitanda vya kujifungulia, vya kawaida, vifaa vya kujifungulia, mashuka na vinginevyo ambavyo vitamwezesha mama ajifungue katika mazingira bora zaidi.
Hili tumelifanya katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya Lindi, Mtwara, Iringa na hivi karibuni tutakuwa na programu ya kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria. Katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, tumefanya mambo kadhaa pia.
Kwa mfano, katika eneo la Hoyoyo tumeanzisha kilimo cha paprika ambako tumelima mara mbili. Kitu kikubwa tunachozingatia katika kila eneo, ni kutoa elimu kwa maana kwamba mtu ukimpa elimu umempa hazina ya kudumu kuliko fedha.
Kwa hiyo tulihakikisha tunawaelimisha watu jinsi ya kulima paprika ili wakitoka pale, waweze kufanya wenyewe. Tulishavuna paprika na tukaiuza Iringa na bahati nzuri tulipata cheti cha kuzalisha paprika bora Tanzania nzima.
Pia tunaendeleza ufugaji na hasa wa kuku wa kienyeji na hii ni kwa sababu Watanzania karibu asilimia 80 wanaishi vijijini na wengi wanafuga kuku wa kienyeji ingawa si kitaalamu.
Kwa hiyo ukimfundisha mwananchi huyu kufuga kwa njia bora, utamwezesha kupata tija na hivyo kuongeza kipato ambacho kitamwezesha kuboresha hali yake ya maisha, ikiwa ni pamoja na kugharimia elimu ya watoto wake na kufanya mambo mbali mbali ya kijamii. Kuhusu watoto yatima, shughuli zetu zinahusisha zaidi utoaji wa misaada ya kibinadamu kama sare za shule. Ila kwa upande mwingine, ni hawa hawa ndio kwa kiasi kikubwa tunaowachukua kwenda sekondari.
Swali: Ni changamoto zipi zinakukabili katika kutekeleza majukumu yako?
Jibu: Kwa kweli changamoto zinazonikabili ni nyingi. Katika taasisi ya WAMA kwa mfano, kazi ni kubwa sana, watu wana matarajio makubwa sana kutokana na jinsi tunavyoendesha shughuli zetu.
Mara zote mwanadamu anakwenda sehemu ambayo ana matumaini ya kusaidiwa, kwa hiyo siku hadi siku watu wengi zaidi wanakimbilia katika taasisi yetu kuomba msaada.
Changamoto yetu kubwa sana hapa ni rasilimali, uwezo tulionao ni mdogo ukilinganisha na majukumu yetu. Tunachoomba ni wadau wa maendeleo watusaidie kwa kiasi kikubwa zaidi, ili tuweze kufikia matarajio ya wananchi kwa jumla. Kama mama na mke wa rais, pia nakabiliwa na changamoto nyingi.
Watoto wengine bado ni wadogo, wanahitaji kwenda shule na wanataka wawe na mama yao karibu, lakini sasa mama huyu anashughulikia masuala ya kijamii na pia anamsaidia baba, ili shughuli zake ziende vizuri, najitahidi muda nilionao kuwafanya waone kila kitu kiko sawa na hawana wanachokikosa.
Swali: Majukumu uliyonayo ni mengi na yamegawanyika katika sehemu kadhaa. Unaugawaje muda wako ili kila upande upate huduma yako stahili?
Jibu: Kitu kikubwa ninachokifanya ni kujaribu kugawa muda wangu vizuri, ni kujipanga na kuona kazi gani zifanyike saa ngapi. Taratibu za maisha yangu ya kila siku zimebadilika kwa kiasi kikubwa tu.
Zamani katika mazingira ya ualimu, unaandaa somo lako, unaingia darasani unafundisha na kadhalika. Lakini sasa hivi mambo ni mengi, kuna mialiko mbalimbali ambayo ni lazima uende na ufanye kazi husika ambayo ni sehemu ya majukumu yangu ya kijamii na Taifa kwa jumla.
Jamii inapokuhitaji huwezi kukataa, ni lazima uende na ufanye walichokuitia. Wakati mwingine kuna mikutano ambayo inabidi niambatane na Mheshimiwa Rais na wakati mwingine inabidi nibaki ili niweze kufanya shughuli za taasisi yangu ya WAMA.
Swali: Una mipango gani ya baadaye?
Jibu: Kwa jumla mipango yetu katika taasisi ya WAMA ni mikubwa sana. Sasa ndio tumeanza, tuna shule moja tu, lakini tunatarajia kuongeza shule nyingi zaidi katika maeneo tuliyoyakusudia kwa sababu watoto wanaohitaji msaada wako wengi sana.
WAMA tunachangia kidogo katika juhudi za serikali za kuboresha maeneo hayo, kwa hiyo lengo letu ni kuzidi kuboresha na kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata elimu. Hali kadhalika katika maeneo yale mengine tunafanya hivyo hivyo, tunataka kuwasaidia kina mama wengi zaidi katika maeneo ya kupambana na Ukimwi na hususan kupunguza kasi ya maambukizi katika kuboresha afya zao za uzazi na pia katika kuwawezesha kiuchumi.
Watoto yatima vilevile tuwasaidie zaidi, kwa upande wa mapambano dhidi ya Ukimwi, kitu kikubwa tunachotakiwa kufanya ni kuimarisha utoaji wa elimu ili watu wawe na uelewa mkubwa zaidi. Naamini sauti ya kiongozi ina nguvu zaidi.
Kwa hili napenda kusisitiza kwamba tuna changamoto kubwa ya kupambana na Ukimwi. Nawaomba Watanzania tuhakikishe tunapambana kwa nguvu zetu zote ili ugonjwa huu uwe ni historia kwa Taifa letu. Inawezekana kabisa kuutokomeza Ukimwi wala si suala linalohitaji rasilimali kubwa, zaidi ni kubadili tabia na pia kuhakikisha hizo rasilimali zinazopatikana zinaelekezwa katika maeneo husika.
Pia napenda kuwaomba Watanzania tuweke juhudi kubwa sana katika kuwaendeleza kimasomo watoto wetu wa kike, kwani wanasema ukimwelimisha mwanamke umeelimisha jamii nzima na katika suala hili kuna changamoto nyingi sana, ikiwamo ile ya mimba za watoto wa shule.
Kuna maeneo tatizo hili ni kubwa sana na sababu wanazotoa ni umasikini… sikatai umasikini upo, lakini hata wale wanaopata mimba si kwamba wanapokwenda kwa hao wavulana kuna kitu wanachokipata, kikubwa ni kuchezewa na baada ya muda wanajikuta wako katika mazingira hayo yanayowalazimisha kukatisha masomo.
Siku zote ninapozungumza na wasichana, huwa nawaambia si kweli kwamba mvulana anayekutana naye kwa mara ya kwanza ndiye mara zote anakuwa mwenzi wake wa maisha, hakuna hicho kitu. Ni lazima kujitunza na unapojitunza, mume wako mkubwa ni elimu yako. Hili wasichana ni lazima walizingatie, akina mama waelekeze malezi makubwa kwa watoto kwani watoto ndio ustawi wa Taifa letu.
Swali: Ni kitu gani kinakutia nguvu ya kuanza siku mpya kwa ari na bidii zaidi?
Jibu: Kila mwanadamu kuna kitu ambacho kinamsukuma kufanya jambo fulani. Kwa upande wangu kitu kinachonisukuma na kinachonitia moyo ni kuona jinsi watu wanavyotambua hizi juhudi zetu tulizozianzisha.
Kwa hiyo kama watu wanatambua na kuthamini mchango wetu, jukumu letu ni kuhakikisha tunawasaidia kulingana na matarajio yao na hiyo ni changamoto kubwa kwetu WAMA…tunahitajika kuongeza bidii na kutafuta rasilimali zaidi ili kukidhi mahitaji ya watu wengi zaidi.
Naamini penye nia pana njia…tukidhamiria tunaweza. Tulidhamiria kujenga shule na sasa tunajenga. Tumeanza na moja, tutajenga ya pili, ya tatu na mpaka tutafikia malengo tuliyojiwekea.
Swali: Wewe unatoka Lindi na Mheshimiwa Rais anatoka Pwani, mlikutana wapi na mlifunga ndoa lini?
Jibu: Kila jambo hupangwa na Mwenyezi Mungu. Nilikutana na mume wangu mwaka 1985 nikiwa katika Chuo cha Ualimu Nachingwea, yeye akiwa ni Katibu wa CCM wa Wilaya ya Nachingwea.
Tulipokutana kwa mara ya kwanza kitu ambacho aliniambia ni kwamba “nakupenda na nataka nikuoe”…kusema kweli hakusema anataka awe rafiki yangu au vipi, sijui kama huo ndio utaratibu wa kina baba wote, lakini nasema kutoka moyoni, hicho ndicho alichoniambia na mimi kwa sababu nilimpenda, nilimkubalia, ingawa uamuzi wangu sikuutoa papo hapo.
Tulifunga ndoa Machi 30, 1989 wakati huo yeye akiwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini.
Swali: Baada ya kufunga ndoa ikawaje?
Jibu: Baada ya kufunga ndoa nilifanya taratibu za uhamisho kwa mujibu wa taratibu za kikazi. Kwa hiyo nilihamia Dar es Salaam ambapo niliungana na mume wangu na tukawa tunakaa Mikocheni mtaa wa Ursino.
Swali: Hapa Dar es Salaam ulifanya kazi wapi?
Jibu: Dar es Salaam niliendelea na kazi yangu ya kufundisha na shule yangu ya kwanza ilikuwa ni Mbuyuni, Kinondoni ambako nilifanya kazi kwa takriban miaka 14 kabla ya kuhamishiwa shule ya msingi Kawe A ambako ndiko nilikoondokea kuja hapa Ikulu baada ya mume wangu kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Swali: Katika miaka yenu hii 20 ya ndoa mmejaaliwa kupata watoto wangapi na wako wapi?
Jibu: Tunamshukuru Mwenyezi Mungu tumejaaliwa watoto watano kati yao wanne ni wa kiume na mmoja wa kike. Wote wanasoma, wa kwanza yuko kidato cha sita, wa pili cha nne, wa tatu cha pili, wa nne yuko darasa la tano na wa mwisho yuko darasa la tatu.
Lakini kwa ujumla tuna watoto wanane, ikiwa ni pamoja na watatu ambao mume wangu alipata na mke wake wa kwanza. Hawa wakubwa mmoja ni mwanasheria, mwingine ni daktari na mwingine ni mtaalamu wa Teknohama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano).
Ila siku zote napenda kusema tuna watoto wanane kwa sababu hata hawa wakubwa nimewalea mimi tangu wakiwa na umri mdogo sana. Kwa hiyo hawa ni watoto wangu sawa sawa na hawa niliowazaa mimi.
Swali: Ni kitu gani kimekutokea maishani ambacho huwezi kukisahau?
Jibu: Kuna mambo mengi kama binadamu yamenitokea maishani ambayo siwezi kuyasahau mojawapo ni kuwa mke wa rais. Hii ni kwa sababu hiki ni kitu kikubwa na chenye mamlaka makubwa na majukumu mazito sana.
Ni kitu ambacho sikuwa nimekifikiria… sikuwahi kuwaza au kufikiria kwamba siku moja ningekuwa mke wa rais, lakini kila kitu hupangwa na Mwenyezi Mungu. Ninaamini ni mipango ya Mwenyezi Mungu kwa mimi Salma kuwa mke wa rais.
Swali: Unapendelea nini kupitishia muda?
Jibu: Tangu nikiwa mdogo, nimekuwa napenda kufurahi na watu na kucheza michezo ya aina mbalimbali. Nikiwa shuleni, nilikuwa nacheza mpira wa kikapu, netiboli, nilikuwa nashiriki riadha hasa kukimbia na kuruka chini. Hata nilipokuwa kazini, niliendelea kushiriki michezo hii na mpaka sasa baadhi ya nyakati huwa napenda kucheza nikiwa na watoto wangu, nakimbiakimbia, nacheza mpira wa kikapu.
Swali: Ni mtindo gani wa mavazi unaupendelea zaidi?
Jibu: Mimi napenda sana vitenge, kwa sababu naamini ni vazi la akina mama na ni vazi la heshima la Kiafrika.
Swali: Kuna kitu chochote ungependa kuongezea?
Jibu: Napenda nimshukuru mume wangu, kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika kuendeleza Taifa letu. Tanzania mbali ya kuwa na rasilimali nyingi bado ni nchi masikini na yeye anajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kukabiliana na changamoto mbalimbali katika juhudi za kuondoa umasikini na kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.
Namshukuru kwa msaada mkubwa wa hali na mali anaonipa nikiwa mkewe. Namshukuru sana kwa hili kwa sababu kama mume mwenye majukumu mengi ya kitaifa angeweza kukataa ila yeye hayuko hivyo, wakati wote ninapoomba msaada yuko mstari wa mbele kunisaidia kwa jambo lolote ninalohitaji. Kwa ujumla mume wangu ni mtu mwenye upendo sana kwangu, kwa watoto na watu wengine wanaomzunguka. …Ahsante sana Mama Salma.
Kutoka Habari Leo.
No comments:
Post a Comment