Thursday, November 19, 2009

wataka mjadala wa Muungano


BARAZA la Taifa la Kutathmini Utawala Bora nchini, limesema wananchi wengi wanataka kuitishwe kongamano la kitaifa la kujadili muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Rehema Twalib wakati akiwasilisha ripoti ya ndani ya tathmini ya utawala bora katika mkutano wa kujadili ripoti hiyo kwa watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, jana.

Wataalamu hao walisema baada ya utafiti kufanyika, wananchi wengi wamelalamika kuwa muundo wa Muungano una kasoro na kushauri kuitishwe kongamano la kitaifa la kujadili njia bora za kuuimarisha.

Aidha, alisema wananchi wengi wanataka kuwepo kwa mahakama ya katiba itakayosimamia masuala mbalimbali ya kisheria ya Muungano pamoja na orodha ya mambo ya Muungano kupitiwa upya kwa kuangalia maslahi ya pande mbili za muungano huo.

“Kuna malalamiko katika suala la muundo wa Muungano, na njia ya kuondosha mapungufu wananchi wanapendekeza liitishwe kongamano la kitaifa la kujadili muundo wa Muungano,” alisema.

Hata hivyo, alisema katika utafiti wao suala la kuandikwa kwa katiba mpya ya Zanzibar na ya Muungano limepewa nafasi kubwa na wananchi kwa vile katiba za sasa zimetokana na msingi wa chama kimoja cha siasa.

Vile vile ripoti hiyo imesema kuwa, ZEC na NEC ni tume za uchaguzi ambazo zinaonekana haziko huru katika utekelezaji wa majukumu yao.

Katibu Mtendaji huyo, alisema mtazamo huo unatokana na mfumo wa uteuzi wa wajumbe wa tume kuteuliwa na rais wakati yeye ni miongoni mwa wagombea wa urais katika uchaguzi.

Alisema mbali na hilo, pia suala la mgombea binafsi lilijitokeza wakati wa utafiti na wananchi wametaka liharakishwe kwa vile kuendelea kuchelewa linawanyima haki yao ya kikatiba.

Kufuatia madai hayo, Ofisa Habari wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Idrisa Jecha, alisema hakuna matatizo yoyote kwa rais kuteua wajumbe wa Tume ya Uchaguzi kwa vile wanafanya kazi kwa kuongozwa na sheria ya tume hiyo.

Alisema kabla ya rais kuwateua wajumbe wa tume hiyo, kuna utaratibu mrefu, ikiwemo vyama vya siasa kupendekeza majina na baada ya uteuzi kufanyika ujumbe wote hufanya kazi kama timu na kufuata sheria ya uchaguzi.

Hata hivyo, Kamishna wa ZEC, Ayoub Bakari Hamad, alisema wakati umefika kwa Tume ya Uchaguzi kuweka kiwango maalumu cha fedha kinachostahili kutumiwa na chama cha siasa wakati wa kampeni ili kudhibiti rushwa na fedha haramu katika uchaguzi.

Mkutano huo umeandaliwa na Baraza la Taifa la Kutathmini Utawala Bora na kuwashirikisha watendaji wakuu wa Tume ya Uchaguzi kuanzia ngazi za wilaya hadi taifa, kujadili ripoti ya mafanikio na matatizo katika suala la uimarishaji utawala bora na demokrasia nchini.

Tanzania Daima

No comments: