Saturday, December 19, 2009

Mkataba kati ya TANESCO
na Statnett ya Norway



Shirika la umeme nchini (TANESCO), limeingia mkataba wa Sh8.3 bilioni na kampuni ya kusambaza umeme ya Norway, Statnett. Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugezi wa TANESCO, Stephen Mabada, katika mkataba huo wa miaka mitatu TANESCO itapata fursa kuwasomesha wataalamu wake ili kuongeza elimu juu ya usambazaji umeme.

Kupitia mkataba huu wa miaka mitatu, TANESCO itasomesha wataalamu wao na kuongeza ufanisi juu ya usafirishaji umeme na pia kuongeza ufanisi wa kazi, alisema Mabada.

Alisema kwa sasa TANESCO inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kupanua miundombinu yake pamoja na kuongeza vifaa vya kitaalamu.Upungufu wa umeme ni moja ya changamoto kubwa inayolikabili taifa, umeme ndio unaosaidia kupunguza umaskini ambao ni moja ya malengo ya milenium, kwa hiyo ndiyo maana kila siku tanajitahidi katika kuhakikisha tunatoa huduma hii kwa ufanisi mkubwa.

Mkataba huo wa fedha za Norway, Kroners 37 milioni, umefadhiliwa na serikali ya nchi hiyo na unaweza kuongezwa kwa miaka miwili endapo pande mbili zilizo usaini jana zitakaa na kukubaliana.

Mkataba huo ulisainiwa na Balozi wa Norway nchini, Jon Lomoy na Mkurugenzi Mkuu wa Statnett, Auke Lont kwa upande wa Norway, na kwa upande wa Tanzania ulisainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO, Stephen Mabada pamoja na Meneja usambazaji umeme wa TANESCO, Decklan Mhaiki.

Kwa upande wake, Balozi wa Norway, Lomoy alisema kuwa mpango huo utaisaidia TANESCO katika kuwaunganisha watu wengi zaidi katika gridi ya taifa.Lengo la Norway ni kuisaidia TANESCO ili iweze kuwaunganisha watu wengi zaidi katika gridi ya taifa, katika kipindi cha miaka mitatu, nina imani watakuwa wamefaidika sana na mkataba huu,alisema Lomoy.

TANESCO inatakiwa mjenge uhusiano wa karibu na kampuni nyingine za nchi za jirani ili muweze kubadilishana utaalamu na mbinu za uzalishaji umeme, hata sisi huwa tunabadilishana utaalamu na nchi za majirani zetu, aliongeza.

Chanzo: Mwananchi

No comments: