na Ramadhani Siwayombe, Arusha
SAKATA la raia wa kigeni kuwadhalilisha Watanzania, sasa linaonekana kushika kasi, baada ya raia mwingine wa AfrikaKusini kumdhalilisha askari kwa kummwagia maji machafu.
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya raia wa Canada ambaye pia ni ofisa ubalozi wa nchi hiyo nchini, kumtemea mate askari wa usalama barabarani na mwandishi wa habari.
Katika tukio la juzi, raia huyo wa Afrika Kusini, Gesina Susanna Hayes, alimmwagia maji machafu askari huyo aliyekuwa akilinda Benki ya Barclays iliyopo katika majengo ya TFA na kisha kumtolea matusi ya nguoni.
Baada ya tukio hilo, askari huyo PC Sengerema mwenye namba G.1757, alimdhibiti Hayes na kumfikisha katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa na kufunguliwa jalada namba AR/RB/8591/09 kabla ya kufikishwa mahakamani.
Raia huyo wa Afrika Kusini, alipofikishwa mahakamani alishindwa kujitetea, hivyo Hakimu Magesa wa Mahakama ya Mwanzo Maromboso mjini hapa kumhukumu kifungo cha miezi mitatu jela baada ya kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashitaka.
Wakati hukumu hiyo inatolewa, raia mwingine wa Canada alimdhalilisha askari wa usalama barabarani kwa kutemea mate.
Licha ya raia huyo wa Canada kumtemea mate askari huyo, pia alimtemea mate mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha TBC1, Jerry Muro, lakini kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria, Ubalozi wa Canada nchini ulitangaza kumrejesha nchini kwao kutokana na kitendo hicho.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima 16-12-2009
|
No comments:
Post a Comment