Tuesday, December 01, 2009

Rais Kikwete ziarani Cuba




Na Mwandishi Maalum, Havana, Cuba


Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Havana, Cuba, kuanza ziara rasmi ya siku tatu nchini Cuba kwa mwaliko wa Rais Raul Castro Ruz.

Ndege iliyombeba Rais Kikwete na ujumbe wake imewasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jose Marti, mjini Havana, kiasi cha saa tisa na nusu mchana (sawa na saa tano unusu mchana kwa saa za Afrika Mashariki), ikitokea Trinidad na Tobago.

Rais Kikwete na ujumbe wake umekuwa katika Trinidad na Tobago tokea Alhamisi iliyopita, Novemba 26, 2009, kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Nchi za Jumuia ya Madola uliofanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, wa Port of Spain. Mkutano huo umemalizika jana, Jumapili, Novemba 29, 2009.

Kwenye uwanja wa Jose Marti, Rais Kikwete na ujumbe wake wamelakiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Mama Ana Teresita Gonzalez, Balozi wa Cuba katika Tanzania Ernesto Gomez, na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Cuba Hector Igarza.

Wengine waliompokea Rais Kikwete ni Balozi wa Tanzania katika Cuba Balozi Peter Kallaghe ambaye ana makazi yake nchini Canada, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Profesa David Mwakyusa na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Sultan Mugheiry.

Pamoja na kwamba Rais Kikwete na ujumbe wake ambao ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe amewasili Cuba leo, sherehe za mapokezi yake rasmi zitafanyika kesho, Jumanne, Desemba Mosi, 2009, kwenye Kasri ya Mapinduzi (Palace of the Revolution).

Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo rasmi, Mhe. Rais Kikwete kesho ataanza ziara yake kwa kuweka shada la maua kwenye kumbukumbu ya Shujaa wa Kitaifa wa Cuba, Jose Marti kwenye Bustani ya Mapinduzi na kutembelea Jumba la Maonyesho la Shujaa huyo.

Baadaye, Rais Kikwete atatembelea kiwanda cha dawa cha Labiofam kabla ya kwenda Kasri ya Mapinduzi kwa ajili ya mapokezi rasmi na kufanya mazungumzo ya Kiserikali na Rais Jenerali Raul Castro Ruz.

Jioni ya kesho, Jenerali Raul Castro Ruz, atamwandalia chakula rasmi cha usiku cha makaribisho. Keshokutwa, Jumatano, Desemba 2, 2009, Rais Kikwete atakwenda Jimbo la Santiago de Cuba, ambako yalianzia Mapinduzi ya Cuba ya mwaka 1959.

Mhe. Rais Kikwete aliwasili katika eneo la nchi za Caribbean tokea Jumatatu, Novemba 23, 2009, kuanza ziara rasmi ya Kiserikali yenye mafaniko makubwa katika Jamaica kabla ya kuelekea Trinida na Tobago.

No comments: