Waziri wa sheria:
Utendaji duni wa kazi idara ya uhamiaji.
Waziri wa sheria, Bw. Knut Storberget hafurahishwi na utendaji wa kazi wa idara ya uhamiaji ya Norway, Utlendingsdirektoratet (UDI), hivyo anaangalia uwezekano wa kubadili mwenendo mzima wa utendaji kazi wa idara hiyo.
Storberget amesema watu wengi wanarefusha kesi zao walizoomba vibali vya kuishi kwa kukata rufani mara nyingi kati ya UDI, Halmashauri ya Rufaa za Uhamiaji (UNE = utlendingsnemnda), mahakama za Norway na za kimataifa, hivyo kuendelea kuishi Norway bila sababu.
Storberget amesema haelewi kwa nini mtu anaweza kuomba kibali akanyimwa akakata rufaa zaidi ya mara tatu, akakataliwa na akaanza upya kukataa rufaa na bado akakubaliwa kuendelea na kukata rufaa.
UDI wamekuwa wakisumbuliwa ucheleweshaji wa majibu ya maombi ya vibali vya kuishi na kufanya kazi. Kuna maombi ya zaidi ya 50 000 ya watu wanaosubiri kujibiwa na hawajajibiwa. Mengi ya maombi hayo yana zaidi ya mwaka mzima.
Storberget amesema inaonyesha kuna utendaji duni wa kazi kwenye idara ya uhamiaji. UDI wamekuwa wakilalamika kuwa wanahitaji hela na wameshapewa za kutosha na haelewi kwa nini washindwe kutimiza majukumu yao.
Storberget amesema kuwa kama wingi wa mlundiko wa maombi hayo ni kwa sababu ya kesi hizo alizozitaja za rufaa, basi ataangalia pia uwezekano wa kubadili ukataji rufaa wa kesi za uhamiaji.

No comments:
Post a Comment