Wednesday, March 03, 2010


Hukumu ya Lil Wayne yahairishwa



Hukumu ya "rapa" Lil Wayne (miaka 27) iliyokuwa itolewe jana Jumanne, Machi Mbili imeahirishwa tena. Kuahirishwa kwa hukumu yake kunatokana na moto uliotokea mahakamani kwenye kitongoji cha Manhattan, jijini New York. Mara ya kwanza hukumu iliyokuwa itolewe Januari mwaka iliahirishwa kwa sababu Lil Wayne alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya meno.

Lil Wayne ambaye jina lake haswa ni Dwayne Carter, alikubali mahakamani mwaka jana kosa la kukutwa na kumiliki silaha kinyume cha sheria. Alikamatwa Julai 2007. Mwanzoni alikataa kukubali kosa, lakini mwaka jana alikubali kumiliki silaha kinyume na sheria.

Anatarajiwa kurudi tena mahakamani kesho Jumatano. Lil Wayne pamoja na "rapa" mwingine Ja Rule (Jeff Atkins) walikamatwa nyakati tofauti, lakini walikuwa kwenye konseti moja hiyo siku. Ja Rule amekataa katakata kuwa na kosa la kukutwa na kumiliki silaha isivyo halali.

Kama akihukumiwa kesho Jumatano, Lil Wayne anaweza kupewa adhabu ya kifungo cha mwaka. Anaweza kuachiliwa na kutoka jela baada ya miezi minane akionyesha tabia nzuri.

No comments: