Tuesday, April 20, 2010


Kiswahili kutumika rasmi serikalini


SERIKALI imeagiza kutumika kwa Kiswahili katika usaili kwa watu wanaoomba kazi kwenye Wizara na Idara za Serikali na pia imetaka matangazo yote ya kazi za idara za umma yatolewe kwa lugha hiyo badala ya lugha ya kigeni kama inavyofanyika sasa hivi. 

Katika agizo hilo, pia serikali ambalo lilitolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika bungeni, imeagizwa dhifa mbalimbali za kitaifa, hotuba za viongozi, warsha, semina na mikutano ya kitaifa iendeshwe kwa Kiswahili. 

Pia alisema maofisa wa serikali na mashirika ya umma watumie Kiswahili katika shughuli zote kama vikao vya Bodi na mawasiliano ya kiofisi pia yaendeshwe kwa lugha hiyo ya taifa pamoja na kuandika madokezo. 

Pia aliagiza sheria zote ziandikwe kwa Kiswahili ikiwa ni pamoja na kutafsiri zile zilizoandikwa kwa lugha za kigeni. Alisema jitihada za makusudi zifanyike ili shughuli za Mahakama katika ngazi zote ziendeshwe kwa Kiswahili pia. 

Mijadala inayohusu shughuli za umma iendeshwe kwa Kiswahili na kumbukumbu zote zihifadhiwe kwa lugha ikiwa ni pamoja na nyaraka zilizotumika katika mijadala kuandikwa kwa Kiswahili. Waziri pia aliagiza majina ya barabara, mitaa na mabango yaandikwe kwa Kiswahili. 

Serikali imetoa kauli hiyo baada ya Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein katika kikao cha Baraza la Mawaziri Februari mwaka huu, aliagiza na kusisitiza suala la matumizi ya Kiswahili katika shughuli za serikali na kuwakumbusha watendaji serikalini kuzingatia Waraka wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Rashidi Kawawa wa mwaka 1967. 

Mkuchika pia alisema mwaka 2005, Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), William Lukuvi aliagiza taarifa za mikutano, semina na warsha nchini zitolewe kwa Kiswahili kwa manufaa ya wananchi. 

Alisema taarifa za miradi inayohusu wananchi ni lazima zitolewe kwa Kiswahili ikiwa ni pamoja na vipeperushi na nyaraka zinazohusu miradi hiyo. 

Mwaka 1974, aliyekuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Utumishi), J. Mganga alitoa waraka alioelezea kuhusu matumizi ya Kiswahili katika ofisi za serikali ambao ulisisitiza barua kati ya Wizara na Idara ziwe za Kiswahili isipokuwa kama anayeandikiwa ni raia wa kigeni. 

Pia aliagiza vibao vyote vya majina ya ofisi au wizara na matangazo kama ya mahafali, sikukuu mbalimbali yaandikwe kwa Kiswahili, madokezo baina ya maofisa maofisini yawe ni kwa lugha ya Kiswahili, fomu zote za kujazwa ziwe za Kiswahili. 

Waziri huyo alirejea Waraka wa Kawawa ambaye ulimtaka kila ofisa wa Serikali na viongozi wote wawe mfano mwema katika kutumia lugha ya Kiswahili na kusiwe na kuchanganya changanya lugha na mfano mzuri katika mijadala ndani ya Bunge na watu wote waone fahari katika Kiswahili. 

“Kwa kuzingatia matamko haya na umuhimu wa lugha ya Kiswahili ikiwa sasa ni lugha ya kimataifa inayotumiwa mathalani kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, Serikali inasisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za serikali na kutoa kauli kuwa pamoja na vipengele vilivyosisitizwa awali,” alisema Mkuchika.


No comments: