Friday, October 29, 2010

Jihadhari kutumia kompyuta paja (Lap Top) kwenye sehemu za umma!!!


Je, wewe ni mmoja kati ya wale wanaokaa kwenye mikahawa au sehemu zingine za umma na kutumia kompyuta yako ya pajani?

Kama wewe ni mmoja wao, basi jihadhari sana na kukaa kwenye sehemu hizo halafu ukatumia mtandao bila nyaya "wireless network" ya bure bila ya kutumia nywila (password). Ni hatari kwa usalama wa kompyuta yako, nywila zako za benki, profaili zako kwenye mitandao jamii na vitu vinavyofanana na hivi.

Mwamerika bingwa wa TEKNOHAMA, Eric Butler ametengeneza program "Firesheep" kwa ajili ya Firefox brauza.

Kwa kutumia "Firesheep" unaweza kuingia kwenye kompyuta ya paja yoyote "uka´hacke" kwenye "profaili" ya mtu yeyote yule kiurahisi kabisa na kuiba kila kitu kwenye profaili ya mlengwa.

Juzi mwandishi mmoja, Amund Bakke Foss wa gazeti la kila siku hapa Norway, Verdens Gang (VG) alikutana na bingwa mmoja wa TEKNOHAMA wa PC World, Bjørn Unnersaker kwenye Cafe Fiasco kwenye Stesheni Kuu Oslo ili kuthibitisha wizi wa namna hii.

Wakiwa Cafe Fiasco kwenye mtandao bila nyaya wa bila kutumia nywila, mwandishi wa gazeti la VG, akaingia kwenye profaili yake ya Facebook na jamaa wa PC World naye akaingia kwenye Firesheep.

Bila kujua hili wala lile linatendeka, mwandishi wa VG akashtukia ujumbe unatokea kwenye profaili yake ya Facebook kutoka kwa jamaa wa PC World kuwa:

"Nimehaki profaili yako ya Facebook na naweza kuifanyia chochote nitakacho!"

Mwandishi wa VG kidogo azimie! Firesheep ni rahisi kuitumia na mtu yeyote yule anaweza kuitumia na kuingia kwenye mtandao wa mtu mwingine.

Butler mwenyewe anasema kuwa ametengeneza Firesheep ili kuwatahadharisha watumiaji wa mitandao bila nyaya jinsi ilivyo na wajihadhari za athari zake.




Jinsi ya kujihadhari
  • Jaribu kuepuka kutumia mitandao bila nyaya ambayo huhitajiki kutumia jinatumizi (Username) na nywila (password), kama unaweza tumia "mobile broadband" kama 3G.
  • Na kama umeamua kutumia mtandao bila nyaya ambao hauhitaji kutumia jinatumizi na nywila, basi tumia huduma za VPN (VPN services) ambayo inabadilisha automatiki mawasiliano yako na kuyaweka kwenye koda ili yasiibiwe
  • Ukiwa kwenye mtandao bila waya na huna uhakika jinsi ya kutumia huduma za VPN, basi usije kurogwa na kufungua baruapepe yako, Facebook yako au huduma zingine za namna hii.Huduma za mitandao ambazo unaweza kuwa na imani nazo kuwa ni salama, zinaanza na HTTPS (Hyepertext Transfer Protocol Secure) kwenye anwani ya mtandao. Mfano:
  • https://www.facebook.com/ hii ina usalama kuliko http://www.facebook.com/ hii haina usalama!!

Soma zaidi kuhusu HTTPS: http://en.wikipedia.org/wiki/HTTP_Secure

1 comment:

Tausi Usi Ame Makame said...

Shukran Chama Cha Watanzania Oslo kwa posting hii!!!!!!!