Saturday, November 06, 2010

Kuapishwa kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dr. Jakaya Kikwete akiwa katika gari maalum pamoja na mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,Jenerali Davis Mwamunyange wakati wakiingia katika uwanja wa Uhuru kwa ajili ya shughuli ya kuapishwa kwa Rais Jakaya Kikwete. 

Wanausalama wakiingia kwa staili ya aina yake wakati Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akiingia kwenye uwanja wa Uhuru leo. 

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma naye amehudhuria katika Sherehe hizo kama unavyomuona akielekea jukwaa kuu. 

Wageni mbalimbali wakishuhudia sherehe hizo mchana huu

Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameapishwa leo majira ya saa tano na nusu asubuhi baada ya kushinda matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010.
Rais Kikwete ameapa mbele ya jopo la viongozi wa serikali wakiwemo Jaji Mkuu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Mkuu Kiongozi, Jopo la Majaji, Wakuu wa Vyombo vya ulinzi, Viongozi Watatu wa Madhehebu ya Dini, Wazee Wawili kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani na Karani wa Baraza la Mawaziri.

Baada ya kuapishwa, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alikaa kwenye kiti cha jadi na kukabidhiwa Mkuki na Ngao na wazee wa jadi kama ishara ya uongozi na mafanikio mema.

Naye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal aliapishwa mara baada ya Mheshimiwa Rais kumaliza kiapo chake.Baada ya dua na sala kutoka kwa viongozi wa dini na madhehebu ya dini, Mheshimiwa Rais Kikwete alipokea salamu ya Heshima kutoka kwa majeshi ambapo mizinga 21 ilipigwa, bendera ya Rais kupandishwa, gwaride lillounda Umbo la Alpha na Rais alikagua gwaride hilo.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amehutubia wananchi wa Tanzania kutokea hapa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam. Sherehe hizi za kuapishwa rasmi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete zimehudhuriwa na marais watano wa nchi za Afrika akiwemo Mhe. Robert Mugabe wa Zimbabwe, Mhe. Mwai Kibaki wa Kenya, Mhe. Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini, Mhe. Rupia Banda wa Zambia na Mhe. Joseph Kabila wa DRC.Nao Umoja wa Afrika umewakilishwa na Mhe. Jean Ping ambaye ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika.



No comments: