Monday, June 13, 2011

Serikali Ya Marekani Yaipongeza Tanzania Kwa Kupambana Na Matukio Ya Uharamia

Rais Dr.Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Bi.Hilary Clinton baada ya kufanya naye mazungumzo ikulu jijini Dar es Salaam leo asubuhi. Bi Clinton ambaye alikuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu baadaye aliondoka nchini kuelekea Ethiopia(Picha:Freddy Maro). 


RAIS Jakaya Kikwete ameiomba Serikali ya Marekani kuipatia Tanzania msaada wa Meli kubwa yenye uwezo wa kupita katika kina kirefu cha maji pamoja na mafunzo ya kijeshi ili kupambana na matukio ya uharamia katika bahari ya Hindi.

Rai hiyo imeitoa leo wakati wa mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bi. Hillary Clinton uliofanyika Ikulu Jijini Dar-Es-Salaam.

Mhe. Rais alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hadi sasa kumekuwepo na jumla ya matukio 27 ya majaribio ya utekekaji wa meli katika pwani ya bahari ya Hindi upande wa Tanzania na katika majaribio hayo meli 4 za maharamia hao zimeshikiliwa na tayari watuhumiwa kadhaa wamefikishwa mahakamani kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazowakabili.


Alisema mafanikio hayo yametokana na uwezo mkubwa ulionyeshwa na kikosi cha Wanamaji katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania. “Katika mapambano haya bado Tanzania tunatafuta meli kubwa inakayoingia katika maji ya kina kirefu ili kukabiliana na uharamia huu,” Alisema Rais Kikwete.Kwa upande wake Waziri Hillary Clinton ameeleza kufurahishwa kwake na hatua zilizochuliwa na Tanzania kupambana na vitendo vya uharamia katika bahari ya Hindi na kuhaidi kutoa ushirikiano kwa kadri inavyowezekana.


Akizungumzia kuhusu mgororo unaondelea nchini Sudan, Rais Kikwete ameeleza kuwa ameshafanya mazungumzo na Rais wa Sudan ya Kusini Silva Kiir pamoja na Rais Omar EL- Bashir kuhusu mgogoro huo na anatarajia matokeo ya mkutano wa usuluhishi wa mgogoro huo unaofanyika leo (jana)unaofanyika mjini Addis Ababa Ethiopia utatoa mwelekeo wa kumaliza mgogoro huo.

Aidha katika hatua Mhe. Rais Kikwete amesema hawezi kutabiri Rais atayeiongoza Zimbabwe mara baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

“Kuhusu nani atakuwa Kiongozi wa Zimbabwe hilo liko nje ya uwezo wangu. Zimbabwe ni moja ya maeneo yanayojadiliwa na vikao vya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kinachotakiwa kwa pande zote mbili ni kutimiza makubaliano yao awali ili kuondoa migogoro ya kisiasa nchini humo,” alisema Rais Kikwete.

Viongozi hao awali katika mazungumzo yao Ikulu mjini Dar-Es-Salaam wamezungumzia migogoro mbalimbali ikiwemo ya kisiasa inayozikabili nchi za Bara la Afrika zikiwemo Madagascar, Zimbabwe, Somalia na Sudan.

Bi. Hillary ameipongeza msimamo wa wazi Tanzania katika kutatua migogoro mbalimbali ya kisiasa Barani Afrika.

“Naipongeza Tanzania kwa kuonyesha mwelekeo na msimamo wa wazi katika utatuzi wa migogoro mbalimbali Barani Afrika,” alisema.

Kiongozi huyo wa juu katika Serikali ya Marekani amemaliza ziara yake ya siku tatu ya Kiserikali leo (jana) hapa nchini na ameelekea nchini Eithiopia. Joseph Ishengoma Imeandikwa na Ismail Ngayonga

MAELEZO Dar-Es-Salaam

No comments: