Thursday, June 16, 2011

Tatizo la umeme Tanzania

Norway yashauri mradi wa Stgiler's Gorge ufufuliweImeandikwa na Shadrack Sagati; Tarehe: 16th June 2011 Habari Leo

BALOZI wa Norway nchini, Ingunn Klepsvik ameshauri Tanzania kufufua mradi wa umeme wa maji uliopo katika maporomoko ya mto Rufiji ya Stgiler’s Gorge, ili ipate nishati ya uhakika ya umeme kusaidia kuinua uchumi wake.

Klepsvik alitoa kauli hiyo katika mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Kampuni ya IPP Reginald Mengi hivi karibuni ambaye naye aligusia mradi huo ambao miaka ya nyuma nchi hiyo ilionesha nia ya kuuendeleza lakini ukapata upinzani mkubwa kutoka kwa wanaharakati wa mazingira na Benki ya Dunia.

Klepsvik alisema Tanzania imekuwa na matatizo ya umeme kutokana na vitendo vya ukataji ovyo miti vinavyoendelea hapa nchini kwenye maeneo ya hifadhi za misitu na kulikojengwa vituo vya kuzalishia umeme wa maji.

Balozi huyo ambaye nchi yake ilishiriki katika ujenzi wa baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme wa maji hapa nchini, alisema miaka ya nyuma amewahi kutembelea kituo cha uzalishaji cha Kihansi ambacho kwa sasa hakizalishi umeme kama ilivyotakiwa kutokana na uharibifu wa mazingira.

Alisema, Tanzania inahitaji mikakati za kuondokana na tatizo la nishati ya umeme kwa kufufua mradi huo wa Stigler’s Gorge ambao nchi yake miaka ya nyuma ilijaribu kuufanyia utafiti lakini utekelezaji wake ukakwama.

Maporomoko hayo yanasemekana kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati zaidi ya 2,000 za umeme wa gharama nafuu. Hata hivyo tayari Serikali imeshaunda kikosi kazi cha kuhakikisha mradi huo wa umeme unaanza kufanyiwa kazi.

Kwa upande wake Mengi akizungumzia sekta ya nishati ya umeme, alisema anatambua kuwa Norway ilikuwa tayari kuendeleza mradi huo wa maporomoko ya Stigler’s Gorge lakini wakati huo Benki ya Dunia ikadai kuwa Tanzania ilikuwa haihitaji umeme mwingi huo wa megawati 2000.

Mengi alisema, yeye anaona tatizo la kuwepo upungufu wa nishati ya umeme ni kuwepo mipango ya muda mfupi ambayo kila waziri anayeingia anakuwa na mipango yake na kusahau kuweka mipango ya muda mrefu na endelevu katika kutatua tatizo hilo.

No comments: