Monday, July 11, 2011


Wakimbizi wa Kisomali Kyela


Bado nakumbuka ile story na Mdosi (mwanachama mmoja wa Tanzanet) kuhusu kuzamia Europe kupitia Sudan, Egypt mpaka Greece. Ilikuwa rahisi mtu kufikiria kwamba huenda Mdosi kaongeza chumvi nyingi lakini matukio ya siku za karibuni wilayani Kyela yananifanya nianze kuiamini kabisa ile story ya Mdosi.

Mimi kijijini changu nilichozaliwa kinaitwa Katumba na ndio kijiji cha mwisho kabla ya kuingia Malawi. Upande mmoja kijiji hicho kinapakana na ziwa Nyasa na upande mwingine mto Songwe ambao ndio unatenganisha Tanzania na Malawi.

Kwa muda wa karibu miezi sita sasa nimekuwa nikiambiwa pale kijijini kuna Wasomali wengi wakimbizi. Mwanzoni sikuamini maana out of all the places in the World, kweli Wasomali kule kijijini? Lakini kufikia mwezi wa tano hizo habari zikawa zinazidi kuja na kwamba hata kazi ndogondogo sasa pale kijijini zinafanywa na Wasomali. Wanafanya vibarua ili wapate pesa ya kula wakati wanasubiri kuendelea na safari zao. Hapo ndipo nikakumbuka story ya Mdosi.

Baadaye, nikaambiwa kuna deal kubwa kati ya viongozi wa kijiji hicho na polisi ambao wanawaachia hao Wasomali wazagae hapo kijijini wakati wanasubiri kuendelea na safari zao. Nikaamua kumpigia simu Mwenyekiti wa kijiji ambaye alikuwa anahusika na hilo deal na mimi naelewana naye vizuri na kumwambia ni kosa kuwaficha wakimbizi na watoe taarifa polisi. Yeye akaniambia polisi na viongozi wengine wa wilaya wanajua na kila wiki wanakuja kuchukua mgawo wao. Na kwamba kama viongozi wa juu wanafisadi nchi kwenye mikataba na wao ndio nafasi yao ya kula. Mimi nikawaambia kwa ushauri wangu wasijihusishe na biashara hiyo maana itawaletea balaa na kwenda jela na kuziacha familia zao zikiteseka.

Kama ilivyo biashara yoyote haramu, wale wanaofaidika wakawa wanashangilia na kuona utajiri umewafuata wakati wananchi wengine wakawa wanalalamika. Ushauri wangu ukawa kwa viongozi kupeleka malalamiko rasmi wilaya kwa njia ya mdomo pamoja na barua ili mambo yakiharibika wasije wakalaumiwa. Binafsi nikaona hii hali sasa ni mbaya sana, inakuwaje Wakimbiza kama 150 kwa mpigo wanaonekana kwenye kijiji kimoja na serikali inashindwa kuchukua hatua?

Kumbe kuna deal kubwa, hao Wasomali wanafika Mbeya na kuna vijana wa Kyela wanawafuata kwa magari kutoka huko na kuwapeleka Kijijini katumba ambako wanakaa wakisubiri boti ambalo linawabeba na kuwapeleka Malawi na safari inaendelea huko mpaka South Afrika na lengo likiwa ni kuja Europe.

Sasa, juzi juzi, habari zikafika mkoani na polisi mkoa wakatoa amri wahusika wote wakamatwe mara moja. Polisi wilaya waliposikia hilo nasikia wakawajulisha wahusika kwamba tunakuja kuwakamateni. Wahusika wakawaficha Wasomali msituni na wao wenyewe wakakimbilia upande wa Malawi. Kutoka kijijini kwenda Malawi ni kama dakika 10 kwa mguu. Polisi wakaja pale wakachukua tu mapipa ya petroli kwa ajili ya maboti na wakakamata vijana watatu pale kijijini ambao walionekana wana habari za kuwepo Wasomali. Cha kushangaza hao vijana inasemekana ni wale waliokuwa wanapinga wasomali kuwepo hapo kijijini. Wametupwa rumande Tukuyu bila dhamana mpaka tarehe 14 July. Wale wahusika wenyewe mpaka sasa bado wamejificha Malawi. Baadaye boti zikaja na kuwachukua hao Wasomali. Nafikiri sasa wamewapigia simu wenzao kuwaambia biashara isimame kwanza.

Nimebaki kushangaa, inakuwaje nchi imefika mahali ambapo hakuna anayejali kuhusu usalama wa raia na badala yake kila mtu anafikiria matumbo yake tu? Kama Wasomali wengi kiasi hicho wanaweza kufika kwenye kijiji ambacho kiko pembezoni hivyo na hatua zisichukuliwe kwa karibu miezi kadhaa, je kuna sehemu ngapi zingine mambo kama hayo yanatokea? Jeshi letu kwa kweli is not fit for purpose.

Na George Mwakalinga (MwanaTanzanet)

Imenyofolewa kutoka Tanzanet kwa idhini ya mwandishi



1 comment:

Anonymous said...

Hapa ndo tunaona jinsi gani vyombo vyetu vya usalama vilivyo hohe hahe! yaani haiwajii akilini kuwa inawezekana miongoni mwa hao Wasomali, kuna majangili au magaidi? Haiimanishi kuwa Wasomali wote ni majangali au magaidi la hasha just for security reasons wangekuwa wanafuatiliwa kwa makini. Lakini wapi...mnaofisa wa usalama wa taifa waliowekwa wilayani na mikoani kazi zao ni kula na wao!!