Wednesday, November 23, 2011

Mganga ni wewe mwenyewe

Wa’ngaika kila siku, ukiwasaka waganga,
Waenda kule na huku, umefika hata Tanga,
Mepeleka hadi kuku, ‘lipokwenda Sumbawanga,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Tajihangaisha bure, kudhani wanakuroga,
Mume usimpapure, ukadhani yeye boga,
Mume simcheze shere, kwayo mambo ya kuiga,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Mume usipomtii, lazima atakuchoka,
Kama wewe husikii, ndoa itaharibika,
Na ndoa haikawii, vivi hivi kuvunjika,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Chunga mwenendo wako, uone kama wafaa,
Wacha kufanya vituko, ndoa itakuchakaa,
Sikudanganye wenzako, kwani dunia hadaa,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Mpe mumeo heshima, naye atakuthamini,
Mwambie kwayo hekima, yaliyo mwako moyoni,
Kubali akikutuma, uwache umajinuni,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Usiufate mkumbo, sijaribu asilani,
Yatakuchachia mambo, wenza wacheke pembeni,
Ndoa hainazo tambo, bali busara kichwani,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Mwanamke mpumbavu, hubomoa nyumba yake,
Na mwanamke mvivu, hajui wajibu wake,
Tena hawi msikivu, labda siku atake,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Watu wakikukosoa, ni vema uwaelewe,
Ndoa kiitia doa, talia wewe mwenyewe,
Wengine wataopoa, kutunza usaidiwe,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Kutoka kwa   Fadhili Mshairi

No comments: