Friday, January 27, 2012

Nchi yetu Tanzania, wapi inakwenda?


Na Maggid Mjengwa,

Ndugu zangu,

Juzi hapa nilisiamama kijiji cha Ifupira kule Mufindi. Nilimpa lifti mama aliyekuwa akitoka kwenye kazi ya kibarua cha kuvuna chai kwenye  moja ya mashamba ya wakulima wakubwa  wa chai wa kule Mufindi.

Anaitwa Mama Glad, alionekana kuwa aliyechoka sana baada ya kazi  ngumu ya siku nzima. Ujira wake? Shilingi elfu tatu na mia tano kwa siku.  Ni kazi ngumu  na malipo haba.

Inanikumbusha wimbo wa zamani walioimba wazee wetu;
“ Tumewalimia bure, mashamba ya wakoloni
Nusu mraba, mshahara chumvi!”

Ni kweli, wazee wetu miaka hiyo walilima mashamba ya makabaila kwa mishahara ya nusu kibaba cha chumvi. Na leo hii,  miaka hamsini baada ya uhuru, kuna Watanzania wenzetu wanaofanya kazi ya vibarua kwenye mashamba ya makabaila wanaoitwa wawekezaji . Wanafanya kazi ngumu kwa mishahara isiyotosha hata kununua kilo ya nyama.  Kiko wapi chama cha Wafanyakazi vibarua wa mashambani?

Mama Glad anazungumzia ugumu wa maisha unaomfanya azime kibatari chake  kabla ya saa nne usiku. Ndio, mafuta ya taa yamepanda bei. Mama Glad ananunua mafutaya taa kwa kipimo cha koroboi.  Leo ananunua koroboi ya mafuta kwa shilingi mia mbili. Koroboi ni kipimo cha chini kabisa cha ujazo wa mafuta ya taa. 

Mama Glad ananiambia, kuwa mwaka jana kipimo hicho hicho alinunua kwa shilingi hamsini. Bei ya mafuta ya taa imepanda na ujira wake uko pale pale. Bado anapokea shilingi elfu tatu na mia tano kwa siku.  Na akiumwa kiasi cha kushindwa kwenda  kibaruani? Basi, hana anachokipata kwa siku hiyo. Na kwa ujira wa elfu tatu nam ia tano ikumbuke bei ya sukari Mafinga kwa sasa ni shilingi elfu mbili na mia tano. Bado Mama Glad hajanunua unga au mchele. Anahitaji kitoweo pia.  Maisha yamekuwa magumu kwa Mtanzania wa kawaida.

Maelezo ya Mama Glad yanatuachia tafsiri nyingi. Ona hapa, miaka 50 baada ya uhuru, Mama Glad amepoteza matumaini ya kutumia taa ya umeme nyumbani kwake, na hakika ya kutumia kibatari pia imeanza kupotea.  Na kupanda kwa gharama ya umeme kunaongeza mzigo wa gharama za maisha kwa Mama Glad na Watanzania wengine kwa mamilioni, maana , bei ya bidhaa na huduma nyingine zimepanda na zitaendelea kupanda kama haziachukuliwa hatua  sahihi za kukabiliana na mfumuko huu wa bei unaoendelea sasa.

Na ya mama Glad yananikumbusha asubuhi  moja nikiwa mjini Iringa.  Niliongozana na watoto wangu wawili kwenda sokoni kupata mahitaji ya nyumbani. Ni pale Soko Kuu la Miyomboni. Sokoni pale nilisimama ili ninunue bamia, nyanya chungu na njegere. Aliyejitokeza kuniuzia alikuwa msichana mdogo wa chini ya miaka 13. Alifanya biashara ile akiwa amekaa chini juani.

Niliingiwa na simanzi kubwa, maana msichana yule alikuwa na umri uliokaribiana na watoto wangu. Nao niliwaona wakimwangalia mtoto mwenzao ambaye ameacha kuwa mtoto na kuchukua majukumu ya watu wazima. Nilimwuliza jina lake, anaitwa Rehema. Alifanya biashara ili arudi nyumbani na senti za mahitaji mengine ya nyumbani.  Alitumwa na wazazi wake. Ndivyo alivyonieleza, nilimwamini. Nimesikia simulizi kama hizo kabla.

Nilimpa noti ya shilingi elfu mbili. Nilivyoona kuwa alivyonifungia vimejaa mfuko, nikamwuliza kama kuna hela nyingine napaswa kuongeza. Alinijibu; ” Wewe ndio unanidai shilingi mia tatu, ngoja nikatafute chenji”. Nikamwambia asiende kutafuta chenji. Mia tatu ile abaki nayo.

Ilinitia simanzi zaidi. Hakika, msichana Rehema hakuwa na  kosa. Tatizo ni la kimfumo zaidi. Ndio, tunazidi kuukumbutia ubepari, mfumo unaozidi kuongeza idadi ya masikini, idadi ya wanaoshindia mlo mmoja kwa siku, idadi ya wanaopitisha siku kama walivyoipokea. Idadi ya wasio na ajira na wasio na hakika ya kupata huduma bora za msingi za kijamii ikiwamo  elimu na afya.

Na kuna wanaochuma na kisha kujitangaza kuwa wanawasaidia yatima na wenye kuishi kwenye mazingira magumu. Watu hawa  walipaswa pia  kulipa kodi zitakazosaidia kugharamia elimu na afya za wanyonge walio wengi. Ndio, katika mfumo huu wa soko huria tulipaswa tujenge nidhamu ya kukusanya kodi ili zisaidie kuinua uchumi wa nchi na ustawi wa jamii. Iliwezekana huko nyuma, inawezekana sasa.

Maana, hii ni nchi yetu.Hatima yetu kama watu binafsi, kama vikundi vya watu na kama taifa inatutegemea sisi wenyewe. Umasikini wa watu wetu ni umasikini wetu. Kiitikadi mimi ni ‘ Social Democrat’ na bado naamini mfumo wa enzi za Mwalimu wa Ujamaa na Kujitegemea bado una nafasi katika jamii yetu.


Mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea uliofanyiwa mabadiliko ya kimsingi unaweza kutuhakikishia ulinzi wa maslahi ya nchi yetu. Ni kwa sera zenye kuhakikisha usawa wa watu. Sera zitakazohakikisha kodi inakusanywa na kutumika katika yaliyo muhimu na yenye kumsaidia pia mwananchi wa chini katika nchi yetu. Mwananchi aweze kupata elimu bora na huduma bora za afya kati ya mengineyo ya msingi.

Tuazimie sasa kuwajibika kwa pamoja kwa maslahi ya nchi yetu. Na tukifanya ajizi, tutaigeuza nchi yetu kuwa ‘ nyumba ya njaa’.  Nimeamua kubaki kuwa Mjamaa. Nahitimisha.

(Makala hii imechapwa kwenye gazeti Mwananchi Jumapili, Januari 22, 2012)


No comments: