Sunday, May 05, 2013JINAMIZI la kashfa za ufisadi limeendelea kuwaandama Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye sasa ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), kuwa ndio waliouza nchi katika utawala wao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ndiye aliyewataja viongozi hao kuuza nchi kwa wageni wanaochimba madini yanayowanufaisha zaidi wageni kuliko Watanzania.

Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo jana jijini Mwanza alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa Tanzania Daima Jumapili, muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa muda mkutano wa kujadili na kuchangia mawazo juu ya maendeleo kwa wote katika Mkoa wa Mwanza.

“Kizazi hiki na kijacho viwatupie lawama Mkapa na Chenge, hawa wameliingiza taifa kwenye mikataba ya unyonyaji ya sekta ya madini inayowaneemesha zaidi Wazungu wanaojua thamani na umuhimu wa dhababu kuliko Watanzania wenye ardhi inayotoa madini husika,” alisema.

Alibainisha kuwa Tanzania inatafunwa na saratani mbaya ya mikataba mibovu ya madini iliyoasisiwa na Mkapa kwa kushirikiana na Chenge katika utawala wa Awamu ya Tatu iliyosifika kwa sera ya ubinafsishaji wa mali za umma zilizokabidhiwa kwa wawekezaji wengi wao kutoka nje ya nchi.

No comments: