Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa
taarifa ya tukio la leo, Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa
Katoliki la Mt. Joseph Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha.
Tukio hilo la kigaidi limesababisha mtu mmoja
kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa. Rais Kikwete analaani vikali
shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu katili, waovu na wenye dhamira mbaya
na nia mbaya kwa Tanzania na watu wake.
Rais Kikwete ameagiza vyombo vya usalama nchini
kumsaka mtu au watu waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha kwenye
vyombo vya sheria. Vile vile Rais Kikwete amewataka wananchi wote kuwa
watulivu wakati Serikali na vyombo vyake inaendelea kufuatilia tukio hili.
Tutawasaka popote walipo na kupambana nao bila
huruma. Aidha, tutakabiliana na aina yoyote ya uhalifu nchini iwe ni
ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa namna hiyo au wa namna nyingine, uwe na
chimbuko lake ndani ya nchi ama nje ya nchi yetu.
Kamwe hatutakubali kuwaacha wavuruge amani na
usalama wa Tanzania na watu wake. Rais anaamini kuwa Serikali, kwa msaada na
ushirikiano wa wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa ipasavyo.
Aidha, Rais Kikwete anatoa rambirambi za dhati ya
moyo wake kwa wafiwa na wale wote ambao wamejeruhiwa katika tukio hilo.
Anaungana nao katika machungu na msiba. Rais pia anawaombea wote walioumia
katika tukio hili wapate nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi
wa taifa.
Rais Kikwete vilevile anatoa pole nyingi kwa
viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki kwa tukio hili la kusikitisha na
kuvurugika kwa ibada na shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa Kanisa lao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
5 Mei, 2013
No comments:
Post a Comment