Mabere Marando
Mwanasiasa mashuhuri nchini,Mabere Marando,amesema iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa mwaka huu, basi Uchaguzi Mkuu wa Oktoba hautafanyika.
Kama hakutakuwepo uchaguzi mkuu,basi kuna uwezekano wa Raisi Jakaya Kikwete kuendelea kuwa madarakani,amesema Marando.
Kwahiyo juhudi zozote za kutaka kura ya maoni sasa,wakati hakuna muda wa kutosha, amesema Marando,ni mbinu za kutaka rais Kikwete abaki madarakani zaidi ya muda aliopewa na katiba ya sasa.
Marando amesema kifungu cha 294 cha Katiba Inayopendekezwa kimeweka mashariti ya mpito ambayo lazima yatekelezwe kabla ya uchaguzi mkuu.
Lakini amesema,masharti hayo hayawezi kutekelezwa katika kipindi kifupi kilichosalia;jambo ambalo litalazimisha uchaguzi huo kusogezwa mbele.
Miongoni mwa mashariti ambayo Marando anasema yatazuia kufanyika uchaguzi mkuu,ikiwa kura ya maoni itafanyika na katiba kupitishwa,ni kutokuwapo kwa sheria mpya ya uchaguzi.
Amesema,kwa kuwa Bunge la Muungano litavunjwa Julai,hakutakuwa na bunge la kutunga sheria zinazotamkwa katika katiba mpya na zinazohitajika kwa “utekelezaji bora wa katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya mwaka 2014″ ambayo inapaswa kuanza kutumika kwa mujibu wa sheria mara baada ya kupitishwa.
Naye Prof.Gamaeli Mgongo Fimbo,mmoja wa wasomi wa uandishi wa katiba, amesema kuwa kura ya maoni ikipigwa Oktoba;na wananchi wakapitisha katiba hiyo;nae rais akatangaza kutumika baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba,taifa linaeweza kuingia katika matatizo.
Prof.Mgongo-Fimbo amesema,”kwa hivi ilivyo,labda rais atangaze katiba mpya kutumika baada ya uchaguzi.Vinginevyo, tutaingia katika mgogoro na pengine hata vurugu”.
Msomi huyo amesema kuwa mgongano mkubwa uliopo katika masharti ya Katiba Inayopendekezwa unatokana na Bunge Maalumu la Katiba kutupilia mbali rasimu ya Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Amesema,”Kama wangefuata mapendekezo ya rasimu ya Jaji Warioba,kusingelikuwa na matatizo.Lakini kwa hivi walivyoweka, kulazimisha kura ya maoni,ni kutaka kutofanyika uchaguzi.
“Maana hapa itategemea rais ameamkaje. Itategemea mstuko ulioko nyuma yake.Bali kwa kuwa inatoa muda wa kujiongezea nyadhifa,anaweza kuruhusu katiba itakayopatikana kuanza kutumika kesho,jambo ambalo litaathiri moja kwa moja uchaguzi mkuu,”amesisitiza.
Hata hivyo,Rais Kikwete tayari ameeleza mara kwa mara kuwa hana mpango wa kuendelea kubaki madarakani,kinyume na muda wake wa sasa uliotajwa na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya mwaka 1977.
Akiongelea hilo Marando anasema “yawezekana Rais Kikwete hataki kubaki Madarakani.Lakini kwa haya yaliyomo humu,hakuna namna ambavyo anaweza kujiepusha na kitu hicho.
Marando amesema mgongano mkubwa uliopo katika katiba Inayopendekezwa na uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu,unaanzia kifungu cha 285 hadi 288,vinavyohusu utumishi wa umma katika Jamuhuri ya Muungano.
Kifungu cha 285 cha katiba kinasema,mtu ambae anashika madaraka ya urais kabla ya kuanza kutumika katiba hiyo,ataendelea kushika nafasi ya madaraka ya urais kwa mashariti ya katiba hii,hadi hapo rais mwingine atakapochaguliwa badala yake katika uchaguzi mkuu kwa kufuata katiba mpya.
“Hii maana yake ni kwamba,ili uchaguzu mkuu ufanyike,lazima kuundwe vyombo vitakavyosimamia uchaguzi huo.Kwa mfano,lazima kuundwe Mahakama ya Juu ya Jamuhuri ya Muungano,ambayo itaruhusu matokeo ya uchaguzi kuhojiwa mahakamani,” amefafanua.
Marando anasema,kizingiti kingine cha kutofanyika uchaguzi kiko katika mambo ya mpito kwa Bunge Maalumu la Katiba,limewekewa kipindi cha mpito kuwa miaka minne;na kupendekeza kuwa katiba ya sasa itakufa mara baada ya katiba mpya kuanza kutumika.
“Anasema Jaji Warioba alikwenda mbali zaidi.Aliweka muda wa mwisho wa kipindi cha mpito kuwa 31 Desemba 2018.Kabla ya hapo,katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya mwaka 1977 ingeendelea kutumika katika baadhi ya maeneo ambayo sheria zake hazijatungwa katika katiba mpya ya mwaka 2014.
“Lakini Katiba ya Sitta na Chenge, ilivifuta vifungu hivyo na kuelekeza kuwa Katiba ya 1977 itakoma mara baada ya katiba mpya kupitishwa na kuanza kutumika”.
Akichambua kifungu kimoja baada ya kingine,Marando amesema,ikiwa Katiba inayopendekezwa itapita,itasababisha uchaguzi mkuu wa Oktoba kutofanyika.
Marando amesema kama rais hataki kuendelea kubaki madarakani basi aachane na kura ya maoni kabla ya uchaguzi mkuu.
“Vinginevyo,hakuna namna ya kufanyika kura ya maoni;na wanaoileta wanataka kupata ushindi;na kisha katiba hiyo isiweze kutumika. Hakuna,” amesisitiza.
Chanzo cha habari: http://www.wavuti.com/katiba-inayopendekezwa-ikipita
No comments:
Post a Comment