Monday, April 13, 2015

ZITTO ASHANGAA RUGEMALIRA KUPEWA TENDA YA UJENZI




Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameeleza kushangazwa na hatua ya Serikali kuwapatia kazi ya ujenzi wa Bandari ya Mwambani mkoani Tanga watuhumiwa wa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Amesema watuhumiwa hao wamepewa kazi hiyo kupitia Mradi wa Mwambani Economic Corridor (MWAPORC), ambao utagharimu Sh trilioni 54, huku kukiwa hakuna taratibu za utangazaji wa zabuni zilizofuatwa na Serikali.
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akihutubia mikutano ya hadhara iliyofanyika katika miji ya Mafinga na Iringa ambapo alisema Serikali imeipa kazi ya ujenzi Kampuni ya VIP Engineering and Management inayomilikiwa na James Rugemalira ambaye anahusika katika sakata la Escrow.
Zitto alisema ACT-Wazalendo wanamtaka Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta afanye uchunguzi kuhusu mradi huo wa Mwambani na achukue hatua kwa kile alichodai kuwa utapeli wa watu wa Escrow.
“Mwambani Economic Corridor Project hapakuwa na zabuni yoyote iliyotangazwa, na huu mradi umekuwa ukiandaliwa na Serikali. Sheria ya Private Public Partnership (PPP) imeweka utaratibu wa zabuni kwa miradi ya ubia na Serikali.
“Taratibu hazijafuatwa, hakuna zabuni iliyotangazwa kuhusu Bandari ya Mwambani, miradi mikubwa kama hii Serikali hutakiwa kutoa ‘guarantee’ kwa mikopo ambayo inachukuliwa.
“Hivyo kuhusika kwa Rugemalira wa Escrow na mwanasheria Cathbert Tenga wa Richmond kwenye mradi huu ni mwendelezo wa miradi ya kitapeli,” alisema Zitto.
Zitto ambaye pia alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema uzito wa mradi huo wa bandari unakwenda sambamba na reli ambayo itafika hadi Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Alimtaka Waziri Sitta kutoa taarifa kwa umma kwa kuwa taifa limechoshwa na miradi ya kitapeli.

No comments: