Friday, November 16, 2007

WASIFU WA WIKI


Dk Sengondo Mvungi:

Kumeibuka ubaguzi katika elimu

Aristariko Konga

OKTOBA 14,2006, kulifanyika kongamano lililojadili hatari ya kuibuka kwa matabaka katika sekta ya elimu nchini, na umuhimu wa serikali kuzuia hali hiyo.

Katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alitoa mada iliyokuwa ikizungumzia wimbi la kuibuka kwa ubaguzi katika sekta hiyo, na kuonya kwamba endapo hali hiyo isingedhibitiwa, basi amani ya nchi ingekuwa mtegoni.

Mada hiyo, ilivuta wadau wengi wa sekta ya elimu, kuanzia wale wa shule binafsi, za kidini, yaani za Kiislamu na Kikristo, na hata zile za serikali. Mada ilibeba kichwa kiitwacho: "Utekelezaji wa Sera na Mipango ya Elimu Unavyojenga Matabaka Miongoni mwa Watanzania."

Katika kufuatilia maudhui ya mada hiyo, ilibidi kufanyike kongamano jingine kama hilo kujadili ubaguzi katika elimu, na hilo likafanyika Novemba 11, 2006, takribani mwezi mmoja baada ya lile la mwanzo.

Kilichoamsha hasa majadiliano kuhusu kuibuka kwa ubaguzi katika elimu ni baada ya serikali kupanga kwamba ingetoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi waliopata daraja la kwanza pekee, kwa upande wa wavulana, na daraja la kwanza na la pili kwa upande wa wasichana.

Hatari ya uamuzi huo, ni kwamba wanafunzi wanaochukua masomo ya sayansi wanakuwa katika nafasi finyu ya kupata ufadhili huo wa serikali, kwa kuwa ni wanafunzi wachache mno hufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza na la pili.

Lakini pia kuna maoni kwamba kwa kuweka madaraja kama hayo, itakuwa ni kutokuzitendea haki baadhi ya shule zilizoko kwenye mazingira magumu, zikikabiliwa na uhaba wa vifaa vya elimu, madarasa na hata walimu.Kwa hiyo, kwa maoni ya wengi, kulikuwa na haja ya Serikali kutoa mikopo bila ya kuwa na vigezo hivyo, kwani vinapalilia misingi ya kibaguzi katika sekta hiyo, jambo ambalo nchi ilikwishaondokana nalo.


DK Sengondo Mvungi

Taasisi ya Elimu ya Sheria Tanzania, yaani Tanzania Legal Education Trust (TANLET), chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake, Dk Sengondo Mvungi, ambaye pia ni mhadhiri wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ndiyo iliyoandaa kongamano hilo la pili, juu ya umuhimu wa kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu sera ya elimu ya Tanzania.

Katika kufuatilia hilo, mjadala uliofanyika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, Novemba 11, 2006, uliunda kamati ya kutafuta maoni na kuchunguza hali halisi ya ubaguzi wa kielimu nchini, kazi ambayo mpaka sasa inaratibiwa na TANLET, chini ya Mwenyekiti wake, Iddi Simba na Katibu wake, Nderakindo Kessy, ambaye pia ni Katibu wa Mipango wa TANLET.

Hivi karibuni kulifanyika mahojiano baina ya Mkurugenzi wa TANLET, Dk Mvungi na Katibu wa Mipango, Kessy, kuhusu maendeleo ya kazi za kamati hiyo na mambo ambayo imebaini, baada ya kazi ya takribani mwaka mmoja tangu kupewa kazi hiyo ya kitafiti.

"Uchunguzi umebaini kuwa katika matokeo ya mtihani (wa shule za sekondari) mwaka huu, shule za Wakatoliki ndizo zimeongoza na kati ya hizo shule ya kwanza hadi ya 10 ni za wasichana chini ya madhehebu ya Kikristo.

"Lakini jambo la ajabu, Serikali katika kuonyesha ubaguzi wa elimu, imetoa matokeo kwa njia mbili tofauti. Mosi, ikayagawa matokeo yale kati ya shule za serikali na za binafsi. Ikachukua wanafunzi watatu bora kwa upande wa wasichana na wavulana watatu bora kwenye shule za Serikali.

"Halafu Serikali ikachukua wanafunzi bora watatu wa kike na watatu wa kiume kwa shule za binafsi.Serikali haikufanya hivyo kwa bahati mbaya, ni makusudi matupu. Ni ubaguzi.

"Imetenganisha hivyo kwa sababu shule za binafsi zimefanya vizuri zaidi, wakati shule za Serikali zimefanya vibaya, na wala zisingeweza kushindanishwa na za binafsi," anasema Dk. Mvungi.Kuna maeneo mawili ya ubaguzi katika hilo, nayo ni ubaguzi kwa njia za kijinsia, kwa maana kwamba matokeo yanatolewa kwa misingi ya wasichana na wavulana, wakati ikifahamika wazi kuwa shule 10 za mwanzo zilizofanya vizuri ni za wasichana, tena zinazomilikiwa na madhehebu ya Kikristo.

Lakini pia kuna ubaguzi wa pili, ambao unahusu kutenganisha matokeo ya shule za binafsi na za Serikali. Kwa maana hiyo, wanafunzi sita ambao wamefanya vizuri katika shule za Serikali, wameziba nafasi sita za wanafunzi wa shule binafsi, kama matokeo yangetolewa bila kuangalia umiliki wa shule na ujinsia.

"Kama ni scholarship (nafasi za kusoma zaidi), basi matokeo haya yangewanyima wanafunzi sita waliofanya vizuri katika shule za binafsi, ambao nafasi zao zimechukuliwa bila kustahili na wanafunzi wa shule za Serikali, ambao, kwa kweli, hawajafanya vizuri kulinganisha na wale wa shule binafsi. Huu ni ubaguzi katika ngazi ya watunga sera," anasema Nderakindo Kessy.

Katika kubaini ni mwanafunzi gani ni Mkristo na ni yupi Muislamu, Dk Mvungi anasema TANLET imebaini kwamba majina ya wanafunzi hayatoi ushahidi wa dhehebu au dini ya mtu. Hayasemi chochote.

Badala yake, ushahidi wa kama ni shule ya Kikristo au ya Kiislamu, unatokana na umiliki wa shule yenyewe. "Hapa ndipo tumeweza kuona ni shule zipi ni za Kiislamu na ni zipi ni za Kikristo. Lakini majina ya wanafunzi hayathibitishi lolote kuhusu kuwapo kwa ubaguzi."

Kwa mujibu wa Dk Mvungi, shule za binafsi zilizofanya vizuri zinatoa picha kwamba kuna madaraja ya wanafunzi ambao wanalipiwa vizuri na walipaji wana uwezo wa kulipa ada kubwa. Kwa hiyo kadri uwezo wa kugharamia elimu unavyozidi kuwa mkubwa, ndivyo nafasi ya mwanafunzi kufaulu vizuri, inavyozidi kuwa kubwa zaidi. Hilo linajidhihirisha kwa kuwa hivi sasa kuna shule za Wakatoliki, ambazo zinatoza ada ndogo, na kwa hakika, matokeo ya shule hizo ni ya chini, ikilinganishwa na zile zinazotoza ada kubwa.

"Utafiti unaonyesha kwamba shule zenye matokeo mazuri, basi zina walimu wazuri. Na kama kuna walimu wazuri, ni wazi kuwa wanalipwa vizuri.Viwango vya ada ni jawabu la wanafunzi kufaulu vizuri, ingawa hii haina maana kwamba kiwango cha elimu kipo juu.

"Kiwango cha wanafunzi wengi kufaulu kutokana na kuwa na walimu wazuri, wanaolipwa vizuri, hakina uhusiano wowote wa kuwa na viwango vya juu vya elimu. Kufaulu sana hakuna maana kiwango cha elimu kipo juu," anasema Dk Mvungi.

Ni wazi kuwa shule zinazoongozwa na madhehebu ya dini na kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa, zinakuwa hivyo kutokana na mambo mawili: Mosi ni mazingira yake ya kuvutia walimu wazuri, na pili, ni kujenga na kulinda nidhamu ya wanafunzi wake.

"Hivi sasa utafiti wetu umebaini kuwa shule nyingi zinazomilikiwa na Wakatoliki, na ambazo zilikuwa ni mchanganyiko wa wasichana na wavulana, sasa zinaondolewa. Zinabaki ama zikiwa za wasichana watupu au wavulana tu.

"Hii inatokana na ukweli kwamba shule za mchanganyiko wa wavulana na wasichana ni vigumu sana kudhibiti nidhamu yake, wakati shule za wanafunzi wa jinsia moja ni rahisi kufanya hivyo," anasema Dk Mvungi.

Kati ya misitari mingi iliyokuwa katika mada ya James Mbatia, mimi nilivutiwa na dondoo iliyosema: "Namna nzuri ya kumsaidia masikini wa Kitanzania ni kumpatia mtoto wake elimu iliyo bora." Katika kutimiza azma hiyo, Mbatia akasema kwamba elimu kwa mtoto huyo wa masikini haina budi kutolewa katika kujenga mambo manne-maarifa, nidhamu, maadili ya kijamii na utamaduni wa taifa.

Katika mada hiyo, Mbatia anaainisha wazi mambo ambayo yanachochea kustawi kwa ubaguzi katika elimu, tofauti za maendeleo na uhasama miongoni mwa Watanzania.

Akachukua mfano wa shule za sekondari za mikoa ya Rukwa na Kigoma, mikoa ambayo ina jumla ya shule 133 za sekondari, zinazohudumia jumla ya wakazi 2,891,800 wa mikoa hiyo miwili, ikilinganishwa na Mkoa wa Kilimanjaro, wenye shule za sekondari 222 zinazohudumia wakazi 1,417,786 wa mkoa huo pekee. Ikumbukwe kuwa hizo ni takwimu za mwaka 2005.

"Idadi ya shule zote za sekondari za mikoa ya Rukwa na Kigoma ni ndogo kuliko zile za mkoa moja wa Kilimanjaro. Kwa uhakika zaidi kitakwimu, Mkoa wa Kilimanjaro una asilimia 67 zaidi ya shule za Kigoma na Rukwa, japo una nusu ya wakazi wa mikoa ya Kigoma na Rukwa," anasema Mbatia.

Katika kuainisha takwimu zaidi, imebainika kuwa shule zilizo nyingi, zinazoshika nafasi 10 za mwanzo, ama ni za jinsia moja au zinamilikiwa na madhehebu ya Kikristo, hususan, Wakatoliki. Za madhehebu ya Kiislamu zikiwa hazimo.

Tofauti na hilo, shule zilizo nyingi zinazoshika nafasi 10 za mwisho ni za mchanganyiko, yaani wavulana na wasichana, na baadhi ya shule hizo zinamilikiwa na madhehebu ya Kiislamu.

Kwa kuwa takwimu zinaonyesha bayana, kwamba kuna tofauti kubwa katika viwango vya kufaulu na kujitambua kwa watoto, Serikali na jamii kwa ujumla ni lazima zijifunze kutoka kwa Wakatoliki, mbinu na vigezo wanavyotumia ili viweze kutumika ili kuimarisha shule zote kwa maslahi ya Taifa.

Kwamba, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha inayapatia ruzuku madhehebu ya dini ili yaendelee kutoa huduma nzuri ya elimu ya jamii. Pia ni wajibu wa Serikali kutumia raslimali za taifa kwa uwazi, kuhakikisha tofauti bayana na zisizo bayana, zilizopo katika elimu hapa nchini, zinapungua au kumalizika kabisa.

Pengine uchungu na utetezi wa Dk Mvungi kuhusu haki na usawa katika utoaji wa elimu nchini, unatokana na historia yake binafsi na malezi aliyoyapata tangu utotoni, hadi akafikia ngazi ya chuo kikuu.

Dk Sengondo Mvungi alikulia katika maisha ya kawaida, katikati ya jamii ya wakulima, huko Kisangara Juu, katika Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro. Ni mtoto wa pili kutoka kitindamimba katika familia ya watoto saba. Na kwa hiyo, baba yake alikuwa ni mkulima, aliyestawisha kahawa, mahindi, ndizi, mihogo na maharage. Pia mzee huyo alikuwa mfugaji, akitunza ng'ombe wa maziwa.

"Kwa hakika tulikuwa pia na mbuzi na jukumu langu mojawapo katika utoto wangu lilikuwa ni kuchunga hawa mbuzi na ng'ombe waliokuwapo. Baba yangu alinifundisha jinsi ya kulima, namna ya kulitumia jembe, panga na shoka. Alinifundisha jinsi ya kuenenda kama binadamu katika jamii ile ya wakulima," anasema Dk Mvungi.

Baba yake pia alimfundisha jinsi utamaduni wa jamii yao ulivyo. Alimfundisha pia maadili mazuri, heshima kwa wakubwa na wengine. Lakini pia Dk Mvungi anasema kwamba baba yake alimfundisha jinsi ya kuwatunza na kuwatetea wanyonge, kutumia uwezo wake wote. "Kwa hiyo sikuweza kuvumilia kuona mtu akionewa. Na hivi ndivyo nilivyokuwa hadi leo. Lakini jambo la ajabu ni kwamba baba yangu hakuniandaa hata kidogo kuwa kiongozi wa aina yoyote ile."

Hata hivyo, Dk Mvungi alionja uongozi pale alipoingia shule ya msingi, ambako alikuwa ni kaka mkuu wa shule. Katika shule ya sekondari alikuwa ni kiongozi mkuu wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kigoma. Akiwa Shule ya Sekondari ya Mzumbe pia alikuwa ni kiongozi wa wanafunzi.

"Nilipojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wazazi wangu, kwa hakika kabisa, walipinga sana hatua yangu ya kugombea uongozi chuoni, kwa kuwa walihofia ningehusika katika migogoro ya wanafunzi.

"Hata hivyo, nilichaguliwa wakati mimi mwenyewe sipo,kuwa katibu wa serikali ya wanafunzi. Nililichukua jukumu hilo, na` huo ukawa mwanzo wangu wa uongozi katika kiwango cha juu. Lakini sikuwahi kufikiria kwamba siku moja ningekuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano."

Dk Mvungi alikuwa ni mmoja wa wagombea urais wakati wa uchaguzi mkuu wa 2005, akiwa amebeba bendera ya NCCRMageuzi. Ilibidi aache ajira yake ya kufundisha katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa mujibu wa sheria za nchi.

Hata hivyo, baada ya uchaguzi kumalizika, Dk. Edimund Adrian Sengondo Mvungi alirejea wadhifa wake katika chuo hicho, akifundisha na kupambana na mambo mengine, kama hili la kufanyia utafiti wimbi la kuibuba kwa matabaka katika sekta ya elimu nchini.

Amelifanikisha suala hilo kupitia TANLET, angalau kwa kuwekana sawa pale jahazi la elimu linapokwenda mrama. Ni juu ya mamlaka husika kuufanyia kazi utafiti huu ili kuwa na mustakabali mwema wa elimu katika nchi.

1 comment:

Anonymous said...

Profesa Kighoma Ali Malima alilizungumzia hili akaoneka mdini. Leo linazungumzwa na wataalamu tena Wakristo!