Hatua 5 zitakazomfanya mpenzi aliyekuacha akurudie
Kabla sijasema ninachotaka kukueleza hebu kwanza nimshukuru Mungu kwa mema ambayo amenifanyia tangu nilipokutana nanyi kwenye ukurasa huu wiki iliyopita, ninaamini ni Mungu pekee aliyenilinda na kunitia nguvu za kuwepo hadi wasaa huu ninapoikamata kalamu yangu mkononi na kuandika makala haya.
Baada ya kusema hayo hebu sasa nirejee kwenye mada yangu ya leo ambapo nitaongea nanyi juu ya hatua tano muhimu zinazoweza kukusaidia kukutoa katika machungu na endapo utazifuatilia kwa umakini na kuzifanyia kazi basi kwa hakika utafanikiwa kulipata tena penzi la mwenza wako unayempenda kwa dhati licha ya yeye kukuacha. Fuatilia kwa umakini...
Kama ujuavyo kuna ugumu mkubwa kuuteka upya moyo wa mwenza wako aliyekutoa akilini na kufuta hisia zote za mapenzi dhidi yako, inaweza kuwa rahisi endapo tu itagawanywa katika hatua tano ambazo zinaweza kuwa muongozo bora na rahisi kukufanya usahau yaliyotokea na kuishi maisha yako ya kawaida kama hapo awali “getting your life back on track.” Nitajitahidi kuelezea hatua zote tano katika hali itakayokufanya uzielewe kila kitu unachohitaji kufahamu kupitia hatua hizi zifuatazo:
Hatua ya kwanza; Usiharakishe kupigania akurudie.
Hili ni kosa ambalo wengi hulifanya, unapaswa kufahamu kuwa mpenzi wako mara baada ya kuachana na wewe huwa katika kipindi ambacho hahitaji kusikia lolote kutoka kwako. Mpe muda na nafasi yakuweza kurudi katika hali yake ya kawaida kwani msongo wa mawazo kwa walioachana humsonga aliyeachwa na aliyemuacha mwenzie pia.
Hatua ya 2: Katika kipindi cha upweke tafakari kilichosababisha kutengana. Ukishafanya tafakuri yako jiulize ni mambo gani ambayo wewe unawajibika nayo yaliyosababisha mkatengana? Jinsi gani unaweza kuweka mambo sawa ili yasije kusababisha matatizo tena katika uhusino wako? Haya ndio mambo ambayo unapaswa kufikiria na zaidi kuhakikisha hurudii tena makosa yaliyomtibua mwandani wako hadi akaona huna umuhimu tena katika nafsi yake na kukuacha.
Hatua ya 3: Baada ya muda wakutosha kupita na akili yako kutengemaa, unaweza kuwasiliana na mwenza wako aliyekuacha. Hata hivyo, unapaswa kuhakikisha mawasiliano yenu yanakuwa ya kawaida na unayoyamudu, unaweza ukampigia simu, kumtumia sms au barua pepe ukitaka kujua anaendeleaje. Katika kipindi hiki hupaswi kumueleza moja kwa moja kuwa unamuhitaji maishani mwako kwa kumueleza mambo matamu, usifanye papala fanya mambo taratibu.
Hatua ya 4: Baada ya kurejesha mawasiliano taratibu pasipo ugomvi, yawezekana kabisa mkajikuta mnatumia muda wenu pamoja kama zamani. Hakikisha unatumia kipindi hicho kufanyiana mambo mbalimbali ambayo una hakika enzi za uhusiano wenu yaliwafanya wote mfurahie kikamilifu. Kwa kufanya hivyo itawasaidi kuamsha kumbukumbu na hisia za penzi lenu la zamani na itampa nafasi mpenzio kubaini mabadiliko uliyofanya katika mambo yaliyosababisha kukuacha na kwa kumshawishi kwa jinsi hii kunaweza kumfanya ashawishike zaidi kukupa nafasi ya pili ndani ya moyo wake.
Hatua ya 5: Kama yote uliyomfanyia mwenza wako yamekusaidia kumrudisha katika himaya yako akikupa nafasi nyingine tena kuweza kudumisha penzi lenu, sasa kinachofuata ni hatua mojawapo muhimu sana ambayo ni kuhakikisha unamkamata vema na kumfanya ahisi uamuzi wake aliotaka kuchukua angeujutia daima! Shikamana na usilegelege hata kidogo kwani ukimkosa kwa mara nyingine hutaweza kumshawishi kwa namna yoyote kukurudia.
Hivyo mara zote kumbuka kwamba kujitoa muhanga na maelewano ndio nguzo pekee za uhusiano ulio imara. Kila mtu ana mahitaji ambayo ni lazima ayatimize, na wewe ndiye unayehusika moja kwa moja na mwenza wako. Kutilia mkazo na kumsaidia mwenza wako kutimiza ndoto na malengo yake haraka ndio njia ya haraka na sahihi zaidi ya kumfanya mpenzi wako aliyekuacha kushawishika kurejea kwako.
Unayaonaje makala haya?
Kama una chochote, ushauri, maoni juu ya kile nachokiandika cheki nami kwa
Na. 0715 888887,
email:brazatk@yahoo.com au
http://mwakilaga.blogspot.com
Kutoka: Global Publishers Tanzania.
No comments:
Post a Comment