Monday, February 04, 2008

CCM Miaka thelathini na moja 1977 - 2008

JK akiwapungia wanachama wa CCM Pemba katika uwanja wa Gombani jana. kulia Rais Amani Abeid Amani Karume wa Zanzibar.
Picha kwa hisani ya http://issamichuzi.blogspot.com/



Mama Salma Kikwete na Mke wa Rais wa Zanzibar mama Shadya Karume wakati wa sherehe za miaka 31 ya kuzaliwa CCM huko uwanja wa michezo Gombani Pemba jana.
Picha kwa hisani ya http://issamichuzi.blogspot.com/


JK akitoa hotuba katika maadhimisho ya sherehe za miaka 31 ya kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi katika uwanja wa Michezo wa Gombani Pemba jana.



Viongozi wasio waadilifu

wametuponza -

Jakaya Kikwete


Habari LEO
; Monday,February 04, 2008 @00:02


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amesema imani ya wananchi kwa viongozi inaanza kupungua kutokana na ukosefu wa uadilifu na uaminifu, hali ambayo inahitaji kushughulikiwa haraka kabla hali haijawa mbaya.

Kikwete alionya jana Chake Chake, Pemba, kuwa suala la kutokuwa waadilifu linasumbua na kuudhi wananchi, hali inayowafanya wawe na chuki, kukosa imani na hata kuwapotezea heshima viongozi pamoja na chama.

Akitoa hotuba yake katika maadhimisho ya miaka 31 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uwanja wa Gombani, alitahadharisha kuwa upo uwezekano wa kiongozi kufanya mambo mengi mazuri, lakini iwapo uadilifu wake hauridhishi, ataendelea kukataliwa na wananchi.

Akikumbushia uamuzi alioutangaza hivi karibuni wa kuwadhibiti viongozi wa kisiasa wanapokuwa madarakani kutokujishughulisha moja kwa moja na biashara, Rais Kikwete alisema hilo ni miongoni mwa mambo yanayopunguza imani. “Imani ya viongozi na wananchi inaanza kupungua.

Na inawezekana yanayotufanya tupunguze imani ni mambo haya. Na mtaji wetu viongozi ni wananchi kuwa na imani na sisi. Siku wakipoteza imani na sisi, mjue tumekwisha. Na uhai wetu unatoweka. Tunataka tuendelee kuaminiwa na kupewa ridhaa,” alisisitiza.

Aliendelea kuonya, “Haya tusipoyafanya, tutafanya mambo mengi mazuri, ya barabara, ya maji, ya umeme, ya kuwapa maziwa na asali, lakini ukienda pale ukaona bado wanakataa, kumbe kinachowaudhi sasa wanajadili uadilifu wako, wanajadili uaminifu wako.” Alisema sheria ya kuzuia mawaziri na wabunge kufanya biashara itakapopitishwa, hakuna haja ya wanasiasa hao kuwakabidhi watoto wao mali kwa kificho, bali wanatakiwa kutamka wazi, ili mali hizo zikabidhiwe kwenye dhamana ili kuepusha migongano ya maslahi.

Alisisitiza, “Hunyanganywi mali yako wala kumkabidhi mwanao kwa kificho. Unatamka wazi, hoteli hii mali yangu, daladala 10 za Dar es Salaam kwenda Gongo la Mboto ni zangu.” Kwa mujibu wa Kikwete, sheria ya kuzuia wanasiasa hao kufanya biashara, itaepusha manung’uniko ambayo yamekuwa yakitolewa huku yakiwahusisha viongozi na shughuli mbalimbali.

“Manung’uniko ya watu tunayasikia (vinginevyo tunaishi dunia ya mbali) wanavyotuhusisha sisi na shughuli hii na shughuli ile. Ndiyo maana nimesema jambo hili tukae tulitafakari vizuri,” alisisitiza. Alisema Ibara ya 110 ya CCM inasisitiza suala la maadili na hivyo, mwaka huu, uwe wa kusimamia kikamilifu maadili ya viongozi wa chama na serikali.

Kuhusu uhusiano mbaya kati ya CCM na Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Kikwete alisema chanzo cha tatizo siyo chama chake kwa kuwa chenyewe kinaongoza nchi na hakina maslahi katika kugombana. Alisema CCM ina maslahi katika kupatana na ndiyo maana ilikuwa ya kwanza kupendekeza mazungumzo ya mwafaka kwa dhamira ya kubadilisha uhusiano huo wa kihasama ili uwe katika misingi ya kidemokrasia.

Katika kuelezea kukerwa kwake na siasa za chuki kugeuzwa mazoea, Rais Kikwete alisema baada ya mazungumzo yanayoendelea ambayo yako mbioni kukamilika, inabidi liwe fundisho ili hali hiyo isijirudie. Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo wa CCM amepiga marufuku wagombea katika chaguzi ndani ya chama hicho, kukusanya wajumbe kwa lengo la kuzungumza nao kabla ya uchaguzi kwa lengo la kuwashawishi wawapigie kura.

Alikuwa akizungumzia uchaguzi ngazi ya Jumuiya, unaotarajiwa kufanyika mwaka huu. “Safari hii marufuku kumuita mjumbe yeyote. Na tutakuwa makini..mliozoea hayo muache, atakayeitisha huo mkutano uongozi hautaki,” alisema Kikwete.

Katika sherehe hizo, Kikwete alitaja majukumu saba ya msingi yatakayotekelezwa na chama chake mwaka huu kuwa ni pamoja na kutekeleza Ilani, kuimarisha uhusiano na vyama vingine vya siasa, maadalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Wapigakura, Kuendelea kusimamia maadili ya viongozi na uongozi, Uchaguzi wa jumuiya, na Kutekeleza mradi wa kuimarisha Chama.


No comments: