Friday, February 08, 2008

Hotuba ya Lowassa jana Bungeni

Mh Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa
Tanzania akitoka nje
ya ukumbi wa B mjini
Dodoma hapo jana baada ya kutangaza rasmi
kujiuzulu
wadhifa huo picha na Edwin Mjwahuzi.

IFUATAYO ni hotuba fupi aliyoitoa Waziri Mkuu Edward Lowassa katika Bunge mjini Dodoma jana (Alhamisi Feb. 7, 2008) asubuhi, wakati wa mjadala wa Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Mchakato wa Zabuni ya Kuzalisha Umeme wa Dharura Ulioipa Ushindi "Richmond Development Company LLC" ya Huston, Texas, Marekani mwaka 2006:


"Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunifanya msemaji wa kwanza katika hoja hii.

Lakini la pili, nimpongeze Dk. Harrison Mkwakyembe, Mwenyekiti wa kamati Teule kwa kuwasilisha kwa mbwembwe nyingi sana taarifa yake, mbwembwe zilikuwa nzuri kweli.

Kwa kazi nzuri kwa maoni yao, wamewasilisha vizuri. Lakini nimesimama kuweka kwenye kumbukumbu kutoridhika kwangu na jinsi kazi hiyo ilivyofanywa. Mheshimiwa Dk. Mwakyembe ni Mwanasheria, tena Daktari alikuwa anafundisha Chuo Kikuu. Moja ya vitu alivyokuwa anafundisha ni "Natural Justice".
Mheshimiwa Spika, wewe ni Mwanasheria unafahamu suala la Natural Justice.

Kwamba Kamati Teule imesikiliza watu wengine wote pamoja na wanaoita minong'ono ya mitaani, wamesafiri mpaka Marekani kutafuta mashahidi, lakini mimi ambaye ni mmoja kati ya watuhumiwa mle hawakunihoji hata siku moja.Mheshimiwa Spika, nimesimama kueleza masikitiko yangu. Ofisi ya Bunge mpaka ofisini kwangu hata kama wangeniita ningekwenda kwa miguu kama hamna gari na nilikuwa tayari kufanya hivyo.

Hawa ni watu makini sana siwezi kuamini kwamba wanaweza wakafanya oversite kama hiyo. Kwa sababu katika kila hoja walizojenga wamesema Waziri Mkuu ilikuwa hivi. Kulikuwa na shida gani kuja kuniuliza Waziri Mkuu wanasema uliotoa dokezo hili ni sawa sawa kweli? Kulikuwa na shida gani kwa mfano kufuata utaratibu wa Westminster kuthibitisha hapo unaposema mwenye Richmond ni fulani uka-lay on the table records na ushahidi kuwa ni fulani.

Mheshimiwa Spika, Taifa letu ni Taifa changa, lakini chombo hiki ndiyo mahali pa demokrasia pakubwa katika nchi pote, hapa ndipo penyewe. Kama katika chombo hiki haki haitaonekana kutendeka nchi yetu haitakwenda vizuri. Hapa ndipo tunategemea tuwaonyeshe umakini wetu, umahiri wetu katika mambo ya demokrasia. Kwa nhiyo nilichofanyiwa napenda kuweka kumbukumbu sawa kwamba naona si sahihi, nimefadhaika sana, nimedhalilishwa sana, nimeonewa sana katika hili.

Maana zimechukuliwa tuhuma zikaelezwa hapa kwamba hivi ndivyo ilivyo. Mimi sijauliza. Kulikuwa na shida gani kuniuliza, kwa nini muamini minong'ono ya mitaani kuliko maelezo yangu. Sisi wote hapa ni wanasiasa tukianza kuamini minong'ono ya mitaani niambieni mwanasiasa atakayesimama. Hatuwezi, Tume imepewa muda wa kutosha lakini inashindwa kumuona mtu ambaye wanamtuhumu na wanamsema kwa kirefu sana.

Mheshimiwa Spika, lakini hata pale uliponinong'oneza ukaniambia una ushahidi wowote? Nilikupa ushahidi huo wa maandishi. Katika taarifa yao hakuna hata moja ya ushahidi ambao umetoka Waziri Mkuu. Kile kitabu cha majedwali kimejaa majedwali mengi pamoja na magazeti mpaka ya Udaku lakini maelezo ya Waziri Mkuu hakuna hata moja.

Mheshimiwa Spika, naamini ingekuwa ni heshima wangeiweka halafu wakasema tunakataa kitambulisho hiki kwa sababu hii na hii, hiyo ndiyo imejengwa hoja. Lakini kujenga hoja na kuja hapa Bungeni tunahutubia nchi nzima na kusema Waziri Mkuu amefanya hiki, amefanya hiki bila ya kumsikiliza nachelea kuuliza hivi mtu wa chini itakuwaje?

Mheshimiwa Spika, lakini nimetafakari kwa makini sana jambo hili nikajiuliza hivi kulikoni mpaka watu wazima wenye uwezo wao, watu maarufu wenye heshima zao, mpaka wafike mahali waache jambo la msingi kama hilo kulikoni? Mimi nadhani there is a wish which I am going to grant, ni Uwaziri Mkuu. Nadhani tatizo ni Uwaziri Mkuu. Kwamba ionekane Waziri Mkuu ndio amefanya haya, tumuondolee heshima au tumwajibishe.

Mheshimiwa Spika, nimetafakari kwa niaba ya chama changu, kwa niaba ya Serikali yangu nimeamua kumwandikia Rais barua ya kumwomba niachie ngazi. Nafanya hivyo kwa moyo mweupe kabisa ili kuonyesha dhana ya uwajibikaji lakini kutokubaliana na utaratibu uliotumika kusema uongo ndani ya Bunge wa kumsingizia mtu.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais kwa heshima aliyonipa ya kutumikia nchi hii kwa Uwaziri Mkuu kwa miaka miwili. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Nakushukuru wewe, nawashukuru Mawaziri na Manaibu Waziri, nawshukuru Waheshimiwa Wabunge na wanachama wa CCM tuliyosimamia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nashukuru".


Kutoka: http://haki-hakingowi.blogspot.com/


2 comments:

Anonymous said...

Du! Mbona muheshimiwa hapa anaonekana hana nguvu?Huo mwendo! Na mapaparazi wanae!

Anonymous said...

Si mchezo, si kazidiwa na kuuacha Uwaziri Mkuu kwa kuambiwa atangaze mwenyewe kuwa anajiuzulu kuliko kuumbuliwa kwa kufukuzwa kazi....