Sunday, November 02, 2008

“Sambusa ni tamu”

Nipeni kiti nikae, nikae na niteteme,
Ndugu msinishangae, nililonalo niseme,
Ya chakula cha ukae, maneno yangu nipime, 
Sambusa ni tamu bwana, hasa za kitanzania!

Nilialikwa na Rozi, Fatuma naye Amina,
Nikawa kama balozi, mlaji mwenye amana,
Hawakupika mbaazi, bali sambusa kwa sana,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Ilikuwa tafrija, ya vyakula vya nyumbani,
Chakula kimoja moja, kikajapangwa mezani,
Mtori sinia moja, na pilau mdalasini
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania.

Pembeni wali wa nazi, na nyama ya binzari,
Bakuli ya maandazi, yaliyopikwa vizuri,
Sikuifanya ajizi, wa kijiji sina shari,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za kitanzania!

Vyote hivyo sikutaka, nilichotaka sambusa,
Kuleni mnavyotaka, wadada niliwaasa, 
Mkila mlivyopika, niachieni sambusa,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Ndipo nikala za Rozi, sambusa zilivoiva,
Nilikula kama chizi, kama ninakula mbeva,
Nikatafuna kwa pozi, utadhani mi dereva,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za kitanzania!

Ndipo kaleta Fatuma, sambusa kanigawia,
Ulimi nikajiuma, utamu kuniingia,
Nikakumbuka Dodoma, Sambusa zake Sofia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Ndipo akaja Amina, sambusa kunipatia,
Funga kazi kiaina, jinsi kanipakulia,
Nikala tena na tena, manusura kuzimia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Kama hujala sambusa, hasa za Kitanzania,
Hujui unachokosa, utamu wauachia,
Jaribu hata Mombasa, bure watakupikia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania.

Si fumbo nililosema, msianze kuwazia,
Wajanja mkalalama, kusema nawafumbia,
Yote niliyoyasema, ni sambusa nasifia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania

Kaditamati natama, beti haziendi tena,
Kapiga simu Rehema, mwaliko katoa jana,
Juma lijalo kasema, ni kwake kwenda jichana,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Na M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)

No comments: